Itakumbukwa kwamba tarehe 19 Februari 2014 Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum Pandu Kificho aliteua Kamati ya Wajumbe ishirini yenye uwakilishi wa makundi yote yanayounda Bunge Maalum kwa ajili ya kumshauri kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.

Rasimu ya kwanza ya Bunge Maalum iliandaliwa na Kamati ya Maandalizi chini ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (nakala yake niliwapa hapa: http://goo.gl/hEI4aw ).

Kazi ya mjumbe ni kuwakilisha na kuwasilisha; katika kutekeleza wajibu huo, jana 26 Februari 2014 tulikuwa na Semina ya Bunge Maalum kuhusu Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum toleo la 2014. 

Katika mjadala wa jana niliunga mkono mapendekezo ya rasimu katika sehemu ya nne kuhusu kupunguzwa kwa mamlaka na madaraka makubwa ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, tofauti na rasimu ya kwanza; sasa maamuzi ya mwenyekiti hayatakuwa ya mwisho. Mjumbe asiporidhika anaweza kukata rufaa na pia rasimu sasa inapendekeza kwamba mwenyekiti au makamu wanaweza kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani.

Niliunga mkono kuruhusiwa kwa utaratibu wa kuwasilisha Taarifa ya Maoni Kinzani (dissenting opinion); hii ni kwa sababu rasimu ya kwanza haikuwa na utaratibu wa uwasilishaji bungeni wa hoja za wabunge, hoja zote ilikuwa ni kamati. Njia pekee ya kuwezesha mawazo mbadala kuweza kufika katika ukumbi wa Bunge kwa ukamilifu ukiondoa michango ya wabunge ni kupitia Taarifa za Maoni Kinzani.


Utaratibu huu utawezesha pia kufanya wajumbe walio wengi wenye msimamo unaofafanana kuepusha uwepo wa maoni kinzani kwa kujadiliana na kuridhiana na wachache wenye maoni ya msingi bila kujali idadi yao na hivyo kujenga muafaka wa kitaifa. Taarifa ya Maoni Kinzani isiporuhusiwa upigaji kura utatumika kwa haraka kupitisha msimamo wa wengi bila kutafakari kwa kina mtizamo wa wachache ndani ya kamati ambao wakati mwingine unaweza kuwa unawasilisha maoni ya wananchi wengi nje ya Bunge.

Nimeunga mkono utaratibu wa kura ya siri kutumika kupitisha hoja za kamati na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara na hatimaye kupitisha rasimu ya mwisho ya katiba. Mtizamo wangu wa awali ulikuwa ni kura kuwa ya wazi kwa kuzingatia kwamba wajumbe ni wawakilishi. Hivyo, ni muhimu wanaowawakilisha wakafahamu wawakilishi wao wamesimamia upande gani na pia kuwezesha kila mjumbe kuwajibika kutokana na kura yake. Aidha, kura ya wazi inaweza kudhibiti wajumbe dhidi ya ushawishi usio sawa (undue influence) ikiwemo unaowezesha kuhusisha ufisadi kwa kuwa mjumbe atajulikana wazi iwapo atakwenda kinyume cha maoni ya wananchi kwenye masuala ya msingi kwa sababu ya ushawishi huo.

Kwa kuzingatia mtizamo huo, nilipendekeza kwa wenzangu kwamba kura ziwe za mchanyato/mchanganyiko; katika hatua ya kwanza ya kura kupigwa wakati wa kupitisha ibara moja moja ya katiba, kura ya siri itumike. Ili wajumbe wawe huru katika hatua hiyo kupigia kura ibara kwa ibara kwa kadiri ya ripoti za kamati na majadiliano. Lakini kura ya mwisho, baada ya kuwa ibara zote zimekubaliwa; ya kupitisha katiba kwa ujumla wake basi kura iwe ni ya wazi ya kuitwa jina mjumbe mmoja mmoja kama ambavyo Bunge hufanya wakati wa kupitisha bajeti.

Hata hivyo, baada ya kupata Waraka na. 3 wa Siri wa CCM kuhusu Rasimu ya Katiba wa Februari 2014 ambapo pamoja na mambo mengine ni wa ‘kujipanga vizuri katika hatua zinazofuata za mchakato wa kuunda katiba mpya’ ikiwemo katika Bunge Maalum na kusikiliza michango ya baadhi ya wajumbe jana niliona wazi kwamba watetezi wa kura ya siri wana ajenda ya siri nyuma yao. 

Katika mazingira hayo, ili kuwezesha uhuru wa wajumbe katika uamuzi kwa kuzingatia maoni ya wananchi na majadiliano yatayofanyika bungeni kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa katika mchakato wa katiba nimeamua kwa nia njema kuwa mtetezi wa kura ya siri kutumika katika Bunge Maalum.

Kila mjumbe awezeshwe kuwajibika kwa nchi yake, nafsi yake na Mungu wake kwa kuzingatia maoni ya nchi na maslahi ya taifa badala ya kupiga kura kwa kuhofia msimamo wa chama, taasisi au kundi analoliwakilisha katika Bunge Maalum.
Nilieleza wazi kwamba wanaopendekeza kuwa ibara za rasimu ya katiba zipitishwe kwa wingi wa kawaida (simple majority) na kwamba wingi wa theluthi mbili utumike wakati wa kuamua kuhusu rasimu ya mwisho pekee wanataka Bunge Maalum lipitishe kanuni inayokwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo kimsingi itakuwa batili.

Nilieleza kwamba watetezi wa hoja hii wanasoma sheria toleo la Kiswahili pekee ambalo lina makosa; kifungu cha 26 (2) kinasema “Ili katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa” wakati ambapo ya Kiingereza inasema “The provisions of the proposed constitution shall require passing by”; kwa maana ya kwamba inazungumzia vifungu. Aidha, pamoja na kuwa Sheria hiyo hiyo toleo la Kiswahili 32 (4) inasema matoleo ya Kiingereza na Kiswahili “yote ni sahihi” , toleo la Kiingereza limesema “are authentic”; kwa maana ya kuwa ni halisi. 

Mgongano huo baina ya sheria mbili unapatiwa ufumbuzi kwa kurejea sheria zingine na maamuzi ya mahakama ambapo inaonyesha kwamba kunapotokea mgogoro baina ya matoleo ya lugha zingine za sheria ile ya Kiingereza inatamalaki. Hivyo, kwa kuwa sheria hizo zinazotukuza Kiingereza bado hazijabadilishwa, sheria inayopaswa kuongoza Kanuni ni ya Kiingereza ambayo imeweka bayana kwamba vifungu vitapitishwa kwa kura ya wingi wa mbili ya tatu.

Napendekeza kwamba masuala haya manne ambayo kuna mwelekeo kwamba kuna watu wamekutana juzi, kabla ya mjadala wa jana kupanga kwamba maoni ya kamati yasikubaliwe yanapaswa kuungwa mkono na wajumbe na wananchi nje ya Bunge. 

Pamoja na kuunga mkono masuala hayo, yapo marekebisho ambayo nimependekeza kwa maandishi yafanyike na mengine nitaendelea kuyapendekeza leo na kesho. Katika muktadha huo, naiweka hapa nakala ya Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum ili nawe ushiriki kutoa maoni na kushawishi wajumbe unaoweza kuwafikia ili kwa pamoja tuhakikishe zinatungwa bora zitazowezesha Bunge Maalum kuendeshwa kwa ufanisi katika kuiboresha rasimu na kuifanyia mabadiliko mazuri kwa kuzingatia maoni ya wananchi na maslahi ya nchi.

Wenu katika uwakilishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

27/02/2014
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top