KATIKA hali isiyo ya kawaida, juzi wafanyabiashara wa maduka makubwa eneo la Buzuruga walilazimika kujifungia ndani na wengine kukimbilia kusikojulikana, baada ya watu wanaodaiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha, kuvamia eneo hilo kwa lengo la kuiba fedha.
Tukio hilo lilitokea saa moja usiku, wakati wafanyabiashara hao wakiwa katika harakati za kufunga maduka yao ambapo ghafla walishtukia milio ya risasi kwenye mabanda ya wafanyabiashara wa M- Pesa, Tigo -Pesa na Airtel Money.

Hali hiyo ilizua tafrani eneo la Buzuruga ambalo ni kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, ambapo abiria waliokuwapo walilazimika kukimbia kwa lengo la kunusuru maisha yao.

Hata hivyo majambazi hayo, yakitumia usafiri wa pikipiki, hayakufanikiwa kuchukua fedha kutokana na wafanyabiashara kujifungia ndani.

Bodaboda zilizingira eneo hilo kitendo kilichofanya majambazi hayo kuwatawanya kwa risasi za hewani na kupata upenyo wa kutoweka eneo hilo.

Akizungumza na RAI jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema jeshi limejipanga kufanya doria muda wote nyakati hizi za kuelekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.

“Ni kweli tukio hilo lilitokea jana (juzi) jioni, lakini majambazi hao hawakufanikiwa kuiba kitu chochote na taarifa ilipotufikia polisi waliwahi kufika eneo hilo.

“Tunaendelea kuwasaka lakini jambo kubwa ninaloomba kwa wananchi ni ushirikiano na Jeshi la Polisi, wao wana nafasi kubwa ya kuwabaini wasio na mwenendo mzuri, tukipata taarifa tunatumia utaalamu kuwakamata.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top