
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya
Katiba juzi. Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na
Rais Ali Mohamed Shein, Karimjee, Dar es Salaam
Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya
litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu
hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na wananchi wa kada
zote itatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa Rasimu
ya Kwanza ya Katiba ambayo ilijadiliwa na kuboreshwa katika Mabaraza ya
Katiba yaliyoketi kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo itafanyika leo saa
6.00 mchana katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na asasi
mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba
ndiye atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la Katiba
linalotazamiwa kuanza vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa au kupunguzwa
katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza kama kuna
kilichoondolewa au kurekebishwa... kesho (leo), Watanzania watapata
fursa ya kujua mapendekezo ya tume, wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kujua kama
yamefanyiwa marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni pamoja na mfumo na
muundo wa Muungano, umri wa kugombea urais, wabunge kutokana na mikoa,
umri wa kugombea urais na mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Rasimu ya
Kwanza ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na alipokuwa akizungumzia
hilo wakati akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji Warioba alisema uamuzi huo
ulifikiwa kwa kuwa yalikuwa ni maoni ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilizua mjadala mkubwa
kwani chama tawala, CCM, kilipinga na kuweka bayana kwamba kinataka
muundo wa Muungano uendelee kuwa wa Serikali mbili.
Vyama vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono
pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi
kwa kutaka Zanzibar ipewe mamlaka ya kuwa na dola kamili.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Katika Rasimu ya Kwanza ilipendekezwa mambo saba tu ndiyo yabakie kwenye mamlaka ya Muungano.
Mambo hayo ni pamoja na Katiba na Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji,
Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru
wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mambo hayo, ilipendekezwa na Tume hiyo kuwa chini
ya wizara ambazo zitaongozwa na mawaziri wakazi ambao hawatatokana na
wabunge kwani watatakiwa kuchaguliwa nje ya taasisi hiyo.
Kurejeshwa kwa jina la Tanganyika
Baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza, mjadala
mwingine ulioibuka hasa baada ya kupendekezwa kwa muundo wa Muungano
kuwa wa Serikali Tatu ni hatua ya Tume kuendelea kutumia jina la
Tanzania Bara.
Baadhi ya wadau walikosoa pendekezo hilo wakitaka jina la Tanganyika litajwe katika Katiba badala ya Tanzania Bara.
Katika Rasimu ya Kwanza, Tanzania Bara na Zanzibar zilihesabiwa kuwa washirika wa Muungano.
Ikiwa Serikali tatu zitarudishwa swali linakuja
kama Tanzania Bara itatumia jina la Tanganyika ambalo ililitumia kuanzia
mwaka 1961 hadi 1964 ilipoungana na Zanzibar.
Kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu
Rasimu ya kwanza ilipendekezwa kufutwa kwa wadhifa
wa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Muungano na badala yake kupendekeza
kuwapo kwa Rais na Makamu wake.
Baadhi ya wadau walihoji juu ya usimamizi wa kazi za kila siku za Serikali jukumu ambalo kwa sasa lipo kwa Waziri Mkuu.
Umri wa kugombea urais
Suala hilo nalo lilizusha mjadala mkali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
Mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza yalitaka moja ya
sifa za mgombea urais kuwa miaka 40 lakini baadhi ya wanasiasa, hasa
vijana, wametaka umri huo ushushwe hadi miaka 35.
Wagombea binafsi
Jambo jingine lililopendekezwa katika Rasimu ya Kwanza ni kuwapo kwa mgombea binafsi kuanzia ubunge hadi urais.
Hilo halikuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wadau
mbalimbali kutokana na ukweli kwamba ni jambo ambalo limekuwa
likipigiwa kelele kwa muda mrefu na wananchi.
Muundo wa Bunge la Muungano
Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuwa wabunge watakuwa 75.
Kwa maana ya 50 kutoka Tanzania Bara, 20 kutoka
Zanzibar na watano kutoka kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais kwa
ajili ya kuwatetea watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza, wabunge wa kuchaguliwa watagombea kupitia mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ilipendekeza kuwa kila mkoa
utachagua mbunge mmoja wa kike na wa kiume ili kuleta uwiano na
kupendekeza kufutwa kwa viti maalumu suala ambalo lilizua mjadala.
Haki za Binadamu
Moja ya mambo ambayo yaliibuka mjadala ni haki za
binadamu. Katika Rasimu ya Kwanza, ilipendekezwa kuundwa kwa Tume ya
Haki za Binadamu itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe
wasiozidi saba.
Lakini wadau wengi waliotoa maoni yao walitaka sheria kandamizi 40 za Tume ya Nyalali zisiwepo katika Katiba Mpya.
Mambo mengine
Kuhusu madaraka ya Rais, Tume hiyo ilipendekeza
katika Rasimu yake ya Kwanza kwamba yabaki kama yalivyo hasa kwa uteuzi
wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo
vingine katika uteuzi.
Katika Rasimu hiyo ya Kwanza, pia ilipendekezwa
kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi hiyo itaachwa na
mgombea binafsi lakini kama ni wa kutoka katika chama cha siasa, ijazwe
na mtu kutoka chama chake.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Tume hiyo ilipendekeza
katika Rasimu ya Kwanza kwamba jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC),
libadilishwe na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu hiyo, ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama
ya Juu (Supreme Court), majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani
watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment