Sheikh Issa Ponda
Polisi mjini Dar es Salam Tanzania, wamedhibiti
harakati zozote za wafuasi wa mhubiri wa kiislamu nchini Tanzania
Sheikh Issa Ponda ambaye amelazwa hospitali akiuguza jeraha la risasi baada ya kupigwa risasi siku ya Jumamosi mjini Morogoro.
Wakati huohuo katika taarifa rasmi kwa vyombo
vya habari, kiongozi wa baraza la waisilamu mkoa wa Dar es Salama
(BAKWATA) amesema kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro kulikotokea
tatizo la kupigwa risasi kwa kiongozi wa kidini, Ponda ajiuzulu mara
moja.
Kiongozi huyo amesema kuwa hapakuwa
na haja ya kumpiga risasi Ponda wakati wangeweza tu kumkamata kwani
hakuwa ametatiza mpango wowote wa kukamatwa kwake.
BAKWATA pia limeitaka serikali kuunda tume
itakayochunguza kitendo cha kupigwa risasi, kwa sheikh huyo likisema
kuwa hapakuwa na sababu ya polisi kutumia nguvu dhidi ya Ponda.
Mnamo siku ya Jumapili, Jumuiya ya Taasisi za
kidini za Kiislamu nchini Tanzania imeitaka serikali kufanya uchunguzi
wa kina ili kubaini na kuwachukulia hatua watu waliompiga risasi Sheikh
Ponda Issa Ponda Jumamosi mjini Morogoro, Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es
Salaam, Baruan Muhuza, sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya
mara kwa mara na serikali ya nchi hiyo alipigwa risasi baada ya kutokea
vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa
Kundecha, amewaambia waandishi wa habari mjini humo kuwa endapo serikali
haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya
mustakabali wao na serikali ya Tanzania.
Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa,
Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa
chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera
Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana
na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi
na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa
kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua
iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata
hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi
Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi
wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi,
alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya
kilomita 200.
Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje
cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na
makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.
Chanzo: BBCswahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Chanzo: BBCswahili
0 comments:
Post a Comment