MWISHONI mwa mwezi uliopita Umoja wa Kampuni za Simu za Mkononi Tanzania (MOAT ) ulitoa taarifa kuhusu ongezeko la gharama za mawasiliano nchini ambalo limekuja baada ya serikali kutangaza kupandisha kiwango cha kodi katika sekta ya mawasiliano.

Kwa nujibu wa MOAT, pendekezo la serikali la kuweka kodi ya asilimia 14.5 kwenye huduma za simu za mkononi hazitaweza kukwepesha kupanda kwa gharama za simu kwa watumiaji.

Awali kodi iliyokuwa ikitozwa ni asilimia 12.5 katika huduma ya mawasiliano ya simu na kwamba ongezeko la kufikia asilimia 14.5 tofauti na nchi za jirani Kenya na Uganda ambazo zimeendelea kutoza viwango vya ushuru vya asilimia 10 na 12.5 tu ni mzigo kwa watumiaji wa huduma za simu za mkononi.

Janeth Gama ni mmoja wa Watanzania waliotoa maoni kuhusu ongezeko hili na kusema ingawa kampuni za simu zina pata faida kubwa kuliko nyingine, zinapaswa kuangalia watumiaji wa mwisho wa huduma.

Anasema suala la mawasiliano ni la kawaida, halina mwenye kipato cha chini wala kikubwa, hivyo kwa vyovyote vile wanaoumia ni wananchi.

Masunga Stephen, mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam anasema uamuzi wa kampuni za simu kukata kiasi cha sh 1,000 kwa kila anayetumia huduma ya mawasiliano kwa simu, hicho ni kiwango kikubwa kwani kuna watu wanaoishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku.

“Hali hii ni ngumu, je, itawaweka katika kundi gani hawa ambao kipato chao ni chini ya dola moja kwa siku, ambao wanamiliki simu za mikononi? Wakikatwa sh 1,000 kila mwezi kwa ajili ya kodi uchumi wao utapanda au utazidi kushuka?

“Wakati serikali ikizifikiria kampuni za simu juu ya ongezeko hili, itufikirie na sisi wananchi, kwani ni athari kubwa kwetu sote,” anasema Stephen.

Anasema ni vema serikali ikatafuta vyanzo vingine vya mapato kupitia sekta nyingine lakini si kuigusa sekta ya mawasiliano kwa kujifunza kutoka katika nchi nyingine, ambapo gharama za mawasiliano ni nafuu.

Aidha, kwa mujibu wa Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013, huduma za mawasiliano ni huduma yoyote ya maelezo inayotolewa na kampuni ya mawasiliano ya simu kwa njia ya mawasiliano kwa kutoa au kupokea sauti, maandishi, picha au taarifa ya aina yoyote kupitia mfumo wa kielektroniki.

Taarifa hiyo ya ongezeko la gharama za simu kutoka Kampuni za Vodacom, Airtel, Tigo na Zantel inatokana na mabadiliko ya muswada wa kodi wa mwaka 2013 uliopitishwa na Bunge katika kikao cha bajeti kilichokwisha Juni 28, mwaka huu kueleza kuwa muswada huo unapaswa kuanza kutumika Julai mosi mwaka huu.

Athari za kiuchumi
Mamilioni ya Watanzania wataathirika na uamuzi wa serikali kutoza kila mtumiaji wa simu sh 1,000 kwa mwezi kama kodi ya forodha.

Kutokana na ongezeko hilo lilionza Julai mosi mwaka huu, Watanzania wapatao milioni nane wataathirika kutokana na matumizi yao ya simu kutofikia sh 1,000 kwa mwezi.

Chini ya sheria hii mpya ya kodi, kampuni hizo zitalazimika kuwakata wateja wao wote sh 1,000 kwa mwezi na kuzikusanya kwa niaba ya serikali.

“Zaidi ya watumiaji wa simu milioni nane nchini wataathirika kutokana na ongezeko hilo la kodi mpya ya sh 1,000. Tanzania ina watumiaji wa simu za mkononi wapatao milioni 22 ambao ni sawa na asilimia 48 ya watumiaji wote wa simu,” inasema MOAT.

Iwapo kuna watumiaji milioni nane kwa sasa wanaotumia huduma ya mawasiliano ya simu za mikononi itakuwa ni vigumu kwa wateja wengine wapya kuunganishwa na huduma za simu hasa walioko katika maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa MOAT, kodi mpya ya sh 1,000 haibagui uwezo wa watu kulipia gharama za mawasiliano kwani mtumiaji mkubwa na mdogo wote watatakiwa kulipa kila mwezi.

MOAT imebainisha kuwa zoezi hili la kodi mpya itadhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano ya simu, ambapo tumeshuhudia huduma hizi zikizidi kuwa nafuu kwa watu wote.

Ongezeko hili litazorotesha mpango wa kimataifa wa Universal Communications Services Access Fund (UCSAF), wa kuwezesha mawasiliano nafuu kwa wote.

MOAT inasema eneo mojawapo litakaloathirika ni huduma za intaneti eneo linalohitaji kuwekewa mikakati ya kulikuza kutokana na umuhimu wake katika maisha ya sasa kiuchumi na kijamii na wala si kulizorotesha kwa kusababisha ongezeko la gharama, hivyo kuendelea kuwa na kiwango cha matumizi ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine zikiwamo za Afrika Mashariki.

Aidha, MOAT inaeleza kwamba hatua ya kuongeza kodi itakwenda kinyume cha mipango iliyopo yenye lengo la kuibadili jamii kwa kuipatia maarifa ya msingi kupitia huduma ya intaneti sambamba na mawasiliano ya simu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini ya matumizi ya huduma ya mtandao wa intaneti katika Bara la Afrika, ambapo watumiaji wa huduma hiyo ni asilimia 10 pekee ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya ambayo ina zaidi ya watumiaji asilimia 40.

Msimamo wa MOAT
“Mawasiliano ya simu si anasa bali ni huduma muhimu katika Tanzania ya leo, sasa tunawezaje kuwatoza kodi mara kwa mara watu hao hao ambao wanaitegemea huduma hiyo ili kuboresha maisha yao?” inahoji taarifa ya MOAT.

MOAT inatambua jitihada za serikali katika kukusanya kodi kwa ajili ya mipango ya maendeleo kwa wananchi.

Hata hivyo inabainisha kuwa kuanzishwa kwa kodi hiyo kunakinzana na juhudi za kuwapunguzia mizigo ya kodi wananchi wenye kipato cha chini.

MOAT imeendelea kusema kuwa kwa tozo la kodi ya mapato ya asilimia 35 kwenye sekta hiyo ya mawasiliano ya simu linatosha kiasi kwamba sekta hiyo isingeweza kubeba mzigo zaidi wa ongezeko jingine.

Hivi sasa, upanuzi wa mawasiliano na miundombinu vijijini ndiyo kipaumbele cha sekta nzima.

“Tunaamini hapa ndipo ukuaji wa sekta ya mawasiliano ya simu itakapoonekana katika miaka ijayo. Ongezeko lolote la kodi litazorotesha uwezo wetu wa kutanua huduma zetu za mawasiliano na miundombinu maeneo ya vijijini.

“Tunaelewa kuwa serikali inayafanya haya yote ili kuweza kupata fedha kwa ajili ya kusaidia kwenye huduma za jamii katika maeneo muhimu.

“Ni bahati mbaya kwamba sekta ya huduma ya mawasiliano ya simu inaendelea kubeba mzigo mkubwa wa ongezeko hili ambapo wateja watalazimika kuubeba mzigo wa ongezeko hilo,” inafafanua MOAT.

MOAT inaiomba serikali kufikiria upya juu ya tozo ya kodi hiyo mpya ya sh 1,000 ili kufanikisha ukuaji wa matumizi ya mawasiliano ya simu kwa Watanzania wote.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top