UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, tumekuwepo hapa Bungeni,
Dodoma kwa takriban siku 11 ambapo leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa
katika Mkutano wa Kumi wa Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba
nitumie nafasi hii kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza Wapendwa
wao katika ajali mbalimbali zilizotokea hapa Nchini, ikiwemo ajali ya Jahazi la
Sunrise iliyotokea Wangwi katika
Bahari ya Hindi na Ajali ya Lori kule Mbarali ambapo Watu wamepoteza maisha na
kupata majeraha. Aidha, tunawapa pole Majeruhi wote na Abiria waliopoteza mali
katika ajali hizo. Kwa kipekee kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na
Marafiki wa Askofu Thomas Laiser wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha
ambaye amefariki jana Mchana na Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa
Katoliki, Jimbo la Moshi ambaye
amefariki Usiku wa kuamkia leo huko Nairobi alikokuwa anapata matibabu. Wote tunawapa pole sana!
SHUGHULI
ZA BUNGE
a)
Maswali
3.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu
jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa majibu.
Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na
kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
b) Miswada
4.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu,
Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya Kwanza:
i)
Muswada
wa Sheria ya Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies Bill, 2013]; na
ii)
Muswada
wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013 [The Written Laws Miscellaneous Amendments, Bill 2013].
5.
Mheshimiwa Spika, Muswada wa
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012 [The Written Laws Miscellaneous Ammendments (No. 3) Act, 2012]
ulisomwa kwa mara ya Pili na kupitia ngazi zake zote;
c) Hoja Binafsi za Wabunge
6.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu,
pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa
ya kuwasilisha Hoja Binafsi kama ifuatavyo:
i)
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi ya kuitaka
Serikali iwasilishe Bungeni Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu
ya Juu (The Higher Education Fund Act);
ii)
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kuhusu udhaifu
ulioko katika Sekta ya Elimu Nchini;
iii)
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega ya kuitaka
Serikali ianzishe Mpango Maalum wa Kukuza Ajira kwa Vijana na kuanzisha Mfuko
wa Mikopo ya Vyama Wanaowekeza kwenye Kilimo na Viwanda vyenye uhusiano wa moja
kwa moja na Kilimo; na
iv)
Hoja
Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Ubungo juu ya Kuboresha
Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es
Salaam.
d) Maazimio
7.
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Maazimio Mawili yafuatayo:
i)
Azimio
la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu
wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na Wakala wa Ki-Diplomasia (Convention on The Prevention and Punishment
of Crimes Against Internationally Protected Persons Including Diplomatic Agents
1973); na
ii)
Azimio
la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo vya Ugaidi wa
Kutumia Nyuklia (International Convention
for Suppression of Act of Neuclear Terrorism, 2009).
Ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa kukamilisha Mijadala hiyo.
UJENZI
WA UMOJA WA KITAIFA
8.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Taifa
letu limejaliwa na Mwenyezi Mungu kutimiza miaka zaidi ya 51 sasa ya Uhuru likiwa
bado linaendelea kudumisha Umoja wa Kitaifa.
Umoja huu wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na
misingi imara ya Amani, Utulivu na Mshikamano. Mimi naamini sote tunapaswa
kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao ni Tunu kubwa na nguzo muhimu ya maendeleo
yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa Kitaifa tunaoshuhudia leo uliwekwa na malezi
mazuri ya Waasisi wa Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kujenga Jamii
inayozingatia misingi ya Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Ni jukumu la kila
Mwananchi kulinda Umoja huu ambao hauna mbadala.
9.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina
Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa
Mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya
Watu Milioni 44.929. Aidha, hivi
sasa tuna Madhehebu ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zaidi ya 6,675 na tumejenga Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ambapo hadi
sasa tuna Vyama vya Siasa 19 ambavyo
vimepata Usajili wa Kudumu. Licha ya kuwepo kwa Idadi kubwa ya Watu wa Makabila
tofauti yenye desturi mbalimbali na makundi mbalimbali ya Madhehebu ya Dini,
Itikadi za Kisiasa na Watu wenye Rangi mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana
na hatubaguani kwa namna yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa
Kitaifa na Kimataifa na mfano wa kuigwa.
10.
Kutokana
na Demokrasi pana iliyopo, Wananchi wetu wana Uhuru mkubwa wa kutoa maoni,
kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Siasa pamoja na kushiriki katika kuchagua
Viongozi wa Chama chochote wanachokipenda kwa kuzingatia Misingi ya Katiba na
Sheria za Nchi. Vilevile, Serikali imetoa uhuru mkubwa wa kupata na kutoa
habari kwa uwazi bila vikwazo vyovyote kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni
mbalimbali na Maadili ya Vyombo vya Habari. Kutokana na Uhuru huo, Idadi ya
Vyombo vya Habari imeongezeka sana ambapo hadi sasa Idadi ya Vituo 86 vya Redio vilivyopewa Leseni na vinafanyakazi,
Vituo vya Televisheni 26 na Magazeti
768 yaliyoandikishwa na yanayotolewa
na Taasisi mbalimbali.
11.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio
hayo yanayodhihirika wazi, hivi karibuni kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa yetu
nzuri ya Umoja wa Kitaifa na Amani ambayo imedumu kwa miaka mingi. Tumeshuhudia
Wananchi mmoja mmoja wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni
mwao. Aidha, tumeshuhudia Vyama vya Siasa vikionesha dalili ya kuhamasisha
Wanachama wao kuingia kwenye
malumbano ya Siasa
baina yao wenyewe
kwa wenyewe au baina ya Chama
kimoja cha Siasa na Chama kingine. Baadhi ya Wanachama wameshikana mashati na
kujeruhiana.
12.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa
hii kuwaasa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuepuka kutumia majukwaa ya Siasa
kuvuruga Amani yetu na Utulivu uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na
kuhamasisha Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga
chuki na uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali iliyopo
madarakani. Pamoja na kutofautiana kwa
mawazo na Sera za Vyama vya Siasa, ni muhimu tujenge mazingira ya kuvumiliana
kwa hali ya juu katika kujenga Demokrasia ya kweli hapa Nchini. Viongozi wa
Vyama wanatakiwa kueleza Sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana
na kuzomeana. Tujenge Nchi yetu kwa Amani na Utulivu ndipo tutapata maendeleo
endelevu.
13.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia kuibuka
kwa choko choko za Kidini. Baadhi ya Waumini wa Dini wamekuwa wakikashifu Dini
nyingine kwa kejeli na vitendo vingine visivyostahili. Aidha, baadhi ya
Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa wakiwaingiza Waumini wao katika Migogoro
isiyoisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia Waumini Wasiabudu
siku za Ibada. Napenda kusisitiza kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi kubwa ya
kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na mshikamano. Nawaomba Viongozi wa Madhehebu
ya Dini kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha Waumini wao kuthamini,
kujenga na kuenzi Amani na Utulivu uliopo Nchini. Serikali imetoa uhuru wa
Wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya
Dini moja kukashifu Dini nyingine. Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote choko
choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza katika sehemu mbalimbali Nchini.
14.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi yao yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa
mbele katika kuwarubuni Wananchi kufanya vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu wa
Amani. Napenda kusisitiza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa
la kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa
Mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi
kuvuruga Amani.
15.
Mheshimiwa Spika, nigusie pia Vyombo
vya Habari, ambapo kumekuwa na kutiliana mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo
kuandika habari za Uchochezi, hivyo kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano
wa Kitaifa tuliojijengea. Vyombo vya Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha
Umma na kuhabarisha kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo
wenzetu jirani, husan Vyombo vya Habari vya Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi
vina fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha Amani na Utulivu Nchini.
Tufanye Nini
16.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
changamoto zilizopo za baadhi ya Watu waotaka kubomoa Umoja wa Taifa letu na
kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi kama Taifa hatuna budi kufanya
yafuatayo:
i)
Serikali,
Wananchi na Wadau wote ikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya
Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, n.k. tunapaswa tukae chini tuzungumze
na kutafakari kuhusu hali hii;
ii)
Tunapaswa
kwa namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia Utamaduni wa
Kitanzania na Misingi ya Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu; na
iii)
Wananchi
wote tuzingatie na kuheshimu Utawala Bora wa Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizopo.
17.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa
hii kuwaomba sana Wananchi na Watanzania wenzangu kuendeleza umoja na
mshikamano wa Kitaifa ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo
Nchini. Ni vyema kutambua kuwa Amani
na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira
wezeshi ya kusaidia kila mmoja wetu
kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo. Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya
Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha kwamba, Umoja tuliojijengea
unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Vyombo vya Dola ni lazima
zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu. Vilevile,
kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei. Naziomba
Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha kuwa,
pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.
HALI YA CHAKULA NCHINI
i)
Hali ya Mazao na Mvua
18.
Mheshimiwa
Spika, tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula Nchini
na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa,
yale yanayopata mvua za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora,
na Mtwara mazao mengi yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji. Inatarajiwa
kwamba, endapo mvua hizi zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo
hayo utakuwa mzuri.
19.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo
ya hewa, tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi
Januari 2013 inaonesha upungufu wa chakula katika Wilaya 47 zilizoko katika Mikoa 15
ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika vipindi tofauti. Inakadiriwa kuwa
jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji
jumla ya Tani 32,870 za chakula.
ii) Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
20.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
matarajio hayo ya uhaba wa Chakula, Serikali itahakikisha kuwa Kitengo cha
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo
yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa jumla ya Tani 20,000 zilishatolewa kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara,
Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora. Aidha, Kitengo hicho (NFRA) kitaendelea
kununua nafaka mapema baada ya mavuno ili kuhakikisha kuwa Serikali ina hifadhi
ya kutosha ya chakula kwa ajili ya kusambaza katika maeneo yatakayokuwa na
uhaba wa chakula. Hadi tarehe 6 Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula
lilikuwa na jumla ya Tani 68,712.9
za mahindi pamoja na Tani 3,335.989
za Mtama.
21.
Serikali
itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji wa chakula Nchini na kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi
atakayepoteza maisha kutokana na njaa. Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuweka
utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya mavuno yao baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba
ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao yote.
MAPAMBANO DHIDI YA
UGONJWA WA MALARIA NCHINI
i)
Hali Halisi ya
Ugonjwa wa Malaria Nchini
22.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inayo
changamoto kubwa ya kukabiliana na Magonjwa makubwa Duniani, yakiwemo Malaria,
Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k. Niruhusu leo katika Hotuba yangu
nizungumzie kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa wa Malaria bado unaongoza
kuwa sababu kubwa za Wagonjwa wengi wanaohudhuria katika Vituo vya huduma za
Afya Nchini. Aidha, ugonjwa huu unaongoza kwa kusababisha vifo, hasa kwa Watoto
walio chini ya umri wa miaka Mitano. Takwimu kutoka Vituo vya kutolea huduma ya
Afya Nchini zinaonesha kuwa, takriban Wagonjwa Milioni 11 hadi 12
huhudhuria katika Vituo vya huduma za Afya kwa sababu ya ugonjwa wa Malaria.
Vilevile, tafiti zilizofanyika katika Jamii [Tanzania
HIV/Malaria Indicator Survey (THMIS) 2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya wana
maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria.
ii) Jitihada za Serikali katika kumaliza
tatizo la Malaria Nchini
23.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo hili katika kuhakikisha
Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi dhidi ya ugonjwa wa Malaria,
Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja: Kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa
Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013) ambao una
lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni.
Utekelezaji wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau
mbalimbali hadi katika ngazi ya Jamii;
Pili: Kusambaza na kuongeza matumizi ya vyandarua vyenye
viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya. Hadi sasa zaidi ya vyandarua Milioni
26 vimesambazwa kupitia Kampeni iliyolenga Watoto wenye umri chini ya miaka
Mitano;
Tatu: Kutekeleza Mpango wa Hati Punguzo unaolenga kuhakikisha Akina
Mama Wajawazito na Watoto wanaozaliwa wanaendelea kupata vyandarua hivyo na
kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria;
Nne: Kuendeleza Mpango wa kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili
kutokomeza mazalia ya Mbu. Mpango huo unaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya
Kagera, Mwanza na Mara ambapo zaidi ya Kaya 1,440,000 sawa na Asilimia
90 katika Wilaya za Mikoa hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu. Kutokana na
Mpango huo, zaidi ya Watu 6,500,000 wameendelea kukingwa dhidi ya
maambukizi ya ugonjwa wa Malaria;
Tano: Kuendeleza Mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia
njia za Kibaiolojia. Mpango huu ambao unafanywa na Serikali kwa ushirikiano na
Serikali ya Nchi ya Cuba unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia
mwaka 2011;
Sita: Kutumia Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa Malaria isiyo kali
kwa kutumia Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine
(ALu). Mwongozo huu unaendelea kutumika katika Vituo vyote vya Umma vya
kutolea huduma za Afya; na
Saba: Kusambaza kipimo cha haraka cha kutambua na kuthibitisha uwepo
wa vimelea vya Malaria kwenye damu katika Vituo vyote vya Umma vya kutoa huduma
za afya Nchini.
iii) Changamoto
24.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio
hayo makubwa yaliyopatikana, bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa
kazi. Changamoto hizo ni pamoja na:
Moja: Kujitokeza kwa usugu wa mbu
dhidi ya viuatilifu vya aina ya “pyrethroids”
vinavyotumika katika vyandarua na unyuziaji dawa ya ukoko majumbani;
Pili: Kupata vyanzo zaidi vya
fedha za ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya ukoko majumbani;
Tatu: Uwezo mdogo wa uzalishaji wa
dawa za kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza kuangamiza Viluwiluwi hivyo
katika Jiji la Dar es Salaam; na
Nne: Kuendeleza uhamasishaji
Wananchi kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa inayohitaji
ushiriki wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya Mbu.
iv) Matarajio ya Mkutano wa United Against Malaria – Afrika Kusini
25.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za
kupambana na Malaria Duniani, Shirika la Roll
Back Malaria Partnership wakishirikiana na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini
wanatarajia kufanya Mkutano mkubwa unaohusu mapambano dhidi ya Malaria kwa Nchi
za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia tarehe 9 - 11
Februari, 2013. Mkutano huo unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi ya juu
kutoka Nchi za SADC ikiwa ni pamoja na baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa Afya na
Mawaziri wa Michezo katika Nchi hizo.
Mkutano huo pia utajumuisha Viongozi wa juu wa Makampuni mbalimbali ya Sekta
Binafsi.
26.
Mheshimiwa Spika, lengo la Mkutano huo
ni kukutanisha Viongozi mbalimbali kwa lengo la kuendesha mjadala kuhusu janga
la Malaria katika Nchi za Afrika; ikizingatiwa kuwa ufadhili wa utekelezaji wa
mikakati mbalimbali unazidi kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa chachu kwa
Viongozi kuongeza Bajeti za udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza
ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira
wa Miguu katika dhana nzima ya Mpango
wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kuongeza
kasi ya Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Nchi hizo.
27.
Ni
matumaini yangu kuwa, Mkutano huo utakuwa wa mafanikio makubwa kwa Nchi za
Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, utatupatia
uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria.
v) Jitihada za Chama cha Wabunge cha
Kupambana na Malaria
28.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kupambana na Malaria Nchini, Muungano
wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania walianzisha Asasi
inayojulikana kama Tanzania Parliamentary
Against Malaria (TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii ni kuongeza
utashi wa Kisiasa katika kushiriki na kutekeleza Mpango na Sera ya Taifa ya kutokomeza Ugonjwa
wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa mwaka 2008 na hadi sasa imetekeleza
masuala mbalimbali katika jitihada zake za kupambana na Malaria Nchini kama
ifuatavyo:
Moja: Ugawaji wa Vyandarua kwa Watoto
wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro
na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500
walifaidika na huduma hii;
Pili: Kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa
Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania na kuona uwezekano
wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya Malaria Tanzania. Aidha,
walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria
No More ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza kwa Mradi wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;
Tatu: Kushiriki Kikao cha Nchi za Jumuiya ya Ulaya Nchini
Ufaransa mwaka 2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika
Kupamabana na Malaria Nchini;
Nne: Kushiriki kutayarisha Mwongozo (Advocacy Guideline) utakaotumiwa na
Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa Kisiasa na Kijamii katika Utekelezaji
na ushawishi wao katika kutokomeza Malaria Tanzania.
29.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii
kuwapongeza Wajumbe wote wa TAPAMA chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said Lulida,
Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na Wadau
wengine Nchini na Duniani katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Nazipongeza pia
Taasisi Zisizo za Kiserikali kwa ujumla wao ambazo zimejitokeza katika
Mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali, yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Saratani,
n.k. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge zaidi wazidi kujiunga na Asasi hizi na hasa
za Magonwa ili kuweka hamasa kwa Wananchi katika Kupambana na Maradhi hayo. Aidha,
natoa wito kwa Wananchi wote kwa ujumla kuunganisha nguvu za Kupambana na
Ugonjwa huu wa Malaria ili kunusuru nguvukazi ya Watanzania. Suala kubwa ni
kuzingatia masharti ya Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira yetu na
kutumia Vyandarua kama kinga iliyo ya uhakika.
LISHE
30.
Mheshimiwa Spika, wakati nikitoa hoja
ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mwezi
Novemba, 2012 nilieleza kwa kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Lishe wa Mwaka 2011/2012 – 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua
ambazo Serikali inachukua kuondokana na tatizo
la Lishe Nchini. Jambo kubwa na la msingi katika kupambana na
tatizo la Lishe ni kutoa elimu kwa Jamii ili kula vyakula vyenye Virutubisho
muhimu hasa kwa Mama Wajawazito na Watoto Wachanga. Jitihada za Serikali za
kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika kutoa Elimu ya Lishe Nchini zimeleta
mwamko mzuri ambapo Wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wa Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu
katika utoaji elimu na kukuza kilimo cha mazao yenye virutubisho muhimu ili
kuongeza vyakula vyenye virutubisho.
31.
Mheshimiwa
Spika, katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la
Lishe Nchini, hivi karibuni Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa
Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha
kuongeza hamasa na kuzidisha chachu ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa
Nchini. Nimearifiwa kwamba, Kikundi hicho cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi
12 Januari, 2013 na kukubaliana kuhusu kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti
yao kwenye jamii juu ya umuhimu wa Lishe Bora.
Kikundi pia kimeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye
malengo ya kukuza uelewa wa Umma juu ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto.
Aidha, kikundi hicho kiliazimia kushawishi uwekaji wa vipaumbele vya Lishe
katika Mipango ya Maendeleo na Bajeti za Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa na kuingiza masuala ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto katika Sera na
Mikakati mbalimbali ya Serikali. Azimio lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi
za Bunge kuhusu Lishe, Chakula na Haki za Watoto.
32.
Mheshimiwa
Spika, napenda kuchukua fursa hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki
ambacho kimeona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na
tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki. Niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kusimamia
tatizo hilo ili kupata suluhu ya kudumu. Ninatambua pia umuhimu wa Waheshimiwa
Wabunge kuhamasisha masuala ya Lishe kwa Wananchi wa Majimbo yao. Niwaombe
Waheshimiwa Wabunge wengine wote kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa Wananchi
wa Majimbo yenu katika Mapambano dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja tujenge
Taifa lenye Watu walio na Lishe Bora. Lengo ni kuwawezesha kuchangia zaidi
katika uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa Nchi kwa ujumla.
MCHAKATO KUELEKEA KATIBA MPYA
33.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge
watakumbuka kuwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza kumaliza kazi ya
kukusanya maoni binafsi ya Wananchi mmoja mmoja kama mchango wao kwa ajili ya
kuandika Katiba Mpya. Aidha, imekamilisha kazi ya kukutana na Makundi Maalum,
Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Viongozi wa Kitaifa waliopo Madarakani. Kwa
maana hiyo, Tume sasa imekamilisha kazi ya ukusanyaji maoni kama ilivyopangwa.
Hivi sasa Tume inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na
Wananchi na yale yaliyotolewa na Makundi Maalum ili baadaye kutayarisha
Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa
katika Mabaraza ya Katiba
yatakayoitishwa na Tume Nchini kote.
34.
Kulingana
na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba itafanyika kuanzia mwezi Juni, 2013
na itajumuisha Wajumbe watakaochaguliwa na Wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya
Kijiji. Wajumbe hao ndio watapaswa kuwasilisha maoni ya Wananchi katika
Mikutano ya Mabaraza.
35.
Mheshimiwa Spika, nimearifiwa kuwa
Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa namna bora na ya Kidemokrasia ya kuwapata
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambao unaendelea kusambazwa Nchi nzima. Mwogozo
huo tayari umetangazwa katika Vyombo vya Habari ili Wananchi waufahamu na kutoa
maoni kuhusu namna ya kuuboresha.
36.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Rasimu
hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam,
kila Kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa kutoka miongoni
mwa Wakazi wa Vijiji vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani wa Kata
na Madiwani wa Viti Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa Dar
es Salaam, Tume imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana
na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum. Kwa msingi huo, kutakuwa na jumla ya Wajumbe 18,169 watakaohudhuria Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali
za Mitaa 13. Kila Shehia itawakilishwa
na Wajumbe watatu (3), ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti
Maalum na Madiwani wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo,
Wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198.
38.
Wananchi
wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watatakiwa kuwasilisha
majina yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa
upande wa Tanzania Zanzibar watawasilisha kwa Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo baadaye.
39.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito
kwa Viongozi wote katika ngazi za Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia
kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na Tume. Kwa kufanya hivyo, Wajumbe ambao
watashiriki katika Mabaraza ya Katiba watapatikana kwa njia
za Kidemokrasia na hivyo, kufanikisha
Vikao vya Mabaraza ya Katiba. Ni matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma
Mwongozo huo, na baadaye kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kwa Tume kabla ya
kazi ya uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza rasmi.
40.
Nitumie
fursa hii kuwaomba Wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni kuhusu
Mwongozo huo na pia katika kuwapata Wajumbe watakaoshiriki katika Mabaraza ya
Katiba kwa mujibu wa Sheria, na vilevile Wajumbe hao washiriki kikamilifu
katika Vikao vya Mabaraza ya Katiba na kutoa maoni kwenye Rasimu ya Katiba.
RIPOTI YA TATHMINI YA
UTAWALA BORA AFRIKA (APRM)
41.
Mheshimiwa
Spika, katika kuendeleza dhamira ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala
bora nchini kwa kuwashirikisha Wananchi, Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33
za Umoja wa Afrika zilizoamua kwa hiari yake kujiunga na Mpango wa Bara la
Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (The
African Peer Review Mechanism - APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato huo
mwaka 2004, na Bunge liliuridhia mwaka
2005.
42.
Mheshimiwa
Spika, Mpango huu wa kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi
Sera zetu na za Waasisi wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha,
unahusisha Viongozi wa Afrika na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya
Utawala Bora katika Nchi zao na kuainisha kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa
kuendelezwa na yale yenye changamoto za kufanyiwa kazi. Miongoni mwa sababu za
Nchi yetu kujiunga na Mpango huu ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania tuna
mengi ya kuifundisha Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora na sisi pia
kujifunza kutoka kwa wenzetu.
43.
Mheshimiwa Spika, ninayo furaha
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa baada ya zoezi la muda mrefu la kukusanya
maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu ambapo Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki
kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora, sasa hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu
katika Mchakato huo wa kujitathmini kiutawala bora.
44.
Tarehe
26 Januari 2013, Ripoti ya Hali ya Utawala Bora hapa nchini iliwasilishwa mbele
ya Wakuu wa Nchi za APRM Addis Ababa, Ethiopia ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wetu alipata fursa ya kuzungumzia mwelekeo wa Nchi yetu
katika kujenga Taifa imara zaidi katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
45.
Mheshimiwa Spika, katika Ripoti hiyo
ambayo itatumika kama rejea, zimeainishwa juhudi zetu kubwa za kulinda amani
Nchini. Pamoja na kuimarisha Utawala Bora wa Sheria na Haki za Binadamu. Aidha,
kupitia Ripoti hiyo, wenzetu katika masuala ya kuendesha Utawala Bora, Barani
Afrika na Duniani kwa ujumla wametambua jitihada zetu pamoja na mambo mengine
katika kuulinda Muungano, kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya
yote wamejua sura ya Tanzania katika ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao
Nchi yetu imepongezwa sana kwa juhudi zake.
46.
Ripoti hiyo pia imeainisha changamoto ambazo
wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa kuzifanyia kazi zaidi. Changamoto hizo ni
pamoja na suala la kushughulikia Kero za Muungano, kuimarisha zaidi juhudi za
kuondoa umaskini na kuilinda amani ya Nchi yetu hasa kutokana na chokochoko za
Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa sasa wa
Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka 50 ijayo.
47.
Mheshimiwa Spika, kuwasilishwa kwa
Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa Nchi wa Mpango huu ndio mwanzo sasa wa
Serikali yetu ya kuimarisha maeneo yaliyoonekana kuwa tunafanya vyema. Pia
hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza kutekeleza Mpangokazi wa Miaka Mitano ambao
umeainisha namna gani ya kuyafanyia kazi maeneo ambayo wananchi waliyaona kuwa
yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Suala hili liliwekewa msisitizo na Mheshimiwa
Rais katika Hotuba yake ya Mwisho wa Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.
48.
Mheshimiwa Spika, kutokana na manufaa
ya APRM kama daraja kati ya Serikali na Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja,
Serikali itaendelea kuiimarisha Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa
kitovu chetu cha fikra (think tank)
katika kushauri kuhusu masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha
Taasisi hii kuendelea kuwa kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika
kutathmini na kutupatia mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.
49.
Aidha,
Serikali itaendelea kufadhili shughuli za APRM, kuiimarisha Taasisi kwa
raslimali watu na fedha kwa ajili ya kazi pana zaidi za kutoa ushauri,
kuunganisha Wadau mbalimbali na kuendelea kuratibu tathmini nyingine katika
siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi ya kujikosoa ili kujisahihisha. Napenda
kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakishirikiana
na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo
imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.
UANZISHAJI WA MAENEO
MAPYA YA UTAWALA
i)
Uanzishaji wa Mikoa
na Wilaya
50.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge
watakumbuka kuwa, mwezi Machi 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuanzisha Mikoa
Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali
sasa imekamilisha mchakato wa kuanzisha maeneo hayo Mapya ya Utawala, kwa
kuanzisha Mikoa Minne ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi. Aidha, imekamilisha
uanzishwaji wa Wilaya 19 za Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi,
Itilima, Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele, Momba,
Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo tayari
zimeshaanza kufanya kazi na kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi. Vilevile, Mheshimiwa
Rais alishafanya Uteuzi wa Viongozi Wakuu wa Mikoa na Wilaya Mpya. Serikali
imeendelea kupeleka Watumishi na kuanza kujenga miundombinu muhimu katika
maeneo husika. Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuanzisha
maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi, ikiwemo kupata Watumishi wa kutosha
ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.
ii)
Uanzishaji wa
Halmashauri
51.
Mheshimiwa Spika, ili kupeleka huduma karibu
zaidi kwa Wananchi, Serikali pia iliazimia kuanzisha Halmashauri Mpya 37.
Uanzishaji wa Halmashauri hizo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali kwa
kuzingatia makundi yafuatayo:
Kundi
la Kwanza,
linahusu Halmashauri Mpya 8 za Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri
Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato wa uanzishaji wake tayari umekamilika
Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Jiji
la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Halmashauri
ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya
Busokelo. Halmashauri hizo tayari
zimepata Hati na kupangiwa Wakurugenzi.
Kundi la Pili, linajumuisha
Halmashauri Kumi (10) ambazo mchakato wa kuzianzisha umekamilika na tayari
zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri
hizo ni Kalambo, Nsimbo, Mlele, Bumbuli, Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba
na Kyerwa. Halmashauri hizo kwa sasa zinaandaliwa Hati ili zianze.
Kundi
la Tatu,
ni Halmashauri za Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato wa uhakiki wake umekamilika
na Amri za Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati wowote zitatangazwa katika
Gazeti la Serikali. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Wilaya za Buhigwe,
Kaliua, Nyang’hwale, Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko.
Aidha, zipo Halmashauri nyingine Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake
zinakamilishwa na hatimaye zitasainiwa hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama,
Tarime, Uvinza na Ikungi.
Kundi
la Nne,
linajumuisha Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa uanzishaji wake umekamilika
isipokuwa taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu baadhi ya Kata katika
Halmashauri hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani. Halmashauri hizo Nne (4) ni za
Miji ya Kasulu, Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani,
katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuna Kata 14, na kati ya hizo, Kata 6 ni
mpya na hazina Madiwani. Kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Handeni
ina jumla ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina
Madiwani. Aidha, Halmashauri ya Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina
Madiwani na Halmashauri ya Mji wa Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni
mpya na hazina Madiwani.
52.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha
maeneo hayo mapya ni kuwawezesha Wananchi kupata huduma karibu zaidi kwa
Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Watendaji wote kuwaongoza
Wananchi kutumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa maeneo hayo katika kujiletea
maendeleo. Serikali itaendelea kupeleka huduma zaidi karibu na Wananchi ili
kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo. Aidha, Serikali itaweka
utaratibu wa kuzipatia Halmashauri zinazoanzishwa Watumishi hatua kwa hatua.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI DHIDI YA WATANZANIA
WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI
53.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba,
2012, Bunge lilipitisha Azimio Na. 9/2012 kuhusu kuitaka Serikali kuchukua
hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja
Binafsi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb). Azimio hilo linahitaji,
pamoja na mambo mengine, Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo
cha Asset Recovery Unit ili mabilioni
yanayomilikiwa na Watanzania katika Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa
kukwepa kulipa kodi yarudishwe na kwamba Watanzania wote wenye akaunti za fedha
nje ya Nchi waeleze wamezipataje ili TAKUKURU wachukue hatua za Kisheria dhidi
ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali. Aidha,
iliazimiwa na Bunge na Serikali ikakubali kwamba, katika Mkutano wa Bunge wa 11
italeta Taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa
fedha nje ya Nchi.
54.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Desemba,
2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kitaifa
kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania
walioficha fedha haramu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe wanane
wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu; Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Jeshi la Polisi; Benki Kuu ya Tanzania; Usalama
wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kazi za Kamati hiyo ni:
(i)
Kuchunguza
na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya Nchi kinyume na
Sheria na Kanuni za Nchi;
(ii)
Kuchunguza
iwapo fedha hizo ni haramu au la;
(iii)
Kutambua
Mabenki na Nchi zilizofichwa fedha hizo;
(iv)
Kuandaa
mashtaka dhidi ya Watanzania watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya Nchi;
na
(v)
Kuishauri
Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.
55.
Mheshimiwa Spika, Kamati hii imeanza
kazi zake rasmi tarehe 9 Januari 2013 kwa kupanga namna ya kutekeleza kazi zake
ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha haramu
nje ya Nchi na kuangalia namna ya kupata taarifa muhimu nje ya Nchi. Kamati
hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
56.
Ili
kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi ni wazi kwamba itahitaji
kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi kwa kutoa taarifa mbalimbali
kuhusu suala hili. Hivyo, natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa sahihi na
za ukweli zinazoweza kuisadia Kamati kutekeleza kazi hii wanahimizwa wajitokeze
kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana
kwa karibu na Kamati iliyoundwa na Serikali. Aidha, nawaomba Waheshimiwa
Wabunge nao kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati hii.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda
niwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee nikushukuru
wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu.
Nimshukuru vilevile, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Vikao vya
Bunge kwa ufanisi. Aidha, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu.
Nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake kwa huduma nzuri walizozitoa
wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru Watendaji wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa kutekeleza
majukumu yao vizuri ili kufanikisha shughuli za Bunge zilizopangwa. Niwashukuru
Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kutufikishia habari kwa Wananchi yale
yaliyojiri hapa Bungeni na kwa wakati. Vilevile, navishukuru Vyombo vya Ulinzi
na Usalama kwa kazi yao nzuri na Madereva wote kwa huduma zao kwa Washiriki wa
Bunge hili.
58.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo,
naomba niwatakie Safari Njema na sasa natoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 9
Aprili, 2013 Saa 3:00 Asubuhi kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
59.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment