Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya
 Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za Serikali wameanza kupokea mishahara mipya huku wale wa sekta binafsi wakiendelea kupata mishahara ya zamani.
 
Ijumaa, Serikali ilitangaza viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi wa taasisi zake ikiwa ni wiki tatu baada ya kutangaza viwango vya chini  vya mishahara katika sekta mbalimbali binafsi.
Kima cha chini katika taasisi za Serikali kimepanda kutoka Sh170,000 hadi Sh240,000 huku wengine ikipanda kwa asilimia nane wakati sekta binafsi viwango hivyo,ni vile vilivyotangazwa na Serikali vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine kwa kuanzia Sh40,000 hadi Sh400,000.
  Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti hasa baada ya gazeti hili kuandika habari za mishahara kwa sekta zote, baadhi ya wafanyakazi  wa taasisi za Serikali walidai kupata mishahara mipya wakati ile ya binafsi bado.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema ana matumaini walimu wataanza kupokea mshahara mpya mwezi huu.
“Pamoja na kwamba mishahara bado haijalipwa lakini tumehakikishiwa kwamba marekebisho yameshafanyika kwa ajili ya walimu kuanza kupokea mishahara mipya mwezi huu wa Julai,” alisema Mukoba.
Aliongeza, “suala kubwa kwetu si kuanza kupokea viwango vipya vya mishahara mwezi huu, tunachojadili sasa kiasi kilichopandishwa, tunaendelea kufanya vikao kulijadili.”
Wafanyakazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wao wameshapokea mishahara mipya kama ilivyotangazwa. “Ni kweli mwezi huu nimepokea mshahara mpya,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao ambaye aliomba jina lisitajwe gazetini. 

Mfanyakazi mwingine wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alisema ingawa bado hawajapewa mishahara mipya lakini wamehakikishiwa kuwa wataanza kupokea mwezi huu.
“Idara ya Uhasibu wamepewa majedwali ya viwango vipya vya mishahara hivyo wanafanya kazi hadi usiku kuvibadilisha na wametuhakikishia tutapewa utakapomalizika mwezi huu,” alisema.
Miongoni mwa walimu hao ambao wana shahada walisema wana imani ya kupokea Sh600,000 badala ya Sh532,000 walizokuwa wakizipata awali.
Kwa upande wa polisi nao ni miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali walioanza kupokea mishahara mipya kuanzia mwezi huu.

Sekta binafsi
Hata hivyo wafanyakazi wa sekta hiyo waliohojiwa walisema hawaoni dalili za kupokea mishahara mpya mwezi huu huku wengine wakikiri kuendelea kupokea mishahara ya zamani.
“Pamoja na kwamba bado hatujalipwa mishahara, taarifa nilizonazo ni kwamba tutaendelea kulipwa mishahara ileile ya zamani,” alisema kwa simu mfanyakazi wa kiwanda cha Kioo Ltd.
Kauli hiyo iliungana na mfanyakazi wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) aliyesema wamelipwa mishahara ya zamani.
“Tumeshalipwa lakini ni ile ile ya zamani, hatuoni dalili za kupandishiwa mishahara,” alisema mfanyakazi huyo aliyeomba asitajwe jina lake.  Mfanyakazi mwingine katika Kiwanda cha Namera alisema wameshalipwa mishahara lakini ni ile ya zamani.
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top