Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru kawambwa
 
Tarehe 10 Julai 2013, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza matokeo ya kupangwa Kidato cha 5 wanafunzi waliohitimu kidato cha 4 mwaka 2012. Katika tangazo hilo Wizara iliwahimiza wanafunzi kuripoti katika shule zao walizopangwa kabla ya tarehe 29 Julai 2013. 

Baada ya tangazo hilo, Wizara imepokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kubadili shule au machaguo (combinations) walizopangwa kwa sababu mbalimbali. 

Wizara imetafakari maombi hayo na kufanya mabadiliko ya shule/machaguo kwa wanafunzi wenye sababu zifuatazo:
Waliopangwa shule za kutwa mahali ambapo hawana pa kuishi;
  • Waliopangwa mbali sana kutoka sehemu wanazoishi;
  • Walio wagonjwa wanaohitaji kuwa karibu na hospitali;
  • Walioomba kuhamia shule za kutwa kwa sababu za kiuchumi;
  • Walioomba kubadili ‘combinations’ ambazo hazipo katika shule walizopangwa awali
Wakuu wa shule wanaelekezwa kuwapokea wanafunzi hawa katika shule hizo mpya na kuwasiliana na wakuu wa shule walizopangwa awali ili wawatumie ‘Sel form’ za wanafunzi hawa. 

Aidha, mnatakiwa kuhakiki uhalali wa kila mwanafunzi mnayempokea kwa kutumia orodha ya majina yaliyomo katika tovuti pamoja na Result Slip za wanafunzi hao. 

Wizara inawaagiza wanafunzi wote waliokubaliwa kubadilishiwa shule/combinations ambao taarifa zao zipo kwenye tovuti waripoti mara moja katika shule hizo. 

Wizara haitatoa barua kwa mwanafunzi yeyote. Aidha kuanzia sasa Wizara haitapokea maombi yoyote ya kubadilisha shule/ combinations. Endapo yatakuwepo maombi yo yote yafuate utaratibu wa kawaida wa uhamisho kupitia kwa wakuu wa shule.
Imetolewa na
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI



TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top