Profesa Ibrahim Lipumba
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kuwa nchi inaelekea pabaya kiasi cha umma kuanza kufikiria namna ya kuchukua maamuzi magumu, kutokana na kuwapo kwa dalili za wazi za dola kufeli. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema kitendo cha baadhi ya mahakama na Jeshi la Polisi kutokuwa na weledi, ni dalili mbaya.
Profesa Lipumba alisema kitendo cha mahakimu wa mahakama ya Mkoa wa Mtwara kufanya njama za makusudi za kuwanyima dhamana viongozi sita wa chama hicho kwa kuwawekea masharti magumu, haziwezi kuvumiliwa.

“Zipo dalili za taifa hili kuwa kama mataifa mengine ya Afrika yaliyo na migogoro kati ya umma na dola na kusababisha Serikali kushindwa kuongoza nchi kutokana na vitendo vya unyanyasaji na kutotimiza wajibu wao".

“Mahakimu hao waliwataka kila mshitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mkazi wa Mtwara atakayewasilisha hati ya mali isiyohamishika iliyothaminiwa na yenye thamani ya Sh milioni 20 au zaidi,” alisema.

Profesa Lipumba alisema katika hali ya kawaida, Mkoa wa Mtwara ni vigumu kupata hati za namna hiyo na kuongeza kwamba mahakama hizo hazitaki nyumba ya ofa bali wanahitaji hati halisi zenye vielelezo kuanzia mtaa hadi stakabadhi za malipo ya kodi ya nyumba.

Alisema licha ya kukamilisha hayo na kuwasilisha kumekuwapo na mizengwe ya aina tofauti huku baadhi ya mahakimu wanaosikiliza kesi kujitoa bila taarifa.

Profesa Lipumba alisema kesi hiyo imekaliwa na mkono wa dola, ambao ni kamati ya usalama na ulinzi ya mkoa huo na kutoa maagizo kwa polisi.

“CUF tunasikitishwa na vitendo vinavyofanywa na mahakama na polisi, awali tulisema viongozi wetu sita wamekamatwa Mtwara lakini tulipohoji kisa cha ajabu polisi walikataa,” alisema.

Profesa Lipumba aliongeza: “Tunachosikitishwa ni kwamba, viongozi hao wamebambikiwa kesi ya jinai ya kupanga njama, kufanya mkusanyiko usio halali na uchochezi, kitu ambacho si kweli.

“Ukweli ni kwamba, viongozi hao walikuwa wanarejea Dar es Salaam wakitoka Mtwara tulikowaagiza kusikiliza kesi ya wanachama wetu iliyokuwa ikisikilizwa lakini walitekwa na wanajeshi na kupelekwa kambi ya Naliendele.

“Sasa taarifa tulizonazo mpaka sasa Mkurugenzi wetu wa Mipango, Uchaguzi na Bunge, Shaweji Mketo ana hali mbaya kiafya baada ya kuumizwa tumboni kutokana na upasuaji aliokuwa amefanyiwa,” alisema.

Profesa Lipumba alisema kutokana na vyombo hivyo kutotenda haki, dalili zinaonyesha wananchi walio wengi wameanza kuwa na wasiwasi.
Via Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top