Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd
CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimedai kusikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Pindi Chana, ya kutaka kuwabebesha mzigo usio wao.

Wakati ADC wakimtaka Chana abebe msalaba wake, Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutousaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji, alisema kuwa wamesikitishwa na kufadhaishwa na upotoshwaji wa makusudi unaoendelea kufanywa dhidi ya kiongozi wao aliyeshiriki kutoa maoni juu ya muswada huo.

Alisema kauli iliyotolewa na Chana bungeni kuhusu chama hicho kuwakilishwa katika kamati yake si sahihi, kwani wao kama walivyokuwa waalikwa wengine walitoa maoni yao na si ya kuwawakilisha Wazanzibari kwa ujumla wao.

“Kutaja kwamba ADC ni miongoni mwa vyama vilivyotoa maoni kwa niaba ya Wazanzibari, jambo hilo si la kweli,” alisema.

Miraji alisema kuwa kitendo hicho kinaweza kuihujumu ADC na kuisalitisha kwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, jambo ambalo hawawezi kulinyamazia.

“Ushahidi upo wa ADC kushiriki kama mdau katika kikao hicho, hivyo wanaopotosha ukweli kuhusu jambo hili waache mara moja na wanapojibizana bungeni wasitumie ADC kama ngao ya kujikingia,” alisema.

Alisema ADC kama vyama vingine vya siasa na mdau wa muswada ilipokea barua ya mwaliko kutoka kwa Katibu wa Bunge iliyosainiwa kwa niaba yake na Ruhilabake Julai 22, ikiwa na Kumb. Na. BA. 50/56/01/04 ikiwataka kutuma wawakilishi na ikafanya hivyo.

Alisema katika uwakilishi huo walimtuma aliyewahi kuwa mbunge wa CUF, Shoka Khamis Juma na ambaye kwa asili ni Mzanzibari na alifuatana na Mwamvita Mangupili.

“Kitendo cha kumtuma Shoka hatumaanishi kuwa anawatetea Wazanzibari, sisi tulifanya kama ilivyokuwa kwa CCM, CHADEMA, CUF, NCCR na vyama vingine mbele ya kamati hiyo,” alisema.

CUF nacho kupitia msemaji wake visiwani Zanzibar, Salim Biman, mbali na kumtaka Rais Kikwete asitie saini muswada huo kuwa sheria pia kililaani kitendo cha Naibu Spika, Job Ndugai, kumdhalilisha kiongozi wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe.

Biman alisema kuwa muswada huo haukushirikisha Wazanzibari wala asasi za kiraia, hivyo wamemuomba Rais Kikwete kutousaini kwa kuwa haukutenda haki.

Alisema kuwa muswada huo unapaswa kurejeshwa kwa Watanzania ili ukajadiliwe hatua itakayosaidia kuondoa manung’uniko yaliyopo.

Alisema kuwa kamati ya Chana haikutenda haki kwa Wazanzibari kwani imeonesha haina nia njema juu ya suala hilo.

Alisema kuwa iwapo Rais Kikwete atakapuuza suala hilo kuna hatari ya mchakato huo kukwama na baadhi ya asasi kukimbilia mahakamani kusimamisha suala hilo ambalo limegharimu fedha nyingi.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wameamua kummaliza Rais Kikwete ili aendelee kuchukiwa na upande wa Zanzibar.

Biman alisema kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, ameamua kuizamisha Zanzibar kwa ajili ya masilahi ya chama chake huku akifahamu kuwa upande huo haukushirikishwa katika muswada huo.

“Tunampongeza Tundu Lissu kwa kuamua kuwa mstari wa mbele kuitetea Zanzibar lakini kiongozi ambaye tuliamini ndiye mwenzetu kaamua kutuzamisha na imeonesha kuwa hatuko naye,” alisema.

Katika hotuba yake bungeni, msemaji mkuu wa upinzani kwa Wizara ya Sheria na Katiba, Tundu Lissu, alisema kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekwishatoa Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 19(1)(d) cha Sheria.

Alisema rasimu hiyo imependekeza mabadiliko makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano kwa kupendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu.

“Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu hii kwa mujibu wa kifungu cha 18, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 20(1).”

“Baada ya hapo, Rais, “atachapisha rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalumu kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa,” alisema.

Lissu alisema ili kutimiza matakwa haya ya sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge tukufu linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “...haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.

“Hii ina maana kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55. Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalumu inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke yake,” alisema. 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top