Zitto Kabwe
WAKATI ripoti ya kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza
tuhuma za vigogo walioficha fedha kwenye mabenki ya nje ya nchi ikiwa
bado haijatolewa bungeni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(CHADEMA), amewataja vigogo watatu kuwa miongoni mwa wahusika.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), ndiye
muasisi wa hoja hiyo bungeni. Hivi karibuni alitishia kuwataja wahusika
endapo serikali haitawasilisha ripoti hiyo kwenye mkutano wa Bunge
uliomalizika Jumamosi.
Mbunge huyo aliwataja vigogo hao juzi wilayani Kaliua mkoani Tabora
wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Uwanja wa Kolimba.
Bila kutaja majina yao, Zitto aliwataja kwa nyadhifa zao walizowahi
kushika akisema ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Waziri
wa Ulinzi wa zamani na aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi.
Alisema baada ya kutoa hoja bungeni ya kuitaka serikali ifanye
uchunguzi juu ya Watanzania walioficha fedha nje ya nchi, alichaguliwa
kuongoza timu ya kufuatilia sakata hilo, kupitia taasisi ya Eurodad,
ambapo alifanya ziara katika sehemu mbalimbali ikiwemo nchini Uswisi na
Uingereza.
Zitto alifafanua kuwa akiwa huko alikutana na wadau mbalimbali wa
masuala ya kibenki pamoja na kuhudhuria mkutano wa Waziri Mkuu wa
Uingereza uliokuwa ukizungumzia utoroshwaji wa fedha.
“Hawa watu wanajulikana na tutawataja kwa majina mchakato
ukikamilika, lakini kwa sasa niwaambie miongoni mwa watu hao ni pamoja
na waliowahi kuwa mawaziri na mmoja wa wakuu wa majeshi mstaafu,”
alisema Zitto.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali inaendelea kushikwa na
kigugumizi cha kuwaanika watu hao hadharani licha ya Serikali ya Uswisi
kuitaka isaini mkataba wa kubadilishana taarifa.
Zitto alisema kwa sasa ameshawaagiza wasaidizi wake katika masuala ya
kibunge kuandika utaratibu utakaowasilishwa bungeni kwa ajili ya
kuwadhibiti watu wanaoficha fedha nje bila kuwa na maelezo ya kutosha.
Aliongeza kuwa suala la kuwaanika hadharani watu wanaoficha fedha nje
ya nchi linahitaji uungwaji mkono wa hali ya juu kwa kuwa ni kazi ya
hatari inayowagusa watu wenye maslahi na uwezo mkubwa nchini.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, mbali na Tanzania, nchi nyingi za Afrika
zinaweka fedha nyingi Uingereza pamoja na visiwa vyake 15 ambapo katika
kisiwa cha Jersey pekee kuna paundi bilioni 40 za Uingereza.
Zitto alisema baadhi ya nchi huwafilisi watu ambao wanabainika kuwa
wameficha fedha nje na kuzitumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema kuwa wakati anafanya shughuli hiyo aliyosema ni ajenda ya
kitaifa, alitegemea kuungwa mkono na watu wake wa karibu, ikiwa ni
pamoja na walio ndani ya chama chake.
“Hivi ni vita visivyohitaji utengano, tunapoamua kulumbana sisi kwa
sisi wenzetu wanapata mwanya wa kufanya mambo yao, nilitegemea katika
hali hii CHADEMA tushikamane kuliangamiza hili dude CCM,” alisema
Zitto.
Kuhusu migogoro
Zitto alisema CHADEMA hawama migogoro na kinachofanyika ni mikakati
ya watu wachachahe wasio na shughuli kuamua kuwagonganisha viongozi.
“Kuna watu wachache sana ambao hawana kazi, shughuli yao ni
kugonganisha viongozi ili wagombane na ikitokea hivyo wao ndiyo furaha
kwao, sio ufahari hata kidogo kwa CHADEMA kuonekana ina migogoro,”
alisema.
Zitto alisema mwaka 1995 kabla ya CHADEMA kuamua kuiunga mkono
NCCR-Mageuzi, Edwin Mtei na Bob Makani waligombea nafasi ya kutaka
kuwania urais kupitia chama hicho na hakukuwa na misigano yoyote kwa
kuwa walijua malengo yao ni kuwatumikia Watanzania.
Aliongeza kuwa hali ya watu kuwania nafasi moja ndani ya CHADEMA
ilijirudia mwaka 1998, kwa nafasi ya uenyekiti kuwaniwa na watu wawili
tofauti na hakukuwa na mgogoro.
“Uchaguzi ndani ya CHADEMA ulifanyika mwaka 2009, tukapata viongozi
na tukaingia kazini, mliona tulichofanya, tulivuna wabunge wengi,
madiwani na wenyeviti wa mitaa. Lakini sasa hali inaanza kuwa ya ajabu
ajabu utafikiri kuna mtu aliyetangaza kugombea,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, hatua yake ya kugombea uenyekiti mwaka 2009
ilitokana na kile alichokuwa amekiona kuwa kutekeleza demokrasia ndani
ya chama chake kutokana na waliomtangulia kujitokeza kuwania nafasi
walizoona zinawafaa.
“Mimi ni binadamu, nina damu na nyama, katika umri huu mdogo
nimepigwa mishale mingi sana ya kisiasa, ninaumia na damu inanitoka,
sasa nimechoka kupigwa mishale, ni lazima viongozi tuambiane ukweli na
tukemee hali hii,” alisema Zitto.
Alisema kuwa mwanzoni hapakuwa na chama chenye nguvu kama
NCCR-Mageuzi, lakini walipoanza kupigana kile alichokiita mishale,
chama hicho kilisambaratika.
“Wakamchafua sana Mabere Marando kuwa ndiye msaliti, sasa Marando
yuko wapi? Si ni kamanda wetu? Si ndiye huyu mwanasheria wetu? Lazima
tuambiane ukweli na tuweze kuvikwepa vihunzi vya CCM, lazima sasa
wanachama wanaoleta chokochoko washughulikiwe,” alisema.
Alisema kuwa viongozi lazima waonye haya mambo, kwamba bila kuonya wataonekana wanashiriki.
“Waha tuna msemo; ukiona kifaranga yupo juu ya chungu, jua mama yake yupo chini,” alisema Zitto.
Kapuya ajisalimisha
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma
Kapuya (CCM), juzi alijisalimisha katika ofisi ya CHADEMA akimuomba
Zitto azungumzie matatizo ya barabara katika jimbo lake ili aweze
kusaidiwa.
Kapuya alitoa ombi hilo katika ofisi za CHADEMA wilaya baada ya Zitto
kuwasili eneo hilo saa 9.30 mchana kwa ajili ya kufanya mkutano wa
hadhara, ikiwa ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati alipohutubia
mkutano wa awali kwa njia ya simu wiki tatu zilizopita.
Akiwa ofisini hapo, Prof. Kapuya alihojiwa na Zitto akitaka kujua
sababu ya kuikodishia Halmashauri ya Kaliua nyumba yake huku akiwa ni
mmoja wa madiwani wa wilaya hiyo wanaopaswa kuhakikisha halmashauri
inakuwa na majengo yake.
“Karibu mzee katika ofisi zetu, lakini unaweza kuniambia kama uamuzi
wako wa kuikodishia halmashauri nyumba yako hauingiliani na vikwazo vya
kuiwezesha kupata majengo yake?” alihoji Zitto.
Katika kujitetea, Prof. Kapuya alisema sababu ya kufanya biashara
hiyo na halmashauri ni kutokana na wilaya kutokuwa na majengo yake
binafsi.
“Ni kweli mimi ninakodisha, lakini kiasi ninachochukua ni kidogo
kuliko kile anachochukua Waziri Magufuli katika Wilaya ya Chato, kwani
naye anaikodishia halmashauri ya wilaya yake jengo linalotumika kama
ofisi,” alisema Kapuya.
Katika hali ya kuonyesha kuwa anaomba Zitto asizungumzie upungufu
uliopo katika jimbo lake, Prof. Kapuya alimuomba azungumzie matatizo ya
barabara.
Zitto alisema kimaadili kiongozi anapofanya biashara sehemu anayoweza
kuwa na uamuzi inasababisha hali ya kulinda maslahi ya kiongozi huyo
ikiwa ni pamoja na kukwamisha mradi wa eneo husika usikamilike au
kujiongezea gharama katika biashara husika.
Alimueleza Prof. Kapuya kuwa kinachosabaisha Mkoa wa Tabora
usiendelee, ni pamoja na matatizo ya ubinafsi kati ya wabunge wa mkoa
huo, huku akiwaambia waache tofauti zao na Mbunge wa Urambo Mashariki,
Samuel Sitta katika kuwatumikia wananchi.
0 comments:
Post a Comment