Waziri mkuu, Mizengo Pinda
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini mtandao
wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri mbalimbali hapa
nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk alisema
keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze
kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri
134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na
mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye
vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za
Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo
imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa
Tamisemi, Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao
wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo
ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano
mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana
na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa
ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri
zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,
Wilson Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini
hajachukuliwa hatua na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye
alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea
kupata mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa mshahara, kodi
ya nyumba na marupurupu mengine kama ofisa aliye kazini wakati ana kesi
ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini kuwa Takukuru
inajihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na kupotosha
ukweli wa taarifa za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada
mahakamani.
Via mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Ukiangalia kesi zilizoko mahakamani ambazo upelelezi wake bado
unaendelea utaona wazi kuwa Takukuru ni miongoni mwa watu wanaopokea
rushwa, jambo ambalo limesababisha kuchelewesha upelelezi au kupindisha
ukweli,” aliwatuhumu.
Akizungumzia tuhuma hizo, Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa alisema, “Hazina kuna taratibu na sheria kuhusu matumizi
ya fedha na kama jambo hilo limefanyika kweli ni wazi kuwa litakuwa
kinyume na sheria na taratibu zilizopo.”
Alisema licha ya kuwa mpaka sasa hajasikia
malalamiko yoyote, aliahidi kufuatilia jambo hilo ili kubaini ukweli na
kwamba kama kuna mtu atabainika atachukuliwa hatua stahiki. Alisema,
“Ngoja tufuatilie ili kujua ukweli.”
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Kassim Majaliwa aliomba atafutwe leo kwa maelezo kuwa
atakuwa ameshapata maelezo ya kutosha kuhusu tuhuma hizo.
“Sijajua hizo halmashauri ni zipi, pamoja na idara
ambazo zipo chini ya wizara hii, ngoja kwanza nizungumze na wahusika
ambao pia najua watanieleza kilinachoendelea, nitafute kesho (leo)
nitatoa ufafanuzi wa kina,” alisema Majaliwa.
Kamati yawabana Mambo ya Nje
Katika hatua nyingine; Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), imemwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu
wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa hasa katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gaudence Kayombo
alisema jana alipokutana na viongozi wa wizara hiyo kuwa kuna matumizi
makubwa ya fedha katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
“Kamati itamwandikia CAG, afanye ukaguzi maalumu
ili kubaini utata unaoonekana katika matumizi ya fedha ya wizara hiyo
hasa kwenye eneo la mikutano,” alisema Kayombo.
Kayombo alisema kutokana na utata huo, kamati
imeona haiwezi kuijadili ripoti hiyo ya fedha ya mwaka 2012/13 hadi CAG
atakapofanya ukaguzi maalumu.
Aidha, Kayombo aliwataka viongozi hao wataje
gharama za Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliojengwa kwa mkopo na msaada wa
Serikali ya China, lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule alisema
ataitaja baadaye baada ya kujiridhisha.
“Tunataka kufahamu gharama za ujenzi wa jengo
hilo, vifaa vilivyosamehewa kodi ili kamati iweze kujua, kwa sababu hadi
sasa haieleweki umegharimu kiasi gani,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, alisema asilimia 46 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo ni
msaada wa Serikali ya China huku asilimia 54 ikiwa ni mkopo.Via mwananchi
0 comments:
Post a Comment