Mkurugenzi wa Usalama na Ulinzi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare
WAKATI Mkurugenzi wa Usalama na Ulinzi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare akifikishwa kizimbani kwa
makosa ya ugaidi, mjadala kuhusu video inayodaiwa kumwonyesha akipanga
njama za kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communication Ltd,
Dennis Msacky umeshika kasi na kuacha maswali mengi, Tanzania Daima
Jumatano limebaini.
Mjadala huo umeshika kasi hasa ndani ya wanachama wa CHADEMA ambao
wanaamini si jambo la kupuuzia kwani lina matokeo makubwa sana kwa
siasa, demokrasia, usalama, intelijensia na dhamira ya wanamageuzi
kutaka mabadiliko ya watawala.
Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na nani alimrekodi Lwakatare? Swali
hili ni muhimu kwa maana ya kwamba kama siyo vyombo vya usalama
(undercover) huyu aliyemrekodi ni nani?
Je, mtu huyo alikuwa na mamlaka ya kumrekodi? Je, katika kuingilia
mawasiliano ya mtu hajavunja haki za kikatiba? Kama mtu yeyote anaweza
kutumia ushahidi wa video aliyerekodi mwenyewe bila kupewa mamlaka na
polisi au vyombo vya upelelezi je, inawezekana watu wakamtega rais,
waziri mkuu au kiongozi wa umma kwa kipimo hicho hicho na polisi watatoa
uzito ule ule?
Je, ushahidi ulitunzwaje tangu uchukuliwe Desemba mwaka jana? Swali na
changamoto kubwa ni kwamba video hiyo na nyaraka nyingine
hazikuchezewa?
Kama ushahidi umekusanywa na raia tu na akakaa nao kwa miezi mitatu
(tangu Desemba hadi Machi) swali linapaswa kuuliza je, mkanda huo
umekuwa salama muda huo wote? Nani mwingine aliyeuona na kuupitia?
Kama ambavyo video hiyo inavyoonekana imetolewa kwenye mtandao wa
Youtube, swali kabla ya video hiyo kusambazwa, ilikuwa wapi na kwa nani?
Kwa wale wanaojua mambo ya audio/visual technology, siyo kazi kubwa
sana kubadilisha kitu chochote ambacho kiko kwenye mfumo wa kidijitali.
Kuanzia sauti, picha na hata mazingira yanaweza kubadilishwa vizuri tu
kwa kutumia kompyuta.
Pamoja na ushahidi huu, ni jukumu la vyombo vya usalama kuhakikisha
vinakusanya ushahidi mwingine ili kuupa nguvu ushahidi walionao.
Hii ndiyo sababu ya vyombo vya usalama kwenda kupekua nyumbani kwa Lwakatare na baadaye katika ofisi za CHADEMA.
Wadadisi wa duru za siasa nchini wanasema kuwa endapo ushahidi wa
video hii iliyorekodiwa na kurushwa kwenye mtandao utakubaliwa na
mahakama, mlango mpya wa vita dhidi ya ufisadi utakuwa umefunguliwa.
Wananchi mahali popote walipo wataweza kutumia simu na nyenzo zao
mbalimbali kuwarekodi wahalifu wa kila njama za rushwa au wakipokea
rushwa na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao bila kujulikana, na
polisi watatakiwa kufanyia kazi bila kulazimika kujua nani amerekodi au
kama katika kurekodi taarifa zimebadilishwa kwa namna fulani.
Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliomba jina
lake lihifadhiwe, alisema kuwa ukiiangalia video hiyo, utabaini kuwa
kipande kinachoonesha sehemu ya mpango au mkakati wa kufanya hivyo ni
kweli na kipande cha pili kinaonesha kwamba video hiyo ni feki na
imetengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu kuweza kufanya ionekane njama
ilipangwa.
“Katika hilo la kwanza inaonekana ndio msimamo wa polisi, Lwakatare
amekamatwa, kusachiwa nyumbani kwake na kulala rumande kuendelea na
mahojiano na hatua nyingine.
“Inaonekana polisi wanaamini kuwa video hiyo ni kweli inaonesha njama
za aina hiyo na ndiyo maana wamechukua hatua. Na ni kutokana na hili
bila ya shaka ndiyo maana wamemfikisa mahakamani,” alisema mhadhiri
huyo.
Alisema hata kama video hiyo ni ya kweli na haijachakachuliwa,
haitoshi bado kuwa ushahidi wa mpango uovu wowote hasa kama sehemu yake
ya mwanzo (ilikoanzia) na mwisho wake (ilikoishia) havipo.
“Kwa kutegemea kipande cha katikati tu bado video hiyo inakosa
muktadha wa kueleweka. Ni muhimu kwa polisi kuhakikisha wanapata sehemu
ya mwanzo na ya mwisho ya video hiyo ili kuweza kuelewa. Hili wanaweza
kupata kutoka kwa huyo aliyenao huo mkanda au aliyechukua video.
Wanaweza kumuomba awapatie mkanda mzima na ninaamini mawakili wa
Lwakatare nao watadai waone mkanda mzima siyo sehemu tu kama
ilivyooneshwa,” alisema.
Kama si kweli
Kama sakata zima la Lwakatare sio la kweli, basi wanachama na
mashabiki wa CHADEMA wanapaswa kuendelea na harakati za mabadiliko kwani
bila shaka kuelekea 2015 yanaweza kuibuka mambo mengi makubwa.
Kama suala zima la Lwakatare si kweli, polisi bado wana jukumu la
kuhakikisha wanamtafuta na kumpata mtu aliyetengeneza mkanda huo na
kumtia mbaroni kwani anafanya uchochezi kama wanavyomtuhumu Lwakatare.
Tena mtu huyo anaweza kufanya uchochezi wa hatari zaidi kwa namna yake
kwani amejaribu kuwaaminisha wananchi kuwa chama kizima cha kisiasa
kinahusika na matukio ya utekaji nyara kama mtu kasoma maelezo ya huyo
aliyeiweka kwenye mtandao video hiyo, kwani hakuishia kumtuhumu
Lwakatare tu bali CHADEMA kama chama na viongozi wake wakuu.
Hata hivyo, jukumu la kuthibitisha ukweli wa video hiyo kama inaweza kukubaliwa kuwa ni ushahidi liko mikononi mwa polisi.
Haitoshi tu kusema Lwakatare ameonekana akisema hili au lile; ni
jukumu la polisi kuonesha kuwa ushahidi huo umepatikana kwa njia halali
na ambao haukuharibiwa kwa namna yoyote ile.
Kama sio kweli na mahakama ikashindwa kuwatia hatiani wahusika, basi
uongozi wa polisi nao utatakiwa uwajibike kwa kuboronga uchunguzi huu na
zaidi ya hapo itabidi ihakikishe kuwa wahusika waliotengeneza video
hiyo (kama imechakachuliwa) nao wanakutana na mkono wa sheria vile vile.
Na hata kama itaonekana ni kweli Lwakatare alisema anayodaiwa kusema,
ni jukumu la polisi kuonesha kuwa alikuwa amevunja sheria.
Kama ni kweli
Kama ni kweli Lwakatare amehusika na mkanda ni wake, basi Jeshi la
Polisi halina jinsi isipokuwa kufuata mwanzo wa hilo sakata hadi mwisho
wake kuwakamata wahusika wote yaani Lwakatare, yule aliyekuwa anahojiana
naye, na wale ambao walikuwa wameamua kuufadhili mpango huo.
Endapo utakuwepo ushahidi wowote wenye kuonesha kuhusika ama moja kwa
moja au kwa namna moja wamehusika, basi CHADEMA inapaswa ijichunguze
yenyewe.
Kama Lwakatare alikuwa anapanga hayo akiwa anatekeleza amri au agizo
kutoka kwa kiongozi yeyote wa chama basi kiongozi huyo akitajwa na
ikithibitika mahakamani kuhusika kwake atapaswa kujiuzulu mara moja.
Kama video itaonekana kweli imechakachuliwa basi vyombo vya usalama
vitatakiwa kutumia ari na nguvu ile ile waliyoitumia kwa Lwakatare
kuitumia dhidi ya wahusika wa video hii kwani kuwaachilia, kuwapuuzia ni
kukaribisha watu wengine kuanza kutengeneza makorokocho ya aina hii.
Lwakatare na Ludovick Joseph ambao walikamatwa katika tarehe tofauti
mapema mwezi huu wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya ugaidi.
Katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao wanadaiwa kula njama kwa nia
ya kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky kwa
sumu, kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.
Katika shtaka la pili wanadaiwa kwa pamoja kula njama za kutaka
kumteka Msacky na katika shitaka la tatu wanadaiwa kufanya mkutano wa
vitendo vya kigaidi.
Katika shtaka la nne linalomkabili Lwakatare peke yake ni la kuwezesha
kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23 (a) cha kuzuia
ugaidi nyumbani kwake.
Washitakiwa hao ambao wako mahabusu, huenda wakapewa dhamana leo
wakati mahakama itakapokuwa ikitoa uamuzi wa kupewa dhamana au la.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment