Maelfu ya waandamaji wakishinikiza Morsi aachiwe
Maelfu ya wafuasi wa kiongozi aliyeondolewa
madarakani nchini Misri, Mohammed Morsi wameandamana usiku kucha hadi
karibu na kambi moja ya kijeshi mjini Cairo kabla ya kurudi na kukita
kambi kando ya msikiti mmoja.
Hata hivyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na
jeshi licha ya onyo kutoka kwa waziri wa maswala ya ndani nchini humo
Mohammed Ibrahim, kwamba mamlaka itajibu vitisho vyovyote dhidi ya
usalama kutoka kwa waandamanaji hao.
Zaidi ya wafuasi 70 wanaotaka Morsi
kurejeshwa madarakani waliuawa baada ya ghasia kuzuka kati ya
waandamanaji na vikosi vya jeshi hapo Jumamosi.
Waziri wa mambo ya nje nchini humo amezitaka
pande zote kwenye mgogoro huu kujizuia na kusababisha ghasia, siku moja
baada ya ghasia nchini humo kusababisha vifo vya watu 70.
Kwenye mahojiano na BBC,Nabil Fahmy alisema kuwa pande zote zinapaswa kujizuia na kuchochea ghasia kwa kutumia vurugu.
Mnamo siku ya Jumamosi, wafusai wa aliyekuwa
rais Morsi, walikabiliana na polisi pamoja na maafisa wengine wa usalama
huku maelfu ya waandamanaji hao wakiendelea kupiga kambi.
Wakati huohuo, rais wa muda Adly Mansour amemuamuru waziri wake mkuu kulikabidhi jeshi mamlaka kuwakamata raia.
Mwandishi wa BBC Jim Muir ambaye yuko mjini
Cairo anasema kuwa baadhi ya watu wanaiona hii kama dalili ya wasiwasi
na mwanzo wa serikali kuanza kupambana na waandamanaji waliokita kambi
katika msikiti wa Rabaa al-Adawiya.
Waziri wa mambo ya ndani, Mohamed Ibrahim
amekuwa akionya mara kwa mara kuwa waandamanaji hao watatawanyishwa
karibuni , ingawa waandamanaji wenyewe wanasema hawatabanduka.
Kulikuwa na ghasia siku ya Jumapili, huku watu wawili wakiuawa mjini Cairo.
Mwishoni mwa wiki wapiganaji kumi wa kiisilamu
waliuawa na jeshi katika Rasi ya Sinai ambako wamezidisha mapigano kwa
mujibu wa shirika la habari la serikali la Mena.
Chanzo: BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment