komoro1 cdc7c
YANGA imesonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 na sasa inajiandaa kuikabili Al-Ahly ya Misri. 

Hiyo ni baada ya ushindi wa mabao 7-0 katika mechi ya awali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ushindi mwingine wa mabao 5-2 katika mechi ya marudiano ambayo Yanga ilikuwa ugenini nchini Comoro.

Mambo 10 yafuatayo yanaweza kukupa mwangaza halisi wa jinsi nchi hiyo ilivyo:

1. Hii ni nchi ya Kiislamu yenye idadi ya watu wanaokadiriwa kufika 800,000 na inafuata misingi ya dini ya Kiislamu, kutokana na hilo, Comoro kuna misikiti mingi kila baada ya nyumba 15 hadi 20 msikiti lakini kuna kanisa moja tu kwa ajili ya wageni.

2. Fedha yao ina thamani kuliko Shilingi ya Tanzania kwani Faranga
500 ya Comoro ni zaidi ya Sh2000 ya Tanzania. Hata hivyo wanapenda zaidi kutumia Dola ya Marekani na Euro hata kwa matumizi yao ya kawaida.

3.Usafiri wao mkubwa ni taxi japokuwa daladala zipo chache sana ambazo ni mabasi madogo, lakini taxi na daladala zinatumia nauli moja. Usafiri kutoka Moroni hadi Ntsaweni ni Faranga 500 lakini ukitaka kwenda Mitsamiouli walipocheza Yanga utalipa Faranga 750, kwa usafiri wa ndani ya mji utalipa Faranga 250 tu. Taxi inakufikisha hadi nyumbani na hakuna abiria anayelalamika kuhusu hilo.

4.Pombe ni kitu haramu kwao, kama unataka kunywa pombe unakunywa kwa kificho ndani ya nyumba yako. Zinauzwa jijini Moroni pekee katika baa ambazo ni chache. Ni marufuku kunywa pombe hadharani. Watu kutoka miji mingine hulazimika kusafiri hadi Moroni kufuata pombe. Kwa wale watumiaji wa pombe za kienyeji hasa kwa maeneo ya vijijini, mnazi ndiyo pombe yao kubwa.

5.Chakula kikubwa Comoro ni mikate, tambi, samaki, wali upo lakini ugali hakuna. Ndizi ni nyingi na mihogo, pia vipapatio vya kuku huliwa sana.

6.Vijana wanavuta sana bangi katika maeneo ya katikati ya jiji na vijijini lakini si wahalifu, unaweza kupoteza fedha na simu na ukarudishiwa simu lakini fedha zako watakufikiria. Hawana hulka ya kukaba au kuvunja nyumba.

7.Starehe zote za disco na muziki mwingine zote zipo Moroni tu tena Ijumaa na Jumamosi kwa sehemu chache. Usafiri wa uhakika mwisho saa 3 usiku, zaidi ya hapo ukichukua taxi unapaswa kulipia viti vyote vinne vya abiria, tena kwenda na kurudi.

8.Wanatumia magari ya Renault, Peugeot, Scenic japokuwa Toyota zipo lakini ni chache. Gari zote zinaendeshwa kushoto 'left hand' hivyo dereva wa Dar es Salaam akienda Comoro atapata tabu siku ya kwanza. Madereva wao wanatii sheria, hakuna kutanua ovyo kama Bongo.

9. Soko Kuu la Moroni linaitwa Volovolo, hapo ni kama Kariakoo kuna wachuuzi wa biashara mbalimbali kuanzia nguo, vyakula hadi muda wa hewani. Mateja ndiyo wanaouza muda wa hewani, utawaona wanakufuata wanakuonyesha simu, siyo kwamba wanauza simu wao huuza muda wa hewani wanaitwa Taxi Phone.

10.Biashara ya kuuza miili ipo Moroni tu, tena kwa kificho na ingawa kondomu zinauzwa Moroni kwa uwazi lakini miji mingine ni aghalabu kukuta zinauzwa hadharani. 
Chanzo: Mwanaspoti
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top