Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametengua tangazo la Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki la kuligawa eneo la Pori
Tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kwa kutenga
kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi na kilomita za mraba 2,500
kuwa chini ya Serikali za vijiji.
Machi 19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa
tangazo la Serikali la kuligawa pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za
mraba 4,000 ili Serikali iweze kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500
ambalo alieleza kuwa ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza
ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro
mkubwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo
la Waso jana baada ya kutembelea eneo la mgogoro na kufanya kikao na
ujumbe wa mawaziri alioambatana nao na watendaji wa wizara mbalimbali,
Waziri Mkuu alisema amefikia uamuzi wa kuondoa tangazo hilo la Serikali
na sasa wananchi wa eneo hilo wataendelea na utaratibu uliozoeleka.
Mawaziri waliokuwa katika ziara hiyo ni Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa
Maji, Dk Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Benedict Ole Nangoro na Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa.
“Mara baada ya lile tangazo kuliibuka mgogoro wa
wananchi kupinga na baadhi ya viongozi walinifuata hadi Dodoma na
kuniletea malalamiko yao. Pia CCM iliunda tume na kunipa taarifa lakini
nikasema siwezi kutoa uamuzi hadi nifike mwenyewe katika eneo hili na
sasa nakubaliana na hoja za wananchi kuwa kuligawa eneo kutakuwa na
athari kwenu, naomba sasa mwendelee na utaratibu wenu kama vile
halikuwepo tangazo hilo,” alisema Pinda.
Alisema miongoni mwa hoja za wananchi
zilizosababisha afikie uamuzi huo, ni kuwa eneo hilo la kilomita za
mraba 1,500 ndilo ambalo lina vyanzo vya maji vinavyotegemewa na vijiji
vyote sita ambavyo vingeathiriwa na tangazo hilo. Vijiji hivyo ni
Ololosokwani, Soitsambu, Olorieni Magaiduru, Arash, Piyaya na Oloipili.
Waziri mkuu pia alisema eneo hilo lililotengwa kwa
uhifadhi ndilo tegemeo la wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa
nyakati za kiangazi, pia kuna makazi ya watu, shule na huduma nyingine
muhimu.
Alisema kutokana na uamuzi huo, Serikali
inajipanga kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo
ili kutambulika maeneo ya ufugaji, makazi, kilimo na uhifadhi ili
masilahi ya kila upande yaendelee kulindwa.
“Utaratibu wenu mliojiwekea kabla ya tangazo la
Serikali uendelee kwani tunataka shughuli za uwindaji wa kitalii
ziendelee, upigaji picha uendelee, pia ufugaji uendelee na hapa ni vyema
kukawa na vikao vya wadau wote walau kila baada ya miezi mitatu,”
alisema Pinda.
Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha na Halmashauri ya Ngorongoro kuratibu vikao hivyo kwani lengo ni
kutatua migogoro na kurejesha uhusiano.
Wakazi Loliondo vicheko
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mara baada ya Waziri Mkuu kutangaza uamuzi huo, shangwe
zilitawala na Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o ole Telele na madiwani
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Elias Ngolisa walieleza
kuridhishwa na uamuzi huo wakisema umezingatia kilio cha mamia ya
wananchi wa Tarafa za Loliondo na Sale.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ortello Business Co
operation (OBC), ambayo ingebaki katika eneo lililokuwa limetengwa kwa
uhifadhi, Isack Mollel alisema hapingi uamuzi huo lakini anataka
mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani Ngorongoro, kukubali
mwafaka huo pia kushiriki katika vikao vya kupanga matumizi bora ya
ardhi vijijini muda ukifika.
Hata hivyo, kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huo,
Mollel alisema Serikali isipotenga sasa maeneo ya uhifadhi na ufugaji,
shughuli za utalii zitakufa Loliondo sambamba na kuathirika eneo zima la
ikolojia la Serengeti kwani mifugo imeongezeka na imeanza kuingia hadi
ndani ya Hifadhi ya Serengeti.
Profesa Tibaijuka atoa suluhu
Awali, Profesa Tibaijuka alisema suluhu ya
migogoro ya ardhi Loliondo ni kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi
baada ya vijiji kupimwa kazi ambayo alikwishaianza.
Alisema umefika wakati pia kwa wafugaji wa Loliondo kupunguza mifugo na kuanza kufuga kisasa kwani ardhi haiongezeki.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment