Mjumbe wa Bunge la Katiba, Zitto Kabwe
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Zitto Kabwe amesema kuandikwa kwa
Katiba isiyokubaliwa na pande zote kutasababisha gharama kubwa kuliko
zile zinazotajwa za serikali tatu.
Akichangia hoja kwenye Bunge hilo jana, Zitto
alisema kuna kila sababu ya kukaa na kukubaliana ili kupata Katiba
itakayokubalika pande zote.
“Muundo wa Muungano una hatari ya kuvunjika iwapo
hakuna matakwa ya dhati ya watu kuungana... Maneno ya kusema Serikali
tatu zitavunja Muungano ni ya siasa na hayana msingi wa kisayansi. Urusi
ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na siyo sababu ya idadi ya
Serikali,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema hofu ya gharama inayotajwa katika
uendeshaji wa muundo wa serikali tatu haina msingi wowote kwa kuwa
hakuna ushahidi wa kitaalamu unaothibitisha gharama hizo.
“Nimesikia watu wanasema eti tutalazimika kujenga
ikulu mpya, nani kasema lazima tuwe na marais watatu? Tunaweza kuwa na
rais mmoja kwenye nchi na wakuu wa nchi washirika wawili… Ni jambo la
makubaliano tu,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka huu ni Sh18 trilioni, kati
ya hizo Sh5.3 trilioni ndizo zinazohudumia wizara za Muungano, lakini
serikali ina uwezo wa kukusanya kodi zaidi ya Sh10 trilioni pamoja na
mapato mengine.
“Kuna jumla ya Sh2.3 trilioni hatuzikusanyi kila
mwaka kutoka kwenye kampuni kubwa, kwa uwezo wetu wa pato la ndani
asilimia 17 tunao uwezo wa kuendesha serikali ya muundo wa idadi yoyote.
“Hofu ya Serikali ya Muungano kutokuwa na fedha ni
sababu halisi, ni kweli kwamba ushuru wa bidhaa pekee yake hauwezi
kutuendeshea serikali. Sasa nini kazi yetu, tunaingia hapa ili kuboresha
hayo maeneo, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?” alihoji.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Jussa akomaa
Mjumbe wa Bunge hilo, Ismail Jussa jana
alisisitiza kwamba Wazanzibari wengi hawapo tayari kuendelea na mfumo wa
serikali mbili kwa sababu unawatesa na kuwadhalilisha.
Jussa ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar kupitia CUF, alisema haoni haya kuzungumzia suala hilo kwa
niaba ya Wazanzibari.
“Hoja nyingi zimetoka (kuhusu Muungano), lakini
naendelea kuzungumza kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na katika hili
sioni haya kwa sababu naamini kwamba wanakisimamia kile ambacho sisi
tunasimamia nacho ni Zanzibar yenye mamlaka kamili,” alisema Jussa.
Alisema amekuwa akijiuliza kwa nini serikali mbili
zinang’ang’aniwa na CCM licha ya kunung’unikiwa na baadhi ya wanachama
wake kwa miaka 50?
“Hapa wala maneno hayo hayajasemwa na CUF, wala na
mpinzani. Hapa ninayo Ripoti ya Amina Salum Ali ya Novemba 1992
ikiorodhesha matatizo lukuki ya mfumo wa serikali mbili na wajumbe wake
hawa wote walikuwa ni kutoka CCM, mwenyekiti wake Amina Salum Ali,
katibu wake Ali Juma Shamhuna ndiyo walioleta ripoti hii,” alisema Jussa
huku akionyesha ripoti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema anaona ni
kuwadanganya Wazanzibari kwamba serikali mbili zitatatua matatizo yao,
hivyo kuwafanya wajiulize mbona hazikuyatatua kwa miaka 50 iliyopita?
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment