Rais Kikwete na Uhuru Kenyatta wakiteta jambo
SIKU nne tangu Rais Jakaya Kikwete alihutubie Bunge na kuweka
bayana msimamo wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali
ya Kenya imempongeza huku ikisisitiza kuwa nayo itaendelea kuwa
mwanachama mwaminifu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa na hatua ya
marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni (Uganda) na Paul
Kagame wa Rwanda kuanza mazungumzo ya kuitenga Tanzania, lakini akasema
kamwe haitaondoka kwenye jumuiya hiyo.
Alisema nchi hizo zimeanza mazungumzo kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta, jambo linalovunja misingi ya jumuiya hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, jana alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo
ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Membe
alisema Kenya imesema kuwa mazungumzo kati yake na nchi za Uganda na
Rwanda kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta yalifanyika bila nchi
yake kujua kwamba inavunja misingi ya jumuiya.
“Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya yuko nchini, ametumwa na rais wake,
Uhuru Kenyatta kuja kutoa pongezi kwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
aliyoitoa bungeni,” alisema Membe.
Kwa mujibu wa Membe, Kenya ilidai kuwa ilifanya hivyo bila kufahamu
kwamba nchi hizo zinaibagua Tanzania ambayo ni mwanzilishi wa jumuiya
hiyo.
“Tunapongeza hotuba ya Rais Kikwete bungeni na kuahidi kwamba Kenya
itaendelea kuwa mwanachama imara wa jumuiya hiyo, atakayelinda misingi
imara na taratibu zilizowekwa,” alisema Membe akimkariri Waziri wa
Kenya.
Aliongeza kuwa ujumbe huo ulikiri kutokea kwa tatizo hilo, hasa
ikizingatiwa kwamba viongozi wa nchi hiyo wamechukua madaraka Aprili 8,
mwaka huu.
“Kwa ujumla Kenya inasema ilipotoka kufanya mazungumzo kuhusu mambo
ambayo yapo kwenye mkataba bila kuishirikisha Tanzania,” alisema.
Nchi za Uganda na Rwanda bado hazijasema chochote kuhusiana na hotuba hiyo ya Rais Kikwete.
Lipumba aonya
Wakati Kenya ikijirudi, Chama cha Wananchi (CUF) kimeunga mkono
msimamo wa Rais Kikwete, lakini kikimtaka vile vile akubali udhaifu
uliopo nchini katika usimamizi wa miundombinu mbalimbali ili kuweza
kufanya ushindani na kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CUF, Prof.
Ibrahimu Lipumba, alisema licha ya kuwa na msimamo huo, lakini bado
kuna haja ya kuimarisha uchumi wa ndani ili kuweza kuweka ushindani.
Alisema kulikuwa na taarifa kuhusu Rwanda na Uganda kutotumia bandari
ya Dar es Salaam, na kwamba lisitazamwe kisiasa kutokana na bandari
hiyo kuwa na udhaifu mkubwa unaolalamikiwa na wafanyabiashara wa ndani
na nje ya nchi.
“Sio Rwanda na Uganda tu wanalalamika kuhusu bandari hiyo, bali
Kongo, Zambia na Malawi pia wanailalamikia kuwa na sifa ya
ucheleweshaji wa kupakua shehena za mizigo toka kwenye meli, wizi wa
mizigo yakiwemo makontena na vifaa vya magari kama vile taa, redio.
“Uchakachuaji wa mafuta, urasimu na ucheleweshaji wa mizigo kutoka
bandarini, ukubwa wa tozo za bandari na barabara na ugumu wa magari ya
mizigo kufika na kutoka bandarini, taratibu za utoaji mizigo
zisizotabirika na rushwa bandarini,” alisema.
Kwa mujibu wa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, asilimia 90 ya
biashara yote ya Tanzania na nchi za nje inapita katika bandari ya Dar
es Salaam kutokana na nchi sita jirani za Malawi, Zambia, Kongo,
Burundi, Rwanda na Uganda kutokuwa na bandari.
Alisema rais na watendaji wake wanatakiwa kufahamu kuwa bandari ya
Dar es Salaam inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka bandari ya Mombasa
inayofanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi na bandari ya Beira, Msumbiji
ina ushindani mkubwa kwa mizigo inayokwenda Malawi, Zambia na hata
Kongo.
Prof. Lipumba aliongeza kuwa serikali inaelewa wazi kuwa utendaji wa
bandari ya Dar es Salaam ni mbaya, usioridhisha, lakini kutokana na
ombwe la uongozi imekuwa ikisuasua kufanya mabadiliko ya kuongeza
ufanisi.
Alisema uzembe wa utendaji wa bandari unasababisha msongamano
ambapo kushusha mizigo kunachukua takribani siku 10 ukilinganisha na ile
ya Mombasa inayochukua siku moja .
Pia alisema gharama za tozo Mombasa ni asilimia 22 kwa kila kontena
za tozo kwa bandari ya Dar es Salaam ziko juu kwa asilimia 74
ukilinganisha na bandari ya Mombasa.
Pia aligusia utendaji wa Shirika la Reli kuwa umeporomoka ambapo kwa
mwaka 2012, shirika lilisafirisha tani 154,000 ukilinganisha na tani 1,
446,000.
“Ikiwa reli ya kati itafanya kazi kwa ufanisi na tija ya hali ya juu,
nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda wanaweza kutumia reli ya kati
kusafirisha mizigo yao kwenda na kutoka Dar es Salaam.
“Reli ya Tazara haijatumiwa kwa kadiri ya uwezo wake. Mwaka 2012
ilisafirisha mizigo tani 259,000 ukilinganisha na tani 677,000 kwa
mwaka 2002. Kwa kawaida usafiri wa reli ni wa gharama za chini
ukilinganisha na usafiri wa barabara, tuna wajibu wa kuimarisha
utendaji wa Shirika la Tazara ili kuongeza ushindani wa kibiashara na
kukuza uchumi wetu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment