Latest News

*OCD asema hali ni mbaya, DC asema hali ni tulivu
WATU watano wanadaiwa kufariki dunia wakati wa mapigano makali kati ya wafugaji na wakulima yanayoendelea wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara. Pia, watu zaidi ya kumi wameripotiwa kujeruhiwa wakati wa mapigano mengine yaliyotokea juzi, baada ya mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wakulima na Wafugaji kuvunjwa na Jeshi la Polisi, Wilaya ya Kiteto.

Wakulima na wafugaji hao, wanagombea eneo la Hifadhi ya Embloi Murtangosi.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wananchi wilayani humo zinasema kuwa, kabla ya mapigano ya juzi, wakulima na wafugaji walikutana ili kujadili mvutano baina yao.

Wakati wakiendelea na mkutano huo, taarifa zinasema Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kiteto, aliyefahamika kwa jina la Foka Dinya, aliagiza mkutano huo uvunjwe baada ya kuwepo dalili za kutoweka kwa amani.

Pamoja na kutoa agizo hilo, taarifa zinasema wakulima na wafugaji hao waligoma kutawanyika na hivyo akalazimika kuomba msaada wa Kikosi cha Askari wa Kutuliza Ghasia ambao walifika na kurusha mabomu ya machozi wakati wakiwatawanya watu hao.

Mmoja wa wakulima hao, Ramadhan Machaku, aliwaambia waandishi wa habari waliofika wilayani humo kufuatilia mapigano hayo, kwamba wafugaji wamekuwa wakiwavamia kwenye makazi yao usiku na kuwajeruhi kwa silaha za kienyeji.

“Hali ni mbaya sana huku, yaani tunaishi kama hatuna Serikali kwa sababu hakuna hata kiongozi mmoja anayetujali.

“Huku watu wanachinjwa kama kuku na mfano halisi ni jana, ambapo wafugaji walimchinja dereva wa bodaboda, lakini hakuna anayejali.

“Hapa tulipo hatuelewi hatima yetu, ingawa msimamo wetu ni kutoondoka hapa kwa sababu kilimo ndicho kinachotusaidia katika maisha yetu,” alisema Machaku.

Naye, dada wa mmoja wa marehemu aliyeuawa wakati wa mapigano hayo, Sada Ally ambaye ni mkulima, alisema mdogo wake alifariki baada ya kuchomwa mkuki tumboni.

“Mdogo wangu baada ya kuchomwa mkuki tumboni, tulimpeleka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kwa bahati mbaya, alipoteza maisha wakati akitibiwa.

“Serikali naomba itusaidie jamani, wakulima tunateseka huku Kiteto kwa sababu hatuna mtu wa kutuangalia kwani viongozi wetu wote wanawatetea wafugaji,” alisema Sada.

Kwa upande wake, Msemaji wa Chama cha Wakulima na Wafugaji Wilaya ya Kiteto (CHAWAKI), Hassan Losioki, alisema chama chake kinaitaka Serikali irejeshe ardhi vijijini kwa mujibu wa sheria namba nne na tano ya mwaka 1999, ili wananchi waweze kufanya uamuzi wa matumizi ya ardhi wao wenyewe.

“Mgogoro huu ni wa muda mrefu, kwani umedumu kwa miaka nane sasa na kila mwaka unapofika msimu wa kilimo, lazima watu wanapoteza maisha kama ilivyo kipindi hiki.

“Kwa maana hiyo, tunaiomba Serikali iingilie kati kwani inavyoonekana kuna upande unapendelewa na baadhi ya viongozi na upande mwingine hauangaliwi japokuwa unaumizwa,” alisema Losioki.

Pamoja na hayo, alisema vijiji vitano kati ya saba vilivyo kwenye hifadhi hiyo, vimehama kutoka katika hifadhi inayogombewa baada ya vikao vya Serikali kufanyika.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Nati, Emaliti, Engusilisidani, Lotepesi na Kimana.

Naye, OCD Dinya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alikiri kwamba, hali si shwari wilayani Kiteto kutokana na mauaji yanavyotokea.

“Mimi siwezi kuzungumzia mauaji yaliyotokea kuanzia Desemba 16 mwaka huu, kwa sababu nilikuwa likizo. Lakini ninachojua ni kwamba, kuna mfugaji mmoja aliuawa wakati wa mapigano na amezikwa jana.

“Lakini, leo (juzi) kuna watu wawili wamejeruhiwa na wamepelekwa hospitali na kutokana na hali ilivyo, polisi wanaendelea na doria,” alisema OCD Dinya.

Wakati OCD akisema hayo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kiteto, Martha Umbura ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), aliliambia MTANZANIA kwa simu jana, kwamba wilayani Kiteto hakuna vurugu zozote wala mauaji yaliyowahi kutokea.

“Niko kwenye kikao cha RCC subiri nitakupigia nikimaliza. Lakini kwa kifupi ni kwamba, huku hakuna vurugu wala mauaji yaliyotokea,” alisema Umbura na kukata simu.

Hivi karibuni, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliitisha mkutano na wakulima wilayani Kongwa, ambapo alisema vurugu kati ya wakulima na wafugaji zinazoendelea wilayani Kiteto, zimesababisha vifo vya watu wengi na kwamba aliwahi kushiriki mazishi ya mkulima mmoja aliyeuawa na wafugaji.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, alisema mgogoro huo unachochewa na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, kwa kuwa wananufaika nao kwa njia haramu.

Pamoja na hayo, aliwaahidi wakulima hao ambao wengi wanatoka jimboni kwake, kwamba atafanya kila linalowezekana ili mgogoro huo umalizike kwa amani kwani wanaonyanyaswa zaidi ni wakulima.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top