Waziri Emmanuel Nchimbi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka
Watanzania kuchukua hadhari dhidi ya raia wa kigeni wakati huu ambao
amani ya dunia ipo shakani.
Tamko hilo limekuja wakati kundi la kigaidi la
Al-Shabaab limevamia jengo kubwa la biashara la Westgate huko Nairobi,
Kenya na kuua zaidi ya watu 60 huku mamia wakijeruhiwa na wengine kadhaa
kuendelea kushikiliwa mateka tangu Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, Dk Nchimbi hakugusia tukio hilo kwenye
maelezo yake lakini aliwataka Watanzania waache tabia ya kuwapa hifadhi
raia wa kigeni akisema ni hatari kwa usalama wa taifa... “Watanzania
lazima tuwe makini hasa nyakati hizi ambazo usalama wa dunia upo
shakani.”
Alisema Serikali kwa upande wake, imekuwa
ikijitahidi kuweka nchi katika hali ya usalama ikiwa ni pamoja na
kuendesha operesheni za kuwasaka wahamiaji haramu.
“Hakuna uhalali wa mtu kukaa katika nchi nyingine
bila kufuata taratibu za sheria,” alisema na kuongeza: “Ni lazima vyombo
vya usalama kujua nani kaingia na nani anaondoka.”
Alisema operesheni inayoendelea ya kuwabaini na
kuwachukulia hatua wahamiaji haramu inayojulikana kwa jina la Kimbunga,
waziri huyo alisema imebainika kuwa baadhi ya Watanzania wanawahifadhi
raia wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Alitoa mfano wa raia wa Uingereza ambaye alikuwa
akitafutwa na nchi yake kutokana na vitendo vya kigaidi lakini
akakamatwa akiwa amehifadhiwa na Mtanzania ambaye alikwishamfanyia
mipango ya kupata vitambulisho kama kile cha mpiga kura.
Alisema mkakati wa kuwaondoa raia wa kigeni
ulianza Julai 26, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alipotoa kipindi cha
wiki mbili watu wanaoishi nchini kinyume cha taratibu kuondoka kwa hiari
yao.
“Katika agizo hilo la Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, raia wa kigeni 21,758 waliondoka na kurejea makwao kwa hiari,” alisema.
Dk Nchimbi alisema operesheni ya kuwaondoa wale
ambao hawakutii amri ya Rais Kikwete ilianza Septemba 6, mwaka huu na
hadi ilipomalizika wiki hii, watu 12,604 walikuwa wametiwa mbaroni.
“Kati ya hao Wanyarwanda ni 3,448, Warundi 6,125,
Waganda 2,496, Wakongo 589, Wasomali 44, Myemeni mmoja na Mhindi mmoja,”
alisema Dk Nchimbi.
Kwenye operesheni hiyo alisema pia waliwakamata
watuhumiwa 212 wa unyang’anyi pamoja na silaha mbalimbali zipatazo 61,
baadhi zikiwa za kivita.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Alisema awamu ya pili ya operesheni ya kuwakamata wahamiaji
haramu ipo mbioni ingawa alisema safari hii, idadi ya watakaounda timu
ya uendeshaji wake itapungua.
Waziri huyo alisema kuwa wale wote wanaoishi
nchini wanaweza kuamua kuondoka, kufanya mkakati wa kuomba uraia au kuwa
na hati ya kusafiria pamoja na kibali cha kuwaruhusu kuishi nchini.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment