Rais Jakaya Kikwete
WAKATI sakata la dawa za kulevya likiwa limeichafua Tanzania katika uso wa kimataifa, orodha ya majina ya wanaohusika na biashara hiyo ambayo Rais Jakaya Kikwete alidai kuwa nayo, amesema amekwishaipeleka kwenye Mamlaka husika. 

Rais Kikwete mara kadhaa amekuwa akisema kuwa anayo orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya hapa nchini, hivyo gazeti hili lilimtafuta kupitia kwa msemaji wake, kufahamu suala hilo lilikofikia.

Akizungumza na gazeti hili kupitia kwa Msemaji wake, Salvatory Rweyemamu, Rais Kikwete alisema orodha ambayo alisema anayo alikwishaikabidhi kwa vyombo husika kwa ajili ya hatua zaidi.

“Rais atembee nayo mfukoni ya nini? Hata Nzowa katika taarifa yake alisema alipatiwa… wamepewa vyombo husika, Serikali haiendeshwi kwa vyombo vya habari, kuna vingi vinafanyika bila kutangazwa. Mtafute Nzowa atakwambia vyema,” alisema Rweyemamu, wakati gazeti hili lilipotaka kufahamu juu ya orodha hiyo ya Rais ilikofikia.

Orodha ambayo Rais Kikwete amekuwa akielezwa kuwa anayo, inadaiwa kuwahusisha vigogo mbalimbali nchini, wakiwemo wabunge, mawaziri na wafanyabiashara wakubwa ambao hata hivyo imebainika kuwako kwa ugumu wa kuwachukulia hatua, kutokana na kutokuwa na ushahidi ili kuwabana wahusika.

Kutokana na kauli hiyo ya Rais kupitia kwa msemaji wake, Gazeti hili liliamua kutafuta moja ya mamlaka zinazohusika kupambana na dawa za kulevya ili kufahamu juu ya orodha hiyo iliyokabidhiwa na Rais na hatua ambazo zimechukuliwa.

Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi (ACP), Godfrey Nzowa, hakukiri wala kukana kupokea orodha hiyo kutoka Ikulu.

MTANZANIA Jumapili: Kamanda sisi ni MTANZANIA Jumapili, tumepata taarifa kwamba Ikulu imekupatia majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, vipi umefikia wapi katika kuishughulikia?

NZOWA: “Kutoka wapi? Mimi napata kutoka sehemu mbalimbali, tunakuwa na watu ambao tunakamata na tunawapekua, ikithibitika tunawapeleka mahakamani

Na hivi karibuni nimepatiwa orodha ya watu 261 wanaodaiwa kufanya biashara hiyo, lakini katika upekuzi wetu hatukukuta kitu.

MTANZANIA Jumapili: Kwa hiyo hao mliowapekua ndiyo orodha mliyopatiwa kutoka Ikulu?

Nzowa: Siwezi kutaja moja kwa moja kwa sababu ninapokea orodha kutoka sehemu mbalimbali, kwa hiyo si salama kutaja jina la mtu.

Siwezi ku ‘mention’ kuwa ni Ikulu ama nani. Ushahidi wa moja kwa moja haupo, lakini wa kimazingira upo, tulipeleka kiapo ili washitakiwe Mahakamani.

Kwa mujibu wa Nzowa, wengine zaidi ya 260 waliopatikana na ushahidi wamefunguliwa kesi katika mahakama za hapa nchini.

Hivi karibuni katika Bunge linaloendelea Dodoma, kuliibuka hoja ya kuitaka serikali kutaja orodha ya wanaodaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alishindwa kufanya hivyo.

Badala yake, Lukuvi alisema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo na kwamba angetaja majina, Bunge lisingebaki salama.

Lukuvi alisisitiza kuwa serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka, kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani.

Hata hivyo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai, mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.

Pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam, ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.

Sakata la dawa za kulevya nchini lilitikisa zaidi baada ya kukamatwa kwa wasichana wawili, Agness Gerald (25) na Mellisa Edward (24) katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, (JNIA) wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150, zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 za Tanzania.

Hatua hiyo ilimlazimisha Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwafukuza kazi wafanyakazi wa JNIA, wanaodaiwa kuhusika na upitishwaji wa mzigo huo, huku baadhi ya watendaji wakihamishwa vituo vyao vya kazi.

Moto huo uliowashwa na Mwakyembe, ulikuja baada JNIA kutajwa kuwa moja ya chochoro kubwa za kupitisha dawa hizo, hali ambayo pia imeshuhudia Jeshi la Polisi kuwaondoa kwa kuwahamisha vituo vya kazi, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi (ACP) Deusdedit Kato na Mkuu wa Upelelezi wa Viwanja hivyo, David Mwafwimbo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top