RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na ujumbe kutoka Kituo cha Biashara Duniani (ICT), na kueleza kuwa  hatua za kutumia tasnia ya malibunifu na kuipa karafuu ya Zanzibar utambulisho (branding) maalum utaimarisha uchumi na kuitangaza Zanzibar katika soko la Kimataifa.
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na Ujumbe wa Kituo cha Biashara Duniani (ICT), Ikulu Mjini Zanzibar, ujumbe ambao umeongozwa na Bwana Jacky Charbonneau kutoka kituo hicho.
 
Dk. Shein alipongeza mashirikiano yaliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya Biashara, Viwanda na Masoko pamoja na Shirika la Mali Bunifu (World Intellectual Propety Organization) na Kituo cha Kibiashara cha Kimataifa (ICT) katika kuhakikisha karafuu ya Zanzibar inapata utambulisho na kuimarisha soko lake.
 
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa tayari nchi nyingi za Afrika ikiwemo Ethoipia imeshalipa utambulisho zao lake la kahawa na kulifanya kuwa na soko la uhakika na kutambuliwa, hivyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nayo imeona haja kwa zao lake la karafuu kulipa hadhi hiyo ili liweze kufanya vizuri katika soko la kimataifa.
 
Dk. Shein alisema kuwa licha ya sekta ya utalii kuchukua sehemu kubwa katika kuipatia Zanzibar fedha za kigeni bado zao la karafuu linaendelea kuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
 
Aidha, Dk. Shein aliunga mkono juhudi za Kituo hicho kuwa na azma ya kuitangaza Zanzibar kupitia utambulisho wa karafuu duniani, hatua ambayo itaimarisha sekta ya utalii nchini.
 
Alisema kuwa kutokana na juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya utalii hatua hiyo nayo itasaidia katika kuunga mkono sio tu sekta ya biashara na kilimo bali pia, utalii wa Zanzibar nao utaimarika kwani utapata kutangwaza duniani kote.
 
Alieleza kuwa zao la karafuu ni zao muhimu sana hapa Zanzibar na limekuwa likisaidia kuimarisha maisha ya wananchi walio wengi hivyo hatua hizo pia, zitasaidia kuimarisha uchumi wan chi ambao pia, wananchi nao watanufaika.
 
Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa Wizara hiyo imekuwa na mashirikiano makubwa na Kituo cha Kibiashara Duniani (ICT) pamoja na Shirika la Mali Bunifu (WIPO), katika kuhakikisha kuwa karafuu ya Zanzibar inapatiwa utambulisho maalum.
 
Alisema kuwa tayari ujumbe huo umeshatoa mafunzo mbali mbali kwa wahusika tofauti pamoja na kufanya mkutano na uongozi wa Wizara hiyo hatua ambayo itasaidia katika kutoa mchango wa kufanikisha zoezi hilo.
 
Waziri Mazrui alisema kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha si zaidi ya miaka miwili mkakati huo utakuwa umekamilika na kuweza kuitangaza karafuu ya Zanzibar Kimataifa na kuweza kupata soko bora.
 
Alisema kuwa  ameridhika  na washirika hao jinsi wanavyofanya kazi kwa mashirikiano na Wizara hiyo hali ambayo imetokana na wao wenyewe kuipenda Zanzibar.
 
Sambamba na hayo, Waziri huyo alieleza kuwa baada ya kuridhishwa na hatua katika maandiko ya Mradi, Serikali iliwekeana saini Hati ya Makubaliano(MoU) kati yake na WIPO pamoja na ICT na tayari hatua nzuri imeshafikiwa katika  utekelezaji.
 
Nao Ujumbe huo ukiongozwa na Bwana  Jacky Charbonneau kutoka kituo hicho cha ICT, ulieleza kuwa utahakikisha unachukua juhudi zinazohitajika katika kuifanyia utambulisho karafuu ya Zanzibar ili pia kuitangaza Zanzibar katika biashara za Kimataifa.
 
Alisema kuwa mbali ya utambulisho huo hatua hiyo itaimarisha bei hata kwa wakulima ambao nao hatimae watanufaika katika mauzo yao ya karafuu sanjari na kuinua sekta ya utalii kutokana na utambulisho huo wa karafuu za Zanzibar.
 
Bwana Jaky alieleza kuwa kazi zao wameweza kuzitekeleza kwa haraka sana kutokana na mashirikiano waliyoyapata kutoka uongozi wa Wizara ya Biasahara, Viwanda na Masoko huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa utambulisho huo kutambunguza wizi na kuhakikisha haiba ya karafuu ya Zanzibar inabakia na uasilia wake.
 
Pamoja na hayo, ujumbe huo ulieleza kuwa tayari hatua za kuitangaza Zanzibar katika soko la Kimataifa zimeshaanza kuchukuliwa na kukamilika kwake kutapelekea mtumiaji wa mwisho wa karafuu ataweza kuwasiliana moja kwa moja Zanzibar kupitia Shirika husika la Biashara ya zao hilo (ZSTC).  
 
Sambamba na hayo, ujumbe huo ulieleza kuwa utahakikisha kuwa Zanzibar inasajiliwa na WIPO kupitia Mrajis Mkuu wa Serikali wa hapa Zanzibar.
 
Kutokana na mwenendo wa uzalishaji wa zao la karafuu na kupunguza kwa mchango wake katika shughuli za uchumi na uchangiaji wa fedha za kigeni, ulisukuma Serikali kuweka mkazo maalum katika kuliimarisha zao hilo ikiwa ni pamoja na kuipatia karafuu ya Zanzibar utambulisho.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top