MIKUTANO inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kote nchini kuhusiana na rasimu ya mabadiliko ya katiba, huku
kikihimiza wananchi kuunga mkono pendekezo la kuwepo kwa serikali tatu,
imezua na kuzidisha uhasama mkubwa kati yake na Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vya kuaminika, zimebaini kuwa mwanzoni
mwa wiki hii, kulifanyika jitihada kubwa za kujaribu kuzima mikutano
hiyo kwa kutumia vyombo vya dola, lakini ikashindikana.
Imedaiwa kuwa mmoja wa viongozi wa juu wa CCM alitaka mikutano hiyo
izuiwe na Jeshi la Polisi kwa sababu zozote zile za kiusalama, lakini
mpango huo ulikataliwa na baadhi ya viongozi wanaodaiwa kuchoshwa na
siasa za kikandamizaji.
Hatua hiyo inadaiwa kuchukuliwa baada ya CCM kugundua kuwa mpango wake
wa kushinikiza wananchi kwa kutumia mabaraza ya katiba kuunga mkono
suala la serikali mbili kuelekea kushindwa vibaya.
Aidha, kuna madai kwamba kiongozi huyo alitaka CHADEMA isiruhusiwe
kama itaendelea na mikutano yake, kuzungumzia suala la serikali tatu,
kwa madai kwamba ni kwenda kinyume na sheria iliyokubaliwa ya mchakato
wa maoni ya katiba mpya.
Wakati CCM ikiwa imetoa msimamo wake na kuwaamuru viongozi wake wa
ngazi zote kushikilia msimamo huo na kuusambaza kwa wanachama wake,
uamuzi wa CHADEMA wa kuendesha mikutano ya hadhara na kuelezea msimamo
wake wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba,
umeathiri kwa kiwango kikubwa mpango mzima wa chama hicho tawala
kutimiza lengo la kampeni yake.
Aidha, baadhi ya viongozi wa CCM wanamtuhumu Jaji Warioba kwa kile
walichokiita “kuwabeba” CHADEMA na kuchukua hoja yao ya kutaka muungano
wa serikali tatu.
Jana, Jaji Warioba aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania, alilazimika
tena kutoa kauli akisema kuwa hayupo tayari kuwajibu wanasiasa
wanaopinga muungano wa serikali tatu kwa madai kuwa tume imetimiza
wajibu wake kwa kuhakikisha wanazingatia maoni ya wananchi wengi.
Hata bila kutaja jina la chama, kauli hiyo imeilenga CCM ambayo
kupitia kwa katibu wake wa Itikadi na Uenezi, ilisema wazee
wanaoshabikia mfumo wa serikali tatu wanangoja kufa.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Habari (MCT), Warioba alisema:
“Huu sio wakati wa malumbano bali lazima tukubaliane mambo kwa maslahi
ya taifa, tujielekeze kupata katiba kwa ajili ya Watanzania wote, imguse
kila mtu.
“Tusipowasikiliza wananchi tutapata katiba ya makundi jambo ambalo si
sawa, panueni mawazo yenu mjadili rasimu kwa msingi wa wananchi kwanza.”
Aliwataka wanasiasa kuacha ubinafsi kwa kutaka kuweka mawazo yao
kwenye katiba, huku akieleza kwamba tume yake haitapokea maoni ya
wanasiasa wanaofanya mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tume yake haifanyi biashara ya malumbano
badala yake anajikita kuhakikisha taifa linapata katiba bora huku
akijisifu kwa kufanikiwa kuwa kimya licha ya tume yake kuzongwa na
maneno ya wanasiasa na asasi za kiraia.
Mwenyekiti huyo alisema tume yake ilipokea maoni mengi kutoka kwa
wananchi, lakini waliamua kuchukua mambo ya msingi kwa maslahi ya taifa.
“Hivi sasa tume ya katiba imetoa nafasi kwa mabaraza ya katiba
yanayowakilisha makundi mbalimbali ya watu kujadili rasimu hiyo kwa
kuzingatia mahitaji muhimu ya wananchi wote,” alisema.
CHADEMA kwa upande wake, imeishambulia vikali CCM kwa madai ya
kutojali maslahi ya Watanzania katika kupata katiba bora na yenye
manufaa kwa taifa.
Juzi, akizungumza mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod
Slaa alisema CCM imeamua kuwa wapinzani wakubwa wa rasimu ya katiba
mpya.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini humo, Dk. Slaa alisema CCM
wanapinga hoja nyingi ambazo zimependekezwa katika rasimu ya katiba mpya
na kuwaona viongozi kama vile Jaji Joseph Warioba anayetokana na chama
hicho tawala kama adui na msaliti.
“CHADEMA tunasema iwapo rasimu ya katiba ikichakachuliwa katika Bunge
la Katiba kwa kutumia wingi wa wanachama wa CCM, sisi CHADEMA tutatetea
haki yetu kwa wananchi,” alisema.
Alisema lazima CCM watambue kwamba amani ni tunda la haki na
imeasisiwa na viongozi waliotutangulia, hivyo ni lazima wakawa makini
kuendeleza amani hiyo iliyoachwa na viongozi waliotangulia kwa matendo
na wala siyo kwa maneno.
“Lazima haki ya kikatiba igawanywe vizuri bila ubaguzi, waondoe
unyanyasaji, na ubaguzi, watende haki, wakifanya hivyo kutakuwa hakuna
haja ya kuhubiri amani majukwaani,” alisema Dk. Slaa.
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment