MAKAO Makuu ya Jeshi la Polisi nchini jana yaligeuka uwanja wa
mapambano kati ya askari na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), waliomfuata Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, aliyekwenda
kuhojiwa.
Hali ilianza kuonekana si tulivu kuanzia saa tatu asubuhi, baada ya
askari kutanda katika barabara za maeneo yanayozunguka jengo la Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi maeneo ya Posta Mpya wakiwa na mbwa, mabomu ya
machozi na bunduki.
Majira ya saa nne, barabara zote zinazopita karibu na jengo hilo
ambalo ndiko yaliko makao makuu ya Jeshi la Polisi, zilifungwa kwa kamba
maalumu kuzuia watu wanaoingia.
Amri hiyo ya kufunga barabara na maelekezo kwa wafuasi waliokuwa
wamekusanyika katika maeneo hayo yalikuwa yakitolewa na askari aliyevaa
kitambulisho chenye jina la D.D Muganyizi kwenye sare yake.
Muda mfupi baadaye, askari 12 walitoka ndani ya jengo hilo
walijipanga watatu watatu huku wakiwa na mabomu ya machozi na bunduki.
CHADEMA walivyowasili
Viongozi wa kwanza wa CHADEMA kufika maeneo hayo walikuwa Mkurugenzi
wa Operesheni na Mafunzo, Benson Kigaila, na mjumbe wa bodi ya wadhamini
wa chama hicho, Muslim Hassanal, wakitumia gari aina ya Prado yenye
namba T538 ALG.
Saa 4:49 Wanasheria wa CHADEMA, Profesa Abdallah Safari ambaye pia ni
Makamu Mwenyekiti Bara, na Mabere Marando, Mjumbe wa Kamati Kuu,
waliwasili na kushangiliwa na wafuasi wa CHADEMA.
Saa tano, msafara wa Mbowe ulifika karibu na maeneo ya Wizara ya
Mambo ya Ndani, ukazuiwa huku Polisi waliowataka Mbowe na msafara wake
washuke na kutembea kwa miguu. Viongozi wa CHADEMA walipinga, kukazuka
mzozo kwa takribani dakika tatu, kabla ya Polisi kuwaruhusu.
Mbowe alifika akiwa katika gari yenye namba T968 BKH, Toyota Land
Cruiser, na kuzuiwa kuingia getini kwa muda, ambako kulikuwa na
mabishano makali kati ya askari na wafuasi wa CHADEMA.
Kadri muda ulivyokuwa ukienda, ndivyo wafuasi wa CHADEMA walivyokuwa
wakiongezeka, hivyo kufanya polisi waanze kuwafukuza na kuzuia waandishi
wa habari.
Askari hao walisema wanafanya hivyo kwa maelekezo ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja.
Chagonja alisikika mara kadhaa akitoa amri kwa askari wafungulie mbwa ili wajeruhi angalau mtu mmoja kwa lengo la kuwatawanya.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA, walikaa chini barabarani
wakisikika wakisema ‘liwalo na liwe.’ Wengine walirusha tuhuma kwa
polisi kwa kuwaonea na kuwadhibiti huku wakiacha rasilimali za nchi
zinaporwa.
Wakati wote huo, kulikuwa na fujo getini baada ya polisi kuzuia
mawakili wa CHADEMA kuingia kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya Mbowe,
huku walinzi wa Mbowe wakikabiliana vikali getini kutaka Tundu Lissu na
mawakili wengine waingie, ingawa polisi walikuwa hawataki.
Hata hivyo baada ya purukushani zilizodumu kwa nusu saa, mawakili
waliingia, na hivyo kufanya jopo la mawakili waliomsindika Mbowe kuwa ni
Mabere Marando, Prof. Abdallah Safari, Tundu Lissu, Peter Kibatala,
John Mallya, Jonathan Mndeme, Halima Mdee na wengine ambao majina
hayakupatikana.
Msafara huo uliandamana na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa
Baraza la Wazee wa Chama hicho, Juma Hashim Issa, Mwenyekiti wa Baraza
la Vijana, Paschal Patrobas, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Christopher Ole Sosopi na Katibu
wa Bavicha, Julius Mwita, na viongozi mbalimbali wa chama hicho jijini
Dar es Salaam.
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher
Mtikila, aliwasili kwa bajaji akazuiwa na polisi; akawaambia kuwa yeye
anaunga mkono harakati zozote za kudai Tanganyika.
Mbowe atolewa kwa siri
Baada ya mahojiano yaliyodumu kwa saa nne, Mbowe alipewa dhamana kwa
masharti kuwa awaambie wafuasi wake waondoke maeneo hayo kwa amani, kazi
iliyofanywa na wanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, Mabere
Marando na Naibu Katibu Mkuu John Mnyika.
Hata hivyo, Mbowe aliondolewa kwa siri kupitia mlango wa nyuma na
kusindikizwa na magari matatu ya polisi yaliyojaa polisi waliojihami,
hadi makao makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Baada ya kufika huko, Mbowe aliwashukuru wafuasi wote waliomsindikiza akisema kama wasingefanya vile angelala jela jana.
Dodoma polisi wajihami
Mjini
Dodoma, kutwa nzima ya jana, polisi walikuwa kwenye pilika pilika za
kudhibiti wafuasi wa CHADEMA, waliodhamiria kuandamana hadi eneo la
Bunge kushinikiza Bunge la Katiba lisitishwe.
Maandamano yalipangwa kuanzia eneo la viwanja vya Bustani ya Nyerere
Square na kuhitimishwa eneo la Bunge kuanzia saa nne asubuhi hadi sita
mchana.
Ili kudhibiti maandamano hayo, tangu alfajiri polisi wa kawaida,
trafiki na wale wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), walitanda eneo la
Nyerere Square na Bunge wakiwa na magari, mabomu ya machozi, mbwa na
farasi.
Eneo la Nyerere Square ambalo ni maarufu kwa watu kupumzika wakipiga
picha, chakula, vinyaji baridi, chai na wafanyabiashara ndogo ndogo jana
halikuwa na shughuli hizo.
Katika eneo la kuzunguka Bunge, ulinzi mkali uliimarishwa ikiwa ni
pamoja na kufungwa kwa barabara kuu ya Dar es Salaam-Dodoma inayopita
eneo hilo na hivyo magari kulazimishwa kukatiza barabara ya Dodoma Inn
na ile itokayo mjini kwenda Morogoro kupitia Dodoma Sekondari.
Askari hao katika kuwatia hofu watu wenye nia ya kuandamana, walikuwa
wakizunguka na magari yaliyofungwa bendera nyekundu kila kona ya mji.
Katika harakati hizo, baadhi ya watu walikamatwa kwa kuonesha nia ya kutaka kuandamana kinyume na agizo la polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukuna, aliyezuia
maandamano hayo juzi, naye alikuwa akizunguka mitaani akiwa kwenye gari
la FFU.
Gari moja lililosheheni askari liliegeshwa katika ofisi za CHADEMA Mkoa.
Arusha kuandamana kesho
Wakati huo huo, CHADEMA mkoani Arusha kimetangaza njia yatakapopita
maandamano yao ya amani kupinga kuendelea kwa Bunge la Katiba
yatakayofanyika kesho kuanzia majira ya saa tano asubuhi maeneo ya
Philips.
Maandamano hayo yatashirikisha wananchi na wanachama wa vyama vyote
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA). Yataenda mpaka uwanja wa
Samunge na yatapopokelewa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro, aliwaeleza waandishi
wa habari jana kuwa, tayari majimbo yote saba ya Arusha yaliwasilisha
barua kwa wakuu wa polisi wa wilaya, (OCD), kuwataarifu juu ya
maandamano hayo ya amani tokea Septemba 17 mwaka huu.
Alisema kuwa maandamano hayo ya amani kwa upande wa Arusha Mjini,
yataongozwa na wabunge wote wa chama hicho yatapita Sanawari, Mianziani,
Mzunguko wa Florida, Barabara ya Sokoine ambako yatakomea kwenye
viwanja vya Samunge majira ya saa 10 jioni kutakapofanyikamkutano
mkubwa.
“Hili ni suala la watanzania wote, maandamano haya ya amani yanapinga
matumizi mabaya ya kodi za Watanzania, hivyo nawashauri polisi
waongozane na sisi kwani hakutakuwa na vurugu ya aina yoyote…
“Fedha zinazofujwa ni nyingi mno wakati Watanzania wengi
wanateseka kwa kukosa huduma muhimu, ninyi ni mashahidi, watu wanakufa
kwa kukosa dawa kwenye hospitali zetu, watoto wetu wanakaa chini shule
tunaambiwa serikali haina fedha wakati zinafujwa na kikundi kidogo cha
watu huko Dodoma,” alisema Lazaro.
Alisema kuwa hata kama polisi hawatatoa kibali, wao wataandamana
kwani wamefuata taratibu zote za kufanya maandamano kwa mujibu wa
sheria zinazowataka kuwataarifu ma OCD zaidi ya saa 48 kama sheria
inavyotaka.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mwanzoni mwa wiki hii, alisema kuwa yeye
anafuata msimamo uliotolewa na makao makuu ya jeshi hilo ya kuzuia
kufanyika kwa maandamano hayo, hivyo hata mkoani Arusha maandamano hayo
hayaruhusiwi.
CWT yatangaza mgomo usiokoma Manyara
Mkoani Manyara Chama Cha Waalimu, (CWT) kimesema kuwa kitaanza mgomo usio na kikomo kushikiniza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Aidha, mgomo huo utaambatana na maandamano makubwa kuelekea mkoani
Dodoma kunakofanyika vikao hivyo walivyodai kuwa ni matumizi mabaya ya
fedha za kodi za wananchi, ambazo zilipaswa kupelekwa kwenye matumizi ya
msingi ikiwemo kulipa malimbikizo ya muda mrefu ya madeni ya walimu.
Msimamo huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa CWT mkoani humo, Qambos
Sulle, akiwa ameambatana na Katibu wake, Nuru Senkalwa wakati
akizungumza na waandishi wa habari juu ya maazimio ya mkutano wao mkuu
uliyofanyika Kata ya Gallapo wilayani Babati.
Alisema kuwa mgomo na maandamano hayo, yataanza rasmi Oktoba, endapo
bunge hilo litaendelea na vikao mpaka kufikia mwisho wa mwezi huu.
Mwalimu Sulle, alisema kuwa kwa Taifa kutumia fedha nyingi bila
kuwa na matokeo chanya ni hasara, hivyo akataka viongozi kutafakari juu
ya fedha nyingi zinazotumika kuendesha bunge hilo huku sekta ya
elimu ikikabiliwa na matatizo lukuki, ikiwemo shule nyingi kuwa na
ukosefu wa vitabu, madawati, mishahara duni kwa watendaji wa sekta hiyo
hasa walimu na hospitali kutokuwa na vifaa na dawa.
“Kwa kuwa hakuna uwezekano wa katiba kupatikana kwa wakati kabla
ya uchaguzi mkuu mwakani (2015), ni vema mchakato huu ukasitishwa
mara moja hadi uchaguzi mkuu upite kama Rais Kikwete
alivyosema akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Ikulu Dodoma,”
alisema mwalimu Sulle.
Alisema kuwa wanaunga mkono maandamano yaliyotangazwa na Mwenyekiti
wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa kile alichoeleza kuwa yana
msingi kwani wana haki ya kudai na kutetea maslahi ya wananchi.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment