HOTUBA YA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI
WA KUWEKA JIWE LA MSINGI KUZINDUA UJENZI WA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU
ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA, ENEO LA KIBADA, DAR ES SALAAM, 13
DESEMBA, 2012
Mheshimiwa
Goodluck ole Medeye, Naibu Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;
Mheshimiwa,
Said Meck Sadick, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam;
Ndugu
Kesogukewele Masudi Issa Msita, Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la
Nyumba la Taifa;
Ndugu
Nehemia Kyando Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Nyumba la Taifa;
Menejimenti
na Watumishi wa NHC Mliopo Hapa;
Wageni
Waalikwa,
Mabibi
na Mabwana:
Namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Anna
Tibaijuka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ndugu Kesogukewele
Msita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba na Ndugu Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa
NHC na uongozi wote wa Shirika kwa kunialika kuja kushiriki katika tukio hili
la kihistoria la kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu
zinazojengwa na Shirika hapa Kibada.
Nawapongeza Bodi na Menejimenti ya Shirika
kwa kubuni wazo hili zuri na kulitekeleza.
Mmefanya uamuzi wa busara wa kujenga nyumba hizi kwa ajili ya watu wenye
kipato cha kawaida. Uamuzi huu wa
kizalendo unatoa taswira nzuri ya Shirika kwa jamii na kujenga imani miongoni
mwa watu kuwa Shirika hili ni lao na lipo kwa ajili yao. Shirika sasa linajali hata maslahi ya watu wenye
kipato cha chini na cha kati. Hii ndiyo
ilikuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba mara baada ya Uhuru. Hili mnalofanya leo ndilo hasa jukumu lenu la
msingi. Hongereni sana na naomba
muendelee kufanya kazi hii mliyoianza.
Ndugu
Wananchi;
Wananchi kuwa na nyumba bora za kuishi
ni moja ya malengo makuu ya Serikali tangu uhuru wa nchi yetu miaka 51
iliyopita mpaka sasa. Ni hivyo, kwa
sababu kuwa na nyumba ni mahitaji ya msingi ya mwanadamu. Lakini pia Serikali ililazimika kusisitiza
kuwa na nyumba bora kwa sababu wananchi wengi walikuwa wanaishi katika nyumba
za makuti. Hivyo basi Shirika
lilianzishwa kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kuondoka kwenye nyumba za
makuti na kuwa na nyumba bora. Ndiyo
siri ya kujengwa na kuwepo kwa nyumba nyingi za
“neshnali” Magomeni, Kinondoni, Mwananyamala, Ilala, Temeke, Mburahati,
Buguruni na Keko kwa hapa Dar es Salaam na kwingineko nchini.
Nyumba hizo nzuri na imara zilijengwa
na kuuzwa kwa gharama nafuu na watu wengi wenye kipato cha kawaida waliweza
kumudu kuzinunua. Mpaka leo nyumba hizo zipo, tena bado imara kabisa licha ya
kuwa na umri unakaribia miaka 50.
Kwa bahati mbaya kasi ya Shirika ya
kujenga nyumba mpya za namna hiyo ilipungua hasa kuanzia miaka ya themanini kutokana
na uhusiano wa nchi yetu na Ujerumani kutetereka na uchumi wa nchi kupata
misukosuko kuanzia miaka ya 1970. Na
baada ya nyumba za Msajili kukabidhiwa NHC, Shirika likasahau ujenzi wa nyumba. Shirika likabaki na kazi ya kukusanya kodi ya
pango kwenye nyumba ilizojenga na zile zilizokuwa za Msajili. Kadri muda ulivyokuwa unakwenda Shirika
likasahau kabisa wajibu wake wa kujenga nyumba.
Lakini, si hivyo tu, hata makusanyo ya kodi pia yakaanza kudorora na uwezo wa kujiendesha
wa Shirika ukapungua sana.
Hali hiyo, imekuwa mtihani mkubwa kwa
Serikali kuhusu haja ya kulirejesha Shirika katika hali nzuri. Baadae Shirika likazinduka na kuanza tena
ujenzi wa nyumba, lakini nyumba zake ni ghali sana ambazo watu wa kipato cha
kawaida hawazimudu. Kwa kweli Watanzania
wengi walioajiriwa hawazimudu hata wale wa vyeo vya juu, kwa vile mishahara yao
bado si mikubwa. Bahati mbaya pia hapakuwepo
na utaratibu wa mikopo ya nyumba baada ya kufa kwa Tanzania Housing Bank (THB)
na mpango wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa umma.
Ndugu
wananchi;
Kufuatia hali hiyo Serikali ikaamua kuchukua
hatua za makusudi kuboresha Shirika na kuhuisha Sera na Sheria zinazohusu
uendelezaji wa sekta ya nyumba ili ziendane na hali halisi ya wakati huu. Miongoni
mwa hatua hizo ni kupata Bodi mpya na Mkurugenzi mpya. Pia, kutungwa kwanza kwa Sheria ihusuyo
mikopo ya nyumba ili watu waweze kupata mikopo ya kujenga au kununua
nyumba. Pili ni kutungwa kwa Sheria ya
kuwezesha watu kuuziwa nyumba mojawapo katika ghorofa lenye nyumba nyingi na
kupewa hati ya kumiliki nyumba hiyo.
Utekelezaji wake umeanza, unaendelea ingawaje sijaridhika sana na kasi
ya utekelezaji wa Sheria hizi mbili.
Pamoja na hayo, ujenzi wa nyumba
unaendelea kwa kasi kubwa kote nchini kama tunavyoona wote. Hata hivyo, nyumba hizo ni ghali, watu wenye
vipato vya chini na wafanyakazi si rahisi kumudu. Wengine hushawishika kufanya mambo
yasiyostahili.
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Shirika
la Nyumba la Taifa kwa uamuzi wake wa kujenga nyumba za gharama nafuu. Mmerejea kwenye madhumuni ya awali ya kuwepo
kwenu. Sasa Shirika la Nyumba linafanya
yale ambayo ilitumwa kufanya tangu kuasisiwa kwake.
Nimesikia kilio chenu kuhusu kodi ya
ongezeko la thamani; bei za viwanja n.k.
Wahusika wataambiwa. Pia,
angalieni uwezekano wa kuwakopesha wafanyakazi kwa masharti ya kudhaminiwa na
waajiri wao kuwalipa moja kwa moja.
Nashauri NHC nayo iangalie uwezekano
wa kushiriki katika kuanzisha benki ya nyyumba au kuwa na hisa katika benki
zilizopo. Kukiwa na utaratibu wa mikopo
hususan yenye riba nafuu, wateja wa kununua nyumba watakuwa wengi na Shirika
litanufaika. Mtajenga nyumba za gharama
nafuu na wanunuzi watakuwapo.
Nawapongeza sana viongozi na watumishi
wa Shirika kwa kazi nzuri muifanyao.
Shirika limebadilika na mafanikio yanaonekana. Mmedhihirisha kwa vitendo kuwa mashirika ya
umma yanaweza kufanya mambo mazuri.
Endeleeni na moyo huo tupate mafanikio zaidi. Kinachotakiwa ni uongozi mzuri.
Mheshimiwa
Naibu Waziri;
Ili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu
nchini uweze kuwa endelevu ni lazima Serikali iweke mazingira mazuri ya kisera
na kisheria. Inatupasa tuangalie namna ya kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba: kwa upande wa vifaa vya ujenzi kuwa vya
gharama nafuu, gharama za viwanja, riba za mikopo, na kodi mbalimbali. Wizara ishirikiane na Wizara ya Fedha na
Benki Kuu na taasisi za fedha ili kuangalia uwezekano wa kupunguza riba
anayotozwa mnunuzi aliyechukua mkopo benki. Riba ya asilimia 18 ni kubwa mno. Tafadhali
kaeni na taasisi zinazohusika mjadiliane ili kufanikisha utekelezaji wa sera
yetu ya kujenga nyumba za gharama nafuu. Ni lazima tuendelee na utaratibu huu
bila vikwazo ili watu wengi wanufaike. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanahusu
pia watu kuwa na nyumba bora za kuishi.
Vilevile ningependa Wizara yako ihakikishe
kuwa Halmashauri zote nchini zinaharakisha
kasi ya upimaji wa viwanja na kuviwekea huduma husika na kuviuza kwa bei
nafuu. Halmashauri zisigeuze bei za
viwanja chanzo cha kutafuta mapato na kumaliza shida zake. Itakuwa vigumu kwa Shirika la Nyumba kujenga
nyumba za gharama nafuu kama Halmashauri zetu zitaendelea kuliuzia ardhi
Shirika kwa bei kubwa. Mbona Halmashauri za Geita, Mvomero, Makete, Kongwa na
Mkinga zimeweza kulipatia Shirika ardhi
bila gharama yoyote. Iweje nyingine zishindwe kufanya hivyo? Halmashauri
ikiliuzia Shirika viwanja kwa bei kubwa, gharama za nyumba zinakuwa kubwa na
kupoteza dhana nzima ya unafuu.
Aidha, Wizara inalo jukumu la
kuhakikisha kuwa maeneo mapya yanayopimwa yanakuwa na huduma zote muhimu kama
vile umeme, maji, barabara na mawasiliano ya simu. Huu ni utaratibu wa msingi ambao hautekelezwi
ipasavyo. Naomba tuangalia namna ya
kuurejea utaratibu huu kwani utapunguza kero zisizokuwa za lazima.
Pia naomba Shirika la Nyumba liandae
mpango wa ujenzi wa nchi nzima na kisha kuwasilisha mpango huo Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi mapema iwezekanavyo. Hali hii itawezesha Wizara na taasisi zinazotoa
huduma kuweka mipango yao kulingana na kazi zilizo mbele yao. Mimi nina imani kuwa Shirika la Nyumba likipewa
ushirikiano mzuri, gharama ya nyumba inazojenga itapungua zaidi.
Ndugu
wananchi;
Napenda kuwaahidi kuwa Serikali yenu
itaendelea kuboresha sheria na sera mbalimbali ili mazingira ya kuwekeza kwenye
nyumba yaweze kuwa mazuri zaidi. Aidha,
tutaendelea kuchukua hatua zitakazowezesha vyombo vya fedha kupunguza riba ya
mikopo wanayotoa. Pia, Serikali
inasubiri mapendekezo ya Kamati niliyoiunda Dodoma kuangalia namna ya kuwezesha
ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini. Naomba makampuni binafsi nayo
yajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi zetu. Sisi tupo tayari kushirikiana
nao. Mahitaji ni mengi, Shirika la Nyumba haliwezi kukidhi kiu ya soko la
nyumba za gharama nafuu peke yake.
Mheshimiwa Naibu Waziri;
Naomba
nimalizie kwa kuwashukuru nyote mlioshiriki katika tukio hili la kihistoria la
uwekaji wa jiwe la msingi katika nyumba za gharama nafuu hapa Kibada. Naona sasa ndoto yangu ya kuwa na nyumba za
gharama nafuu nchini inaanza kutimia. Endeleeni kusimamia kwa bidii ujenzi wa
nyumba hizi. Nyumba huleta amani ya nchi, hivyo tuendelee kutimiza wajibu wetu
kwa kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanamudu kuwa na makazi bora.
Baada
ya kusema hayo sasa napenda kutamka rasmi kuwa niko tayari kuweka jiwe la
msingi la nyumba za gharama nafuu hapa Kibada, ikiwa ni ishara ya kuzindua
miradi mingine ya aina hii inayotekelezwa na Shirika katika maeneo mbalimbali
nchini. Wananchi watumie fursa hii vizuri. Nyumba zipo zinaendelea kujengwa
nchi nzima.
Asanteni
kwa kunisikiliza!
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment