Mwalimu
Dominicus Makukula(kulia) kutoka UDSM,Shule ya Uandishi wa Habari na
Hawasiliano ya Umma SJMC akifafanua jambo wakati wa
uwasilishaji,kushoto ni Mtafiti Ally Mohamed Kileo |
- Utangulizi
Utafiti
huu ulifanyika kama sehemu muhimu ya kukamilisha masomo yangu ya stashahada ya
juu katika kozi ya mawasiliano ya umma inayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Nilipanga kuhitimisha masomo yangu kwa kufanya kitu ambacho kingejenga
na kuimarisha wasifu wangu nikiwa msomi katika fani ya mawasiliano lakini pia
kufanya kitu ambacho kinatoa mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya nchi
yangu.
Katika
miaka ya hivi karibuni, kuanzia mwaka 2000 na kuendelea jamii yetu ya Watanzania
imeshuhudia migogoro mingi kati ya wanafunzi wa elimu ya juu hasa vyuo vikuu na
serikali katika upatikanaji wa mikopo ya kugharamia masomo. Upatikanaji wa
mikopo umekuwa kero kubwa na lawama nyingi zikielekezwa katika ufanisi mdogo au
mapungufu ya kiutendaji ya Bodi ya Mikopo. Wanafunzi ambao daima waliona au
kuhisi kutotendewa haki na serikali katika upatikanaji wa mikopo, kwa kupitia
vyama na serikali zao vyuoni wamekuwa wakifanya migomo na maandamano ya mara
kwa mara ambayo yameleta hasara na madhara makubwa katika kufanyika kwa
shughuli za kimasomo vyuoni. Wakati mwingine vurugu hizi zilizusha vitendo vya
uvunjifu wa amani na uharibifu wa miundombinu na samani za taasisi
walizosajiliwa kufanya masomo. Tumeshuhudia mara kadhaa kati ya mwaka 2005 hadi
2011 wanafunzi katika Chuo Kikuu kikongwe cha Dar es salaam wakifanya migomo
iliyosababisha vurugu na hatimaye chuo kufungwa huku wanafunzi wakisimamishwa
kwa muda na kurudishwa baadae kumalizia masomo yao. Wengine walifikishwa mbele
za vyombo vya dola kwa makosa yatokanayo na madai ya mikopo kupitia migomo hiyo
pamoja na wale waliofukuzwa kutoka chuoni moja kwa moja. Migogoro kati ya Bodi
ya Mikopo na Wanafunzi wa Elimu ya Juu imechangia kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa
maendeleo ya elimu ya juu hasa katika utekelezaji wa shughuli za kimasomo. Mihula
ya masomo huvurugika na kuwanyima walimu na wanafunzi muda wa kutosha kufanya
shughuli za kujifunza na ufundishanaji na zaidi kuyafanya mazingira ya vyuo
kukosa utulivu na amani kwa shughuli za kimasomo. Bodi kuna wakati imetumia gharama
kubwa na nguvu nyingi kukabiliana na matokeo ya madai ya wanafunzi badala ya
kuchunguza kiini cha tatizo na kulimaliza kwa usahihi na wakati.
Utafiti
huu maalum ulilenga katika kuchunguza matatizo ya msingi yanayoikabili Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hasa katika eneo la mawasiliano kupitia
teknolojia ya intaneti katika kuwahudumia wadau wake wakuu yaani wanafunzi (wakopaji),
na mwishowe kutoa mapendekezo ya kitaalamu ili kuiwezesha Bodi kutoa huduma
bora zaidi. Matatizo yaliyochunguzwa zaidi katika utafiti yalikuwa katika
mawasiliano wakati wa maombi ya mikopo ya karo na gharama za shughuli za
kimasomo hasa fedha kwa ajili ya kufanyia utafiti na mafunzo kwa vitendo.
Baada
ya kuzichunguza na kuzichambua taratibu na shughuli za kiutendaji za kila siku
za Bodi ya Mikopo, utafiti huu uligundua kuwa matatizo ni mengi na yote
yalianza katika mfumo mbovu wa mawasiliano ambao daima ulisababisha kuibuka kwa
migogoro mikubwa kati ya Bodi, Taasisi za Elimu ya juu (vyuo vikuu) na wakopaji,
yaani wanafunzi wa vyuo vikuu na hatimaye kufanyika migomo na maandamano ya mara
kwa mara.
1. A.
Dhana au Kanuni Zilizotumika Katika Utafiti
Utafiti
huu uliongozwa na kanuni mbili za utafiti ambazo ni:
1.
Njia au chombo cha kutolea habari
huathiri maana na jinsi ujumbe wa mawasiliano unaotolewa na muwasilishaji
(Medium Theory ya McLuhan, 1967) na;
(Medium Theory ya McLuhan, 1967) na;
2.
Kanuni au modeli ya mawasiliano ya
Shannon na Weaver ya mwka 1949.
Dhana
zote mbili zilitumiwa kwa kusudio la kumwezesha mtafiti kuchunguza jinsi na
namna mawasiliano yalivyofanywa na pande zote mbili (1. Bodi ya mikopo- Mtoaji taarifa na mpokeaji na 2. Wanafunzi – watoaji taarifa na wapokeaji pia)
katika mfumo wa mawasiliano wa Bodi ya Mikopo. Dhana ya kwanza ilitumika kama
darubini katika kuhizihakiki njia au vyombo vya habari vinavyotumiwa na Bodi ya
Mikopo kama vinafaa kubeba ujumbe unaokusudiwa na kuwawezesha walengwa wa
mawasiliano kuelewana. Mtafiti alizitumia kanuni hizi kuangalia usahihi wa
ujumbe, njia ya mawasiliano (chombo cha habari, kwa mfano : intaneti, gazeti, radio, t.v n.k), changamoto katika
kufanyika kwa mawasiliano (“ noise”-
visababishi vya kutokamilika kwa mawasiliano) na matokeo ya mawasiliano (
communication impact). Iwapo shughuli ya mawasiliano ilifanyika kwa kuzingatia
kanuni na dhana sahihi za kitaalamu ilitarajiwa kuwa ni rahisi kwa pande hizi
mbili za mawasiliano kufikia mwafaka kwa kila mmoja kujua nafasi yake na hata
kuona na kuelewa kwa urahisi matatizo ya kimawasiliano yaliyojitokeza na kwa
jinsi gani yangeliweza kutatuliwa au kusahihishwa kwa maelewano kati ya pande
zote mbili bila mvutano usio wa lazima.
B. Methodolojia
1. Muundo wa
Utafiti
Utafiti
huu ulifanyika katika misingi ya tafiti za taaluma ya sayansi ya jamii, na
kuakisi methodolojia isiyo ya kitakwimu. Katika metholojia hii matokeo ya
utafiti yametokana na ubunifu wa uchambuzi na tafsiri za mtafiti kutokana na
data iliyokusanywa na sio taarifa ya kitakwimu iliyotokana na data moja kwa
moja.
2. Sampuli ya Washiriki Katika Utafiti.
Utafiti
huu ulitumika sampuli wakilishi ya washiriki 45 ikiwa ni jumla ya wanafunzi 25
wa elimu ya juu, wafanyakazi 10 kutoka taasisi ya elimu ya juu na wafanyakazi
10 kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini. Sampuli ya washiriki
ilichaguliwa kwa kutumia mbinu inayojulikana kama “uchaguzi wa kupangwa au kwa
upendeleo” (purposive sampling). Kati ya washiriki wote 45, washiriki 35
walichaguliwa kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam na 10 waliobakia walitokea
Bodi ya Mikopo. Mtafiti aliona sampuli hii kwa tabia na idadi yake
ilijitosheleza kutoa picha halisi ya malengo ya utafiti.
3. Mbinu ya Ukusanyaji Data Katika Utafiti
Utafiti
huu ulitumia mbinu mbili za ukusanyaji wa data, nazo zilikuwa ni;
- Mahojiano ya uso kwa uso baina ya mtafiti na washiriki (moja baada ya mwingine kwa siri).
- Washiriki wa utafiti kujaza hojaji au dodoso la utafiti lenye maswali ya wazi kumwongoza mshiriki kutoa mawazo, mtazamo na uelewa wake katika tatizo la utafiti kama alivyohojiwa.
4. Uchambuzi wa Matokeo ya Utafiti
Taarifa
za utafiti au matokeo ya utafiti yaliainishwa kwa kutumia maswali mawili ya
utafiti yaliyohoji: 1. Ni aina gani ya mfumo wa mawasiliano unatumiwa na Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya Juu? 2. Kwa jinsi gani mfumo wa mawasiliano wa Bodi ya
Mikopo unasaidia au kuathiri huduma za Bodi kwa wadau wake?. Maswali haya
yalifafanuliwa na kurahisishwa katika maswali madogo manne ili kuwawezesha
washiriki kuyajibu kwa ufasaha kupitia dodoso la utafiti. Katika hatua
iliyofuata, majibu ya washiriki katika madodoso yote 45 yaliyochambuliwa, kuainishwa
na kupangiliwa katika maudhui yaliyofafanuliwa na kuelezea tatizo la utafiti na
kuwasilishwa katika mjadala na majedwali yenye kutoa takwimu fupi za matokeo ya
utafiti.
- Matokeo ya Utafiti
Utafiti
uligundua kuwa tatizo kuu ni mfumo wa mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
juu ya Tanzania. Japokuwa, Bodi ya Mikopo imejiwekea utaratibu wa kutumia njia
au vyombo mchanganyiko katika kufanya mawasiliano na wadau wake, bado matatizo
ya kimawasiliano yamekuwa makubwa na kusababisha shida nyingi baina ya wadau wa
Bodi.
Asilimia
55 (washiriki 25) ya washiriki wote 45 (100%) katika utafiti walisema kuwa,
matumizi ya intaneti, vipeperushi, matangazo ya kubandikwa, matangazo ya redioni
na katika televisheni kama njia za mawasiliano bado hazijaiwezesha Bodi kutoa
au kufanya shughuli za mawasiliano vizuri na kwa wakati baina yake na wadau
wake katika kutoa huduma sahihi na kwa haraka. Katika kuchunguza matumizi ya
mtandao wa intaneti kama chombo kikuu cha mawasiliano (jambo ambalo limechukua
nafasi kubwa katika utafiti huu), mtafiti aligundua mapungufu makubwa zaidi
kama inavyoainishwa hapo chini:
- Kukosekana kwa ubunifu na matumizi madogo ya njia ya mawasiliano ya intaneti
Washiriki
13 wote kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ambapo 3 ni wanafunzi wanaoendelea na masomo, 9 wanafunzi wapya na kiongozi mmoja kutoka umoja wa wanafunzi DARUSO (Dar es Salaam Students
Organization ) walisema, kuna
matatizo katika matumizi ya
njia ya mtandao wa intaneti kwani
hawakuona tofauti kati ya tovuti ya Bodi na bango au tangazo la kubandikwa. Washiriki
walisema walitarajia tovuti hiyo
kusheheni taarifa nyingi, sahihi na za
kina katika kumwezesha mdau (mwombaji)
wa Bodi ya Mikopo kupata taarifa
zote na kukidhi mahitaji yake awapo
mtandaoni bila kulazimika kwenda
Bodi ya Mikopo kwa ajili ya
shughuli hiyo hiyo.
- Urasimu usio wa lazima
Vilevile,
washiriki 25 wote wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Dar es salaam, kati yao wakiwemo viongozi 5 wa DARUSO,
wanafunzi 10 wanaoendelea na masomo ya juu na 10 wapya (waliotarajia
kujiunga na Chuo kikuu cha Dar es
salaam) walilalamikia mlolongo wa
taratibu zilizowekwa ili mwombaji wa
mkopo kufanikisha usajili wake katika Bodi. Kutokana na utaratibu mbovu wa utunzaji wa kumbukumbu za watu
katika mfumo mzima wa elimu wa Tanzania,
Bodi imeweka urasimu mgumu wakati wa
kuzipata taarifa za mwombaji mpya. Utaratibu wa Bodi unahusisha
vyombo au taasisi zisizosaidia kwa
namna yoyote ile
kumtambulisha mwombaji kwa
usahihi; Kwa mfano, katika hili
unatolewa katika kipengele cha ithibati ya serikali ya mtaa anaoishi mwombaji inayohitajika ili
kumtambulisha mwombaji kwa Bodi.
- Kuchelewa kwa majibu ya maswali au maelezo yatokanayo na zoezi la usajili
Katika
hili, washiriki 25 wote wanafunzi wa
chuo kikuu cha Dar es Salaam, kati yao
wakiwemo, viongozi 5 wa DARUSO, wanafunzi 10 wanaoendelea na masomo na
10 wapya waliotarajia kujiunga na
Chuo Kikuu cha Dare s salaam walisema,
walitegemea mtandao wa intaneti
ungelirahisisha upatikanaji wa huduma za
Bodi ya Mikopo na badala yake hawaoni tofauti
yoyote kati ya matumizi ya matumizi ya mtandao wa intaneti na mfumo
wa zamani wa taarifa /mawasiliano kufanyika kupitia mbao za matangazo za Bodi na chache zilizopo katka Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Viongozi
wa DARUSO walibainisha kuwa maswali yao kuhusu taratibu za utoaji wa mikopo
panapotokea ucheleweshwaji, Bodi huchukua muda mrefu kujibu toka muda ule mdau anapouliza.
Vilevile, hata taarifa muhimu juu ya upatikanaji wa mikopo hazipatikani kwa
wakati zinapohitajika kulingana shughuli za kimasomo chuoni. Wanafunzi 7
wanaoendelea na masomo walisema hawakuwahi kujibiwa maswali yao waliyouliza
kupitia anuani ya baruapepe iliyowekwa mtandaoni wala kupatiwa au kutumiwa
taarifa walizoomba kupitia tovuti ya Bodi ya Mikopo.
- Kukosekana kwa uwazi na ukweli katika mchakato wa kupanga mikopo
Utafiti
ulionyesha katika tatizo hili tovuti ya Bodi ya Mikopo imepoteza maana zaidi
kwa kushindwa kutumika kwa ufanisi uliotarajiwa. Washiriki wote 25 wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti huu walisema kuwa, hili ni moja
katika matatizo makubwa yanayoonyesha utendaji wa Bodi unayokosa haki, ukweli
na uwazi kwa waombaji. Washiriki wa utafiti walisema ingekuwa rahisi sana Bodi
kuonyesha matokeo ya mwombaji na madaraja ya mikopo wanayopangiwa wadau kupitia
mtandao wa intaneti kuliko ilivyokuwa siku za nyuma. Teknolojia ya intaneti
ingeiwezesha bodi kuainisha mchakato wote wa upangaji na utoaji wa mikopo kwa
uwazi mkubwa huku kila mwombaji na sifa
zake zikionekana na kupatikana kwa urahisi mtandaoni, lakini jambo hilo
halifanyiki kwa kuzingatia teknolojia tuliyonayo na ubabaishaji bado unandelea
kujitokeza. Hapa mtafiti alitia shaka (observe) kuwa, inawezekana bado Bodi ya
Mikopo inakosa wataalamu wa teknolojia ya mtandao katika mawasiliano ya Umma pamoja
na vyombo vyake.
5. Kukosekana kwa ushirikiano katika
mawasiliano kati ya Bodi ya Mikopo na wadau wake
Mwishowe,
washiriki wote 45 (100%) walikubali kuwa Bodi ya Mikopo haitumii mtandao wa
mawasiliano katika njia inayowakutanisha na wadau wake kwa wakati (interactivity).
Mtafiti aliona tatizo hili kuwa ni la kiufundi zaidi na hivyo kubainisha mawazo
ya washiriki walioona kuwa bado Bodi ya Mikopo inaendelea kutumia njia moja ya
mtiririko wa mawasiliano (Linear communication) isiyoshirikisha (kinyume na
matarajio ya matumizi ya mtandao wa intaneti) walengwa katika mchakato wa
mawasiliano pindi taarifa/mawasiliano yanapofanyika, na hivyo kufanya yasitimie
kwani panakosekana mrejesho (Feedback) baina ya wanamawasiliano kwa wakati.
Mrejesho katika mawasiliano ungelikamilisha shughuli ya mawasiliano mara moja
iwapo pande mbili za mawasiliano zingeshirikishwa kupitia mtandao kama vile
kuchati (instant messaging) au kuwapo kwa kitengo cha mawasiliano ya simu cha
huduma kwa wateja (Student Call Centre) kama ilivyo katika huduma za makampuni
ya simu za kiganjani.
Hitimisho
Kwa
ufupi sana utafiti huu umegundua kukosekana kwa taaluma, wataalam na maana
sahihi ya matumizi ya mtandao wa intaneti katika shughuli za Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu. Katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwenye teknolojia ya
utoaji wa mikopo ya elimu kwa kutumia mtandao wa inteneti kama Afrika ya Kusini
na Botswana shughuli zinazotuchukua muda wa siku mbili sisi Watanzania, wao
huwachukua masaa machahe kuzikamilisha. Utafiti huu pia ulibaini sio tu uzembe
wa watendaji katika vitengo mbalimbali vya Bodi vimefanya huduma za Bodi hiyo
kuwa duni na mbaya, lakini pia kukosekana kwa nia ya dhati ya kuboresha huduma
za Bodi ya Mikopo kunafanya zoezi zima la matumizi ya mtandao wa intaneti kutoa
huduma kuwa kama mchezo wa kuigiza usio na
waigizaji wala watazamaji sahihi. Ni changamoto kubwa kwetu wasomi wa fani
mbalimbali zenye mahusiano na shughuli za Bodi ya Mikopo kutoa michango
endelevu na kuikosoa Bodi ili kuiwezesha
kuona kwa sawasawa nafasi na wajibu wake katika kufanya kazi zake muhimu sana
kwa Tanzania yetu ya leo.
Mapendekezo
Kutokana na matokeo ya utafiti kama
ulivyofanyika na kutoa matokeo yake, mtafiti aliona ni vyema kupendekeza
yafuatayo ili utafiti huu usiwe ni sehemu ya kubomoa bali ni mchango mkubwa
katika kujenga na kuimarisha shughuli za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
Tanzania hususani katika kipengele cha mawasiliano ya intaneti kama
yalivyoorodheshwa hapo chini;
- Bodi ya Mikopo iimarishe na kuboresha huduma za mtandao wa intaneti kwa kuongeza taaluma ya mawasiliano ya umma kwa watendaji wake katika zama hizi za utandawazi.
- Bodi ya Mikopo ijenge kituo cha mawasiliano ya huduma kwa wateja kwa njia ya simu na intaneti itakayopatikana kwa masaa ishirini na nne kwa gharama za mtumiaji wa huduma hiyo. (A Student call centre- for receiving and transmitting a large volume of requests by telephone/online).
- Bodi ianzishe akaunti za wateja mtandaoni ambazo zitaruhusu wadau wote wa eneo la mikopo ya elimu ya juu kuweka na kutoa taarifa na data nyingine muhimu zinazohitajika bila urasimu wowote kwa Bodi na wakopaji.
- Bodi ipunguze idadi ya washiriki katika mchakato wa usajili wa waombaji kwa kuwasiliana na Mwombaji, Tanzania Commission for Universities (TCU), Vyuo husika vya waombaji na Baraza la Mitihani tu kwa kutumia mtandao wa intaneti.
Ahsanteni sana
kwa kunisikiliza
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA!
Ally Mohamed Kileo
Post Graduate Diploma in Mass Communication, 2011
(SJMC-UDSM).
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment