Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji Mark Bomani.
 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji Mark Bomani, ametofautiana na CCM kuhusu muundo wa Muungano akiunga mkono pendekezo la kuwa na Serikali tatu, lakini akitaka ya Bara iitwe Serikali ya Tanganyika.
 
Juzi, Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Dodoma ilitoa tamko ikisema chama hicho kinaamini katika muundo wa Serikali mbili, lakini Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani kwa miaka 11 na mwanachama wa CCM, aliipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kupendekeza muundo wa Serikali tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Bomani alisema: “Pendekezo la kuwa na Serikali tatu limekuwa likipendekezwa na tume zote zilizowahi kuundwa kuhusu muundo wa Muungano.”
Bomani alizitaja tume hizo kuwa ni ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991 na Kamati ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998.
“Msimamo wa jana (juzi) wa Kamati Kuu ya CCM kidogo unanikanganya kwa upande kuna hisia kuwa chama hakitaki Serikali tatu,” alisema Bomani.
Mwanasheria huyo alisema muundo wa Serikali mbili uliopo ulibuniwa haraka haraka na waasisi wa nchi hizi mbili Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Karume.
Alisema migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara hasa kwa upande wa Zanzibar, itapungua kwa kuwa na mfumo wa Serikali tatu.
Mwanasheria huyo alisema woga wa gharama za mfumo wa Serikali tatu hauna msingi na kwamba kuna mifano ya Muungano wa nchi nyingi duniani.
Kuhusu Tanganyika alisema: “Hili jambo la kuziita katika Rasimu ya Katiba Mpya Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar silipendi hata kidogo, tunaogopa nini kuiita Serikali ya Tanganyika,” alisema Bomani na kuongeza kuwa suala hilo lilikosewa na Tume ya Jaji Warioba.
Alisema kabla ya nchi hizo mbili hazijaungana ziliitwa Tanganyika na Zanzibar ndipo baada ya Muungano ikazaliwa Tanzania lakini vigogo wengi wanaona shida kutaja Tanganyika.
Pia Bomani alisema kabla ya rasimu hiyo haijapendekeza muundo wa Muungano wananchi walitakiwa waeleze kama bado wanautaka au la.
Aidha, Bomani alitaka rasimu hiyo iwe na kipengele kinachoonyesha upatikanaji wa huduma za elimu na afya ambavyo ni vitu muhimu katika maisha ya binadamu.

 Sijaona wamefafanua kuhusu elimu na afya, rasimu ya Katiba itamke wazi kuwa ni wajibu wa Serikali hasa za nchi kutoa elimu kwa kiwango fulani bure na iwe ni ya lazima, pia itoe matibabu kwa raia wake bure katika hospitali zake,” alisema Bomani.
 
Kuhusu spika na mawaziri, Jaji Bomani alitofautiana na mapendekezo ya Rasimu kwamba wanaoteuliwa katika nafasi hizo wasiwe wabunge... “Kwa maoni yangu, Spika au Waziri anaweza kuwa mbunge lakini akishateuliwa anaacha ubunge, hivi wanafanya Marekani, Ufaransa na nchi mbalimbali.”
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top