LICHA ya hujuma ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ufanisi mdogo wa
Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimeibuka na ushindi mnono katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata nne
za jijini Arusha.
Katika Kata ya Elerai, mgombea wa CHADEMA Injinia Jeremia Mpinga
alimbwaga Emanueli Laizer wa CCM kwa kura 1,715, dhidi ya 1,239.
Kata hiyo ilikuwa na wapiga kura 23,797 waliojiandikisha na vituo 55
vya kupigia kura, lakini idadi kubwa ya wananchi hawakujitokeza.
Matokeo ya kura yalitangazwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi
zaidi ya 40 wenye silaha, na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wafuasi na
mashabiki wa CHADEMA.
Katika Kata ya Kaloleni, mgombea wa CHADEMA, Kessy Emmanuel Miliare
alimshinda kwa mbali mgombea wa CCM kwa kura 1,470 dhidi ya 530, wakati
mgombea wa CUF ameambulia kura 275. waliojiandikisha 12,674 waliopiga
kura 2,292. Kura halali ni 2,277 na zilizoharibika 15.
Akitangaza matokeo katika Kata ya Themi, Msimamizi wa Uchaguzi, Editha
Mboye alimtangaza mgombea udiwani wa CHADEMA, Mallance Kinabo kuwa
mshindi kwa kupata kura 678, akimwacha mbali mgombea wa CCM Victor
Mkolwe aliyepata kura 326, huku yule wa CUF, Lebora Ndervai akipata kura
313.
Kata ya Kimandolu, CHADEMA pia wameibuka na ushindi mkubwa na kuiacha vibaya CCM.
Mgombea wa CHADEMA, Elishadai Ngowi amemshinda mgombea wa CCM, Edina Sauli kwa kura 2,265, dhidi ya 1,169 za mpinzani wake.
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Jiji la Arusha lilizizima
kwa shangwe na nderemo, huku idadi kubwa ya watu wakijipongeza kwa
ushindi huo mkubwa.
Mwigulu Nchemba atimua
Matokeo hayo ambayo yameonekana kuwasononesha viongozi na wanachama
wa CCM, yalimfanya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, kuondoka
kimya kimya jijini hapa kwa kutumia gari maalumu.
Mwigulu ambaye aliongoza kikosi cha CCM katika kampeni za kimya kimya,
majira ya jioni alionekana akielekea Moshi, huku wasaidizi wake
wakiwemo wabunge wakitoweka katika vituo vya kuhesabia kura.
Mapema, wabunge wa CHADEMA na wa CCM tangu asubuhi walikuwa
wakizunguka katika kata hizo, huku Mbunge wa Viti Maalumu, Catherin
Mgige (CCM) akitumia gari ndogo, Salon yenye vioo vya giza alionekana
akizunguka kata zote jana.
Ulinzi mkali wa polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi Sabas jana aliongoza
kazi ya ulinzi uliokuwa na idadi kubwa ya askari polisi wenye silaha za
moto na mabomu ya machozi.
Akitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba TP 1715, Kamanda
Sabas alionekana akizunguka katika mitaa ya kata zote nne, zilizokuwa
zimesheheni idadi kubwa ya askari, wengi kutoka mkoani Kilimanjaro.
Waangalizi wa kimataifa
Katika tukio la kwanza la kihistoria, uchaguzi wa kata hizo
ulishuhudiwa na waangalizi wa kimataifa kutoka taasisi ya International
Low and Policy Institute yenye makao makuu yake nchini Norway, na wale
wa ndani kutoka Jukwaa la Katiba.
Kiongozi wa waangalizi kutoka Norway, Sterling Roop, akiongea na
Tanzania Daima alisema kuwa idadi ndogo ya wapiga kura imejitokeza na
uwepo wa dosari kadhaa umewafanya baadhi ya wananchi kukosa haki yao ya
kupiga kura.
Roop alisema pamoja na wananchi kuwa na shahada halali za kupigia kura
na majina yao kuwepo, lakini hakukuwa na picha zao katika daftari la
wapiga kura na hivyo wakazuiwa kupiga kura.
Katika vituo vingi, hususani Kata ya Kaloleni dosari kuu ilikuwa ni
kukosekana kwa majina katika daftari la kupiga kura kwa wananchi ambao
wana shahada na pia majina yao kubandikwa katika ofisi za kata kama
wapiga kura halali.
Majina ya wapiga kura yatoweka
Dosari kubwa iliwakumba wapiga kura baada ya majina, picha na maelezo
kukosekana kwenye daftari la wapiga kura karibu katika kata zote.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Hamid M Hamid alikiri
tatizo hilo na kudai kwamba tayari alishawasiliana na wataalamu wake wa
mifumo ya kompyuta (IT) ili washughulikie kasoro hizo kwenye kila kata
iliyokuwa ikiendelea na uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kuwa yeye si mchawi kuweza kubaini chanzo cha
hitilafu hizo zilizojitokeza. Baadhi ya upungufu uliobainika ni baadhi
ya watu kuandikishwa zaidi ya mara moja.
Kata ya Kaloleni kwenye kituo cha AICC Nursery B, mpiga kura Michael
Laurence alikuwa ameandikishwa mara tatu kwenye daftari la wapiga kura
akiwa na namba 48674955, 444666858 na 13142914.
Hata hivyo kwenye majira ya saa saba mchana, wataalamu wa kompyuta wa
Tume ya Uchaguzi walifika na kuanza kuwasaidia wananchi waliokuwa
wamejazana kwenye kituo cha kata hiyo.
Mmoja wa wataalamu hao, Siif Mtezo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa
tatizo hilo lilisababishwa na watu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema kilichowafanya wengi washindwe kuona majina yao ni hofu kama
ile inayowakumba wanafunzi wanaoenda kuangalia matokeo, na kwamba tume
ililazimika kuwapigia simu wananchi wengi waliokuwa wameondoka, na
wakarudi kupiga kura.
Wakala wa Chama cha Wananchi (CUF), Malik Abbas kwenye kituo hicho
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wananchi wengi walifika, lakini
majina yao hayakuonekana na wakaondoka, huku akionyesha baadhi ya picha
ambazo hazionekani vizuri kutokana na kufifia kwenye daftari hilo.
Mgombea udiwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CUF, Abbas Darwesh alisema
wananchi wengi walishindwa kupiga kura akiwemo mtoto wake Omary Othman
ambaye pamoja na kuwa na kitambulisho chake namba 32479962 jina lake
halikuonekana kwenye orodha.
“Inawezekana kweli kuna mchezo mchafu umefanyika kubadili daftari la
wapiga kura kama ambavyo tetesi zilikuwa zimezagaa, kwa sababu mtoto
wangu mwenyewe alipiga kura kwenye kituo hiki katika uchaguzi wa 2010,
lakini leo naambiwa jina lake halipo,” alilalamika Darwesh.
Msimamizi wa uchaguzi Kata ya Kaloleni, Anna Lebisa amekiri kukosekana
kwa majina ya wananchi katika daftari licha ya kuwepo katika mbao za
matangazo na kusema hawakuruhusiwa kupiga kura.
Miongoni mwa waliokumbwa na kadhia hiyo ni Omari Othmani na mtangazaji
wa TBC, Khalifa Mshana ambaye alilazimika kulifikisha suala lao kwa
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Hamid
Mahmood ambaye alimuachia ofisa wa tume kulishughulikia.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba akiwa na timu yake ya
waangalizi wa uchaguzi huo, alisema kura zimeanza kupigwa taratibu na
idadi ndogo ya watu kujitokeza akidai kumechangiwa na hofu kubwa baada
ya kuwepo kwa askari wengi katika vituo vya kupigia kura.
“Wingi wa askari wenye silaha za moto katika vituo vya kupigia kura
umechangia kufanya baadhi ya wananchi kutojitokeza kwa hofu ya askari
hao,’’ alisema Kibamba.
Wafuasi wa CHADEMA watekwa, wapigwa
Matukio ya kutekwa na kupigwa kwa wafuasi wa CHADEMA yalijiri katika uchaguzi huo jana.
Vijana wanaoaminika kuwa ni wa CCM, wakiwa ndani ya gari aina ya Land
Cruiser iliyoegeshwa kwenye uwanja wa AICC wa Soweto waliwakamata na
kuwapiga baadhi ya wananchi waliokuwa wakielekea katika vituo vya
kupigia kura eneo la Soweto.
Msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Kaloleni, Lebisa alikiri kuliona gari
hilo majira ya saa tatu asubuhi. Aliwaelekeza polisi waliokuwa kwenye
kituo hicho kuwafuatilia, lakini waliondoka kabla hawajakamatwa.
Aidha, mwananchi mwingine, Hassan Noor ambaye alikuwa wakala wa
CHADEMA kwenye kituo cha AICC Nursery alishindwa kufanya kazi hiyo baada
ya kunyang’anywa barua yake na vijana waliokuwa kwenye gari aina ya
Land Cruiser ya rangi ya maziwa ambayo namba zake hakuzishika.
Akiongozana na wenzake wawili kwenye mzunguko karibu na kituo hicho
cha kupigia kura, Noor aliona gari hilo likisimama karibu yao na
kuwataka waondoke eneo hilo. Aliwaeleza kuwa ni mawakala, ndipo
walipomtaka awaonyeshe barua.
“Nilijua ni askari, na nilipowapa wakaninyang’anya na kuichana. Kisha
wakampiga mwenzangu Boniface Kimaro. Alipigwa na kitu kama chuma
kichwani na wakaondoka. Tumeripoti Kituo cha Kati cha Polisi,” alisema.
Katika Kata ya Kimandolu, watu sita walikamatwa wakiwa wamekaa katika
gari moja na kupelekwa polisi kwa mahojiano, hali hiyo ikajitokeza tena
katika Kata ya Kaloleni pia, ambako watu wasiojulikana walikamatwa
wakiwa wamejificha ndani ya gari.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment