Waziri wa zamani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mateo Qaresi akitoa maoni yake juu ya Rasimu ya Katiba Mpya katika kikao cha wajumbe wa Baraza la Katiba la wilayani Babati, jana.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Mateo Qaresi ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Pili na Tatu, ikiwamo uwaziri na ukuu wa mkoa, amesema Tanzania kama taifa halina dira wala mwelekeo na matokeo yake mambo yake yamekuwa yakienda bila utaratibu huku akishauri Katiba Mpya iruhusu Rais kushitakiwa.
 
Akitoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya jana, Qaresi ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Babati amepinga mapendekezo mengi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisema ni muhimu Katiba Mpya itaje dira ya taifa.
Qaresi katika utumishi wake wa umma, amewahi kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 - 1990, Waziri wa Utumishi, 1996 - 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi Februari 2006.
“Hivi hawa viongozi wanajua tunapoelekea, leo hii ukiulizwa dira yetu ni nini hakuna anayejua, bali tunajiendea tu,” alisema.
Alisema kwa mfano, Wamarekani licha ya kuwa na vyama viwili vikubwa, lakini dira yao ni ubepari, Wachina au Warusi dira yao ni ujamaa (ukomunisti) na kwa mataifa yote yanazo dira, lakini Tanzania dira yake haijulikani.
“Basi, watangaze kama sisi ni mabepari, wajamaa au waliberali, ili tujue na tufuate misingi hiyo siyo kila kiongozi kuwa na utaratibu wake, wengine ruksa wengine hivi lazima tubadilike,” alisema Qaresi.
Rais aondolewe kinga, ashtakiwe
Akizungumzia ibara ya 83 ya Katiba ambayo inazungumzia kinga za Rais, alisema ni muhimu sasa kuondolewa kwani marais wamekuwa na viburi , hawashauriki.
Alisema kuna makosa ambayo marais wanayafanya ambayo yanafaa kushtakiwa, lakini kutokana na kuwa na kinga, imekuwa ni vigumu kufanya hivyo.
“Katiba ijayo lazima sasa iondoe kinga kwa marais ili mtu yeyote aweze kumshtaki Rais na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa,” alisema Qaresi.
Kuhusu hoja za Kundi la G55 ambalo yeye alikuwa mwasisi na mwanachama la kutaka Serikali ya Tanganyika, alieleza kuwa Serikali tatu haziwezi kuepukika na kuwataka wanasiasa wakiwamo wa CCM kuacha ushabiki.

Qaresi ambaye alikuwa mwenyekiti wa wabunge wa kundi ya G55 mwaka 1993 waliotaka Serikali ya Tanganyika, alisema si Serikali mbili au moja ambazo sasa zitawezekana tena, kwani Wazanzibari wanataka uhuru wao wa kujiamulia mambo na kama ushabiki ukiacha muungano utavunjika kabisa.
“Hoja kuwa Serikali tatu ni gharama kubwa si ukweli, gharama kubwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma na ubadhirifu serikalini na siyo kuwa na Serikali tatu. Leo hii katika bajeti ya nchi ya Sh18.2 trilioni, ni trilioni tano tu ndiyo za maendeleo, sasa tuna Serikali tatu hapo,” alihoji.
Alisema Serikali inajiongezea matumizi makubwa bila sababu ikiwapo kuanzisha wakala katika sekta mbalimbali na kutoa mfano wa Mkurugenzi mkuu wa Wakala kama EWURA ambaye ana mshahara mkubwa zaidi ya katibu mkuu wa wizara.
“Serikali inajenga majengo makubwa bila sababu, mfano jengo la RC (Mkuu wa Mkoa) wa Manyara ni kubwa kupita kiasi hadi wahudumu wana ofisi na kuna vyumba havina watu sawa na jengo la halmashauri ya Mji wa Babati, haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisema.
Alisema wakati wao walipokuwa wanataka Serikali ya Tanganyika, hali haikuwa mbaya, lakini sasa hali ni mbaya zaidi na mahitaji ni makubwa zaidi na haiwezekani upande mmoja tu wa Muungano kuendelea kung’angania mfumo uliopo.
“Malalamiko ya kutaka Serikali tatu, hayajaanza leo, kilichomwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abdu Jumbe ni hoja hiihii na viongozi kadhaa waliondolewa pia, nadhani ndiyo sababu hata leo kuna viongozi wa Zanzibar wanaogopa kuwa wakweli na kudai nao wanataka Serikali mbili,” alisema Qaresi.
Alifafanua kuwa kwa sasa Zanzibar imefika mbali zaidi kwani ina wimbo wake wa taifa, bendera, majeshi yake kama KMKM na JKU na hata wakati wa Sherehe za Mapinduzi Rais wao (Dk Ali Mohammed Shein) ndiye anakagua gwaride kama Amiri Jeshi Mkuu.
“Ni vyema tuache ushabiki wa kisiasa na kuogopa, sasa kama tunataka Muungano ni Serikali tatu tu na wala siyo mbili au moja,”alisema.
Hoja ya uwazi
Qaresi alisema anashangaa kuna watu wanapinga uwazi kwenye tunu za taifa, kwani anashindwa kujua ni kwa manufaa ya nani.
“Kila mtu sasa anataka uwazi katika matumizi ya umma, utendaji serikalini na sehemu nyingine, sasa hawa wanaopinga wanataka nini,” alihoji.
Katika utumishi wake wa umma, amewahi kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 hadi 1990, Waziri wa Utumishi mwaka 1996 hadi 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi 2006.

Pia, alikuwa Mbunge wa Babati nwaka 1985 hadi 1995 na baadaye Mbunge wa Jimbo la Babati Magharibi mwaka 1995 hadi 2000 aliposhindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top