WATUHUMIWA wa ujangili waliokamatwa hivi karibuni katika Operesheni Tokomeza Ujangili mkoani Kilimanjaro, jana walifikishwa mahakamani mjini hapa akiwamo Mohamed Hatiki, aliyekutwa na rundo la bunduki na risasi.

Hatiki anadaiwa kumiliki bunduki sita bila leseni, ambazo ni shotgun namba TZCAR86629, pistol glock namba RUW605, pistol revolver namba TZCAR 59644, rifle 375 namba TZCAR93195, rifle 280 namba TZCAR88522 na rifle 22 namba TZCAR37022.

Hatiki (26), mkazi wa Kata ya Bondeni, Manispaa ya Moshi na Mohamed Sadiq wa Pasua walifikishwa juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sophia Massati, huku Sadiq akizirai akiwa kizimbani baada ya kupata mshituko.

Hatiki, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza anakabiliwa na makosa 15 yanayoangukia chini ya sheria ya uhifadhi na uhujumu uchumi huku katika shitaka la kwanza akidaiwa kupatikana na nyara za serikali ambazo ni kwato mbili za kongoni zenye thamani ya sh milioni 1.04.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Omari Kibwana, akisaidiana na mwendesha mashitaka kutoka Maliasili, Rusticus Mahundi, mshitakiwa huyo anadaiwa kupatikana na nyara hizo Oktoba 23, mwaka huu, alfajiri katika Kata ya Bondeni.

Shitaka la pili hadi la saba, mshitakiwa anadaiwa kumiliki bunduki sita zilizotajwa hapo juu bila kuwa na leseni halali.

Shitaka la nane, Hatiki anadaiwa kupatikana na risasi 23 za bunduki aina ya shotgun na katika shitaka la tisa anadaiwa kupatikana na risasi saba za bunduki aina ya pistol glock yenye namba za usajili RUW605 bila leseni.

Katika shitaka la kumi, Hatiki anadaiwa kupatikana na risasi 56 za bunduki aina ya pistol revolver bila leseni, wakati shitaka la 11 ni kupatikana na risasi nne za bunduki aina ya rifle 375 bila leseni.

Mshitakiwa huyo ambaye yupo nje kwa dhamana, anashitakiwa pia kwa kosa la kukutwa na maganda ya risasi ya bunduki aina ya rifle 375, risasi 15 za bunduki aina ya rifle 280, maganda 10 ya bunduki aina ya rifle 280, na risasi 84 za bunduki aina ya rifle 22.

Naye mshitakiwa wa pili, Sadiq (67), anakabiliwa na makosa tisa, likiwamo kumiliki silaha na risasi bila leseni, pamoja na kukutwa na fuvu la nyati na mfupa wa tembo wenye thamani ya sh milioni 24.1 na tumbili hai mmoja Oktoba 22, mwaka huu, eneo la Pasua.

Silaha hizo ni rifle namba TZCAR 82048, rifle MK4, rifle 22, risasi nne za silaha aina ya shotgun, 12 za bunduki aina ya rifle 303 na 11 za bunduki aina ya rifle 22.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na watu wawili, mmoja aweke dhamana ya fedha taslimu sh milioni 14, hivyo kurejeshwa rumande hadi Novemba 6, mwaka huu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top