Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Agosti, 2014 leo jijini Dar es salaam.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti,
2014 umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 6.5
iliyokuwepo mwezi Julai kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya baadhi
ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Bw.
Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya ongezeko hilo leo jijini Dar es
salaam, amesema kuwa bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo Bia, Sare za
shule, mkaa, samani za nyumbani na bidhaa za vitambaa kwa matumizi ya
nyumbani zimechangia kuwepo kwa ongezeko dogo la mfumuko wa bei nchini.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa ongezeko la
gharama kwenye huduma ya meno, huduma za vyakula kwenye migahawa na zile
za kulala hotelini katika maeneo mbalimbali nchini pia zime kumechangia
mfumuko wa bei.
Aidha, Bw. Kwesigabo amebainisha kuwa
kuongezeka kwa Fahirisi za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumiwa na sampuli
wakilishi ya kaya binafsi nchini hadi 149.31 kwa mwezi Agosti 2014
kutoka 149.16 za mwezi Julai kumechangiwa na kupanda kwa gharama ya
bidhaa zisizo za vyakula.
Kuhusu mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo
cha mwezi kwa mwezi Agosti amesema kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.1
huku uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma
za jamii kwa mwezi Agosti, 2014 ukipungua na kufikia shilingi 66 na
senti 97.
“ Kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa na
huduma katika maeneo mbalimbali kuna athari kwa fedha yetu, hii
inamaanisha kwamba, uwezo wa fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa
za mlaji unapungua, mfumuko wa bei unapopanda thamani ya shilingi nayo
inashuka”
Kwa upande wa ulinganifu wa mfumuko wa bei
wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Bw. Kwesigabo
ameeleza kuwa una mwelekeo unaofanana na kuongeza kuwa mfumuko wa bei
nchini Kenya kwa mwezi Agosti umefikia asilimia 8.36 ikilinganishwa na
7.67 za mwezi Julai huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.8
mwezi Agosti ikilinganishwa na asilimia 4.3 za mwezi Julai.
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment