Hali ya afya ya  Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi aliyelazwa katika Hospitali ya Millpark nchini Afrika Kusini inaelezwa kuwa ni mahututi.
 
Mbunge  wa  Kuteuliwa, James Mbatia akizungumza jana bungeni mjini Dodoma wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Katiba alisema, kutokana na hali ya mjumbe huyo kuwa mbaya, aliwaomba Watanzania kuendelea na sala kwa ajili yake.
Mbatia alisema, “Kwa kuwa tunazungumzia suala la katiba huku mmoja wa wajumbe wake Dk Mvungi ni mgonjwa, tunahitaji kufanya mchakato huu kwa kuweka mbele masilahi ya taifa.
“Hali yake  Dk Mvungi bado ni mbaya sana huko katika hospitali ya Millpark na anahitaji kuombewa, hivyo Watanzania wote tumwombee,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Mwananchi lilipata taarifa kutoka katika hospitali hiyo ambapo kitengo cha ICU kilithibitisha kuwa hali ya Mvungi siyo nzuri na sasa yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi.
 Daktari wa kitengo hicho ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake alisema, wanaendelea kufanya kila mbinu za kitaaluma ili kuokoa maisha ya Mtanzania huyo.
“Tunafanya kila tuwezalo kumwondoa katika hali hii kwa sababu ameumia zaidi katika mishipa ya fahamu. Tunajitahidi,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja alisema wizara inafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya Dk Mvungi ingawa hawezi kusema chochote kwani suala hilo lipo mikononi mwa familia.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top