Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, huku kukiwa na ushindani wa maeneo mawili ambayo baadhi ya wabunge walionyesha hofu.
 
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa hati ya dharura kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika Oktoba 15, mwaka huu, baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, baada ya muswada wa awali kususwa na vyama vya upinzani bungeni.
Katika mjadala ulioanza juzi na kuhitimishwa jana, wabunge wengi kutoka pande zote; CCM na upinzani waliyaunga mkono mapendekezo ya Serikali, lakini kulikuwa na hofu kuhusu idadi ya wajumbe watakaoteuliwa na Rais kuingia kwenye Bunge Maalumu na suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Marekebisho hayo yameiweka kando Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo haitakuwapo baada ya kukabidhi rasimu ya pili ya Katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete, Desemba 15, mwaka huu.
Uhai wa tume hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyozua ubishi baina ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa wakitaka iendelee kuwapo na wale wa chama tawala na Serikali, ambao walitaka iondoke kwa maelezo kwamba haitakuwa na kazi baada ya kukabidhi rasimu kwa rais kama inavyoeleza sheria ya kuanzishwa kwake.
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani alisema kuvunjwa kwa tume kutaathiri utekelezaji wa vifungu vingine vya sheria hivyo, ikiwa ni pamoja na kile kinachotaka Mwenyekiti wa Tume, makamu wake au makamishna kuitwa kwenye Bunge la Katiba kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mambo yatakayozua utata.
Kwa msingi huo kambi hiyo ilipendekeza tume hiyo isivunjwe na wajumbe wake waingie katika Bunge Maalumu la Katiba kama wataalamu wa kulisaidia Bunge hilo, lakini wasiwe na haki ya kushiriki uamuzi kwa maana ya kupiga kura.
Hata hivyo, mapendekezo hayo na mengine ya aina hiyo yaliyoletwa na nyaraka za marekebisho (schedule of amendments) wakati Bunge lilipoketi kama kamati kupitia muswada huo vifungu kwa vifungu yalitupwa, hivyo kuweka ukomo wa Tume ya Warioba mara baada ya kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais Kikwete, Desemba 15, 2013.
Wakati wakivutana, Lissu aliwarushia lawama wabunge wa CCM kuwa wanawakataa wajumbe wa tume kwa sababu ilipendekeza serikali tatu ambazo wao hawazitaki.
Lissu alisema kwa kauli na vitendo hivyo, vilionyesha wazi kuwa CCM kinamsaliti Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba ambaye amefanya kazi kubwa na ya weledi kiasi cha kupongezwa na Rais Kikwete.
Katika majibu yake kwa wabunge, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alipinga na kueleza kuwa hata kama wabunge wangetaka Tume ya Warioba iwe ni sehemu ya Bunge la Katiba, hakuna umuhimu huo.
Chikawe alifafanua kuwa sheria inaeleza wazi kuwa kipindi cha uhai wa tume hiyo kinakoma baada ya kukabidhi rasimu tu.

Bunge la Katiba
Kulikuwa na hoja iliyotaka wabunge watakaoteuliwa na raia kutoka katika makundi idadi yao iongezwe hadi 292, kutoka wajumbe 201 waliokuwa wamependekezwa.
Itakumbukwa kuwa Serikali ilishaongeza idadi hiyo ambayo awali ilikuwa ni wajumbe 166 hadi kufikia wajumbe 201 ambao hata hivyo bado baadhi ya wabunge walipinga kuwa ni wachache.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alitoa hoja hiyo na kueleza sababu za kutaka idadi hiyo ambapo alisema kuwa makubaliano ya awali yalikuwa ni lazima kuwepo na theluthi mbili ya wabunge hao.
“Awali pendekezo la Serikali lilikuwa ni kupata mbili ya tatu ya wabunge wote, mheshimiwa mwenyekiti, ikiwa sasa wabunge wa Bunge la Jamhuri pamoja na Wawakilishi tunafika jumla yetu 438, Serikali haioni kuwa mbili ya tatu ni watu 292 ni kwa nini wasikubali wazo letu,” alihoji Mnyika.
Hoja hiyo ilileta mvutano huku wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi wakilalamikia kuwa kuongeza idadi ni sawa na kuongeza gharama za bunge.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba alisema kuwa kinachompa wasiwasi Mnyika ni kutokana na ukweli kuwa wanaotakiwa kushiriki bunge hilo wengi wanatoka Chama Cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alipinga pendekezo la Mnyika na kudai kuwa halikuwa na mashiko yenye masilahi kwa Taifa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Mnyika hakina mashiko kwani suala la kuongeza idadi ya wajumbe halipaswi kuingizwa, sisi tuliomo humu ndani tumechaguliwa na wananchi wote sawa na hao anaopendekeza Mnyika, kwani shida ni nini tena?” alihoji Bulaya.
Wasomi na wanasheria wanena
Akizungumzia hatua hiyo iliyopitishwa na Bunge, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Tolly Mbwete alisema uamuzi huo umezingatia busara na utasaidia kuepusha wajumbe wa Bunge la Katiba kulazimishwa kukubaliana na mawazo yaliyopo kwenye rasimu.
Alisema kuwa ni vyema wajumbe hao wakaingia ndani ya Bunge hilo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi au maelezo pale itakapobidi, lakini wasishiriki kama wajumbe wa Bunge hilo.

“Naona uamuzi huu umefanyika kwa busara, kwani wajumbe wa tume tayari wameshatoa mawazo yao endapo wataingia pia kwenye Bunge la Katiba kuna hatari ya kulazimisha mawazo hayo kupitishwa na hatimaye kuandika kwenye Katiba ila endapo watahitajika kutoa ufafanuzi waruhusiwe kuingia.”
Naye Profesa Abdalla Safari ambaye ni mwanasheria alisema hakuna sababu ya wajumbe hao kuingia kwenye Bunge la Katiba kwa kuwa mawazo yao wameshayatoa kwenye rasimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema uamuzi huo haukupaswa kupitishwa kwa kuwa wajumbe wa Tume ya Warioba ndio walioandaa rasimu, hivyo walipaswa kushiriki katika Bunge hilo kwa ajili ya kuiwasilisha na kuitolea ufafanuzi.
Aliongeza kuwa Serikali haina mamlaka ya kuuwasilisha muswada huo kwa kuwa tume hiyo ilichaguliwa kuwawakilisha wananchi, hivyo kutoshiriki katika Bunge hilo kunawanyima haki ya msingi Watanzania ambao ndiyo wanahusika na katiba hiyo.
“Tume ya Warioba inasimama badala ya wananchi kuwanyima haki ya kushiriki katika Bunge hilo kunamaanisha kuwatoa wawakilishi wa wananchi ambao wana uwezo wa kusimamia na kutolea ufafanuzi wa rasimu ambayo itatengenezewa Katiba ya Tanzania,” alisema Dk Bisimba.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top