JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF), limetoa tamko kali kuhusiana na
kuzorota kwa mahusiano baina ya Wakristo, Waislamu na msimamo wa
serikali.
TCF imeeleza kusikitishwa kwake na mgogoro uliotokea hivi karibuni
kuhusiana na nani anastahili kuchinja ambapo wameeleza kuwa wanashindwa
kuelewa msimamo wa Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine waandamizi
kupata kigugumizi kuhusiana na suala hilo.
“Tumeshindwa kabisa kuelewa msimamo wa Rais Kikwete na viongozi
wengine wa serikali. Wakati wa Serikali ya Rais mstaafu Ali Hassan
Mwinyi ambaye pia ni Muislamu, ilipotokea ugomvi wa mabucha ya nyama ya
nguruwe Dar es Salaam, rais huyo kwa kulinda katiba ya nchi ambayo
aliapa kuilinda, alisema mwenyewe kwa nguvu zote kuwa kila mtu ana uhuru
wa kula anachotaka na mtu wa dini moja asimhukumu mwingine kwa kile
anachokula. Baada ya kusema hivyo hali ikawa ya amani, kwanini Rais
Kikwete anapata kigugumizi kuhusu nani achinje?” ilisema taarifa hiyo
iliyosaniwa na maaskofu hao.
Tamko hilo lilitolewa kwa niaba ya viongozi wa TCF na Askofu Peter
Kitula wa Umoja wa Wakristo (CCT), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa
Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu Batholomeo Sheggah wa Baraza
la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (PCT).
Walisema kuwa serikali
imekuwa na kigugumizi kuhusu nani achinje, hivyo wanaitaka iweke
utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu.
“Kila Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka na
Wakristo wote Tanzania waelewe kuwa hawajavunja sheria yoyote ya nchi
wakiamua kuchinja kitoweo chao wenyewe,” lilisema tamko hilo.
Pia walieleza kwa kuwa zipo bidhaa zilizoandikwa neno ‘Halal’ na
nyingine zisizo na nembo, hivyo ni dhahiri kuwa vyakula hivyo
vimegawanyika kwa kufuata misingi ya imani za dini.
Maaskofu hao pia walisema kuwa wanatambua kuchinja ni ibada ya
Waislamu lakini wametaka Wakristo wasilazimishwe kula nyama
zilizochinjwa kwa misingi ya ibada ya Waislamu na kuitaka serikali
itamke wazi kuwa kila raia ana uhuru wa kufuata imani yake katika suala
hilo.
Uchomaji wa makanisa
Kuhusiana na suala la uchomaji wa makanisa ulioambatana na mauaji ya
viongozi wa dini, maaskofu hao wamelaani na kueleza kuwa serikali na
vyombo vya usalama wa taifa wameshindwa kuchukua hatua kwa wakati, hivyo
kuonesha udhaifu na kuliaminisha kanisa kuwa serikali ina ajenda ya
siri dhidi ya Ukristo.
TCF imeitaka serikali kutenda haki kwa usawa bila ubaguzi kwani
kinachoonekana ni kushindwa kuheshimu katiba juu ya haki za raia hali
inayosababisha waamini wa dini ya Kikristo kukosa imani na serikali
iliyoko madarakani.
“Jukumu la kulinda raia ni haki ya kikatiba na kisheria, serikali
inatakiwa iwalinde raia wake, kama imeshindwa kanisa linataka serikali
ikiri hivyo ili kanisa liwaambie wananchi waiwajibishe serikali na
viongozi wake kwa kushindwa kutimiza wajibu wake,” walisema maaskofu
hao.
Aidha, walisema endapo serikali haitachukua hatua za makusudi, kanisa
litachukua hatua ya kuwaambia waamini wake kuwa inaibeba dini moja na
kutafakari upya uhusiano wake na serikali.
Pia walitaka serikali kuwahakikishia Wakristo walioko Zanzibar usalama na mali zao kwani wana haki kikatiba.
“Kigezo cha unyanyasaji wa Wakristo walioko Zanzibar ni suala la dini
na muungano, inaonekana kama vile Watanzania waliozaliwa Bara hawana
haki ya kuishi visiwani, wakati waliozaliwa visiwani wafikapo bara wana
haki zote, ni vyema serikali ichukue hatua za makusudi za kuzuia vitisho
na mauaji kwa viongozi wa kanisa na Wakristo,” ilisema taarifa hiyo.
TCF ilikutana Machi 8, mwaka huu katika mkutano wa dharura
ulioshirikisha maaskofu 177 na kutoa maazimio hayo pamoja na kuwataka
Wakristo wote kuwa watulivu na kufunga na kuomba kwa siku saba kuanzia
Machi 24 hadi 30, mwaka huu.
Tamko hilo limekuja kufuatia tukio la mchungaji wa Kanisa la
Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT) Buseresere, Wilaya ya
Chato, Mathayo Kachila (45) kufariki dunia huku watu wengine 15
wakijeruhiwa kwa mapanga kufuatia vurugu zilizotokana na mgogoro wa
kuchinja.
Katika vurugu hizo nyama ndani ya bucha hiyo ilimwagiwa maji, ikiwamo kuharibiwa kwa madirisha na milango yake.
Tukio lingine ni la Padri Evarist Mushi, ambaye alikuwa paroko wa
parokia ya Minara Miwili - Mtoni Zanzibar kupigwa risasi na watu
wasiojulikana na kuuawa.
Padri huyo aliuawa wakati akijiandaa kuingia kanisani akitokea kwenye
gari yake ambapo ghafla ilitokea gari ndogo na waliokuwamo ndani ya gari
ile wakamrushia risasi.
Pia katika tukio lingine makanisa kadhaa yalichomwa moto na Padri
Ambrose Mkenda, kushambuliwa na risasi huku kukiwako na vitisho pamoja
na vipeperushi vilivyoeleza kuwa kushambuliwa kwa padri huyo sio mwisho
wa mapambano.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment