Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameapa
kuendelea kudai mfumo wa Muungano wa serikali tatu nje ya Bunge la
Katiba kwa nguvu zote, ikiwamo kufanya maandamano ya amani nchi nzima.
Msimamo huo ulielezwa na viongozi hao kwa nyakati
tofauti katika mkutano wa hadhara uliofurika mashabiki kwenye Viwanja
vya Kibandamaiti, Unguja jana.
Mwenyekiti Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua
kuliacha Bunge la Katiba kutokana na harufu za rushwa, vitisho na matusi
huku baadhi ya wabunge wakiahidiwa vyeo. Mbowe ambaye hata hivyo
hakufafanua zaidi, alisema Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza
dhamira chafu walionayo wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa
Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph
Warioba.
“Ni jambo la hatari katika mchakato wa Katiba
wananchi kuwa waoga au wenye hofu... Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala
kuwa tuna umoja imara, tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na
Zanzibar, Rais Kikwete (Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi
kuchukua madaraka,” alisema Mbowe.
Lipumba anena
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema wajumbe wa Ukawa wameamua kujitoa bungeni kutokana na
kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambayo alidai kuwa iliibeza na
kuidhalilisha Tume ya Warioba.
Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.
Alidai kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua
kutetea sera za chama chake na kupingana na maoni yaliyotolewa na
wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Rais Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba
Mpya, amekuwa akijulishwa kila hatua na jinsi maoni ya wananchi
walivyokuwa wakipendekeza serikali tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya
Pili naye akawa anaafiki, inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya
wengi,” alisema Profesa Lipumba.
Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila
alisema aliwahi kufungwa jela mara tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa
kudai lipatikane Taifa la Tanganyika huku watawala wakikataa matakwa ya
wengi kwa sababu na hoja dhaifu.
Mchungaji Mtikila aliongeza kusema kwamba
wanachokitaka CCM na Serikali zake ni kuendelea kuwabana wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar wasiweze kuwa huru na kujivunia mataifa yao.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Seif: Mimi Ukawa damu
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif Shariff Hamad alieleza msimamo wake kuwa anaunga mkono harakati
hizo na yeye ni Ukawa damudamu.
“Walikuwa hawajui msimamo wangu, waelewe kwamba mimi ni Ukawa damu,” alisema.
Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, alisema wanaotetea mfumo wa serikali mbili ni sawa na watu
wanaopigania kuendelea kuwapo kwa dhuluma Tanzania.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo huu, tumekuwa
tukipiga kelele kwamba Muungano huu wa serikali mbili umeteka mamlaka
yetu,” alisema Maalim Seif. Alimtaka Rais Kikwete asiwatishe wananchi
kwa sababu wamependekeza mfumo mpya wa serikali... “Unaposema kwamba
jeshi litapindua nchi kama tukiwa na Muungano wa serikali tatu,
unamaanisha nini kama Amiri Jeshi Mkuu?” alihoji Maalim.
Katika mkutano huo, ulinzi uliimarishwa vya
kutosha huku magari ya FFU na vikosi vya SMZ yakiwa yameegeshwa pembeni
na askari waliokuwa wamebeba silaha na mabomu viunoni wakilinda.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment