WAKATI Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema leo
anakutana na waandishi wa habari kuzungumzia suala la vyama vya siasa
kuwa na vikundi vya ulinzi, jeshi hilo limeendelea kuwa kimya kuhusiana
na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumiliki kikundi cha vijana cha Green
Guard.
Badala yake polisi wameendelea kukikamia na kutoa vitisho zaidi kwa
chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufuatia msimamo wake wa
kuendelea na hatua yake ya kuimarisha chama chao kwa ajili ya mafunzo ya
ukakamavu kusaidia kujilinda.
Tangu kutolewa kwa tamko la CHADEMA kutaka kuendesha mafunzo kwa
vijana wake wa Red Brigade kama wafanyavyo CCM kwa Green Guard, polisi
wameendelea kusisitiza kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa
juu wa chama hicho kutokana na kile walichosema kuunda kikosi cha
kijeshi kinyume na sheria.
Juzi msemaji wa polisi, Advera Senso aliweka wazi kuwa wiki hii
watachukua hatua kali za kisheria dhidi ya viongozi wa CHADEMA na
kuwaonya vijana kote nchini, kukataa kutumiwa na wanasiasa waliodaiwa
kutaka kuhatarisha amani ya nchi.
Mbali na polisi, mamlaka nyingine zilizokemea uamuzi wa CHADEMA ni
pamoja na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alisema kinachotaka kufanywa na
chama hicho kimelenga kuhatarisha amani.
Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia naye juzi
alikaririwa akiishambulia CHADEMA kwa uamuzi huo aliouita ni wa hatari.
Hata hivyo, kwa makusudi ama kwa lengo la kukana ukweli, Jeshi la
Polisi limekuwa likikwepa mara zote kugusia kuhusiana na CCM kumiliki
kikosi cha Green Guard, ambacho baada ya kubanwa na waandishi wa habari,
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alikiri wiki iliyopita kuwa kipo
na kinafanya kazi ya kulinda usalama wa viongozi na wanachama katika
shughuli zao.
Kadhalika, jeshi hilo limeonekana kupuuza na kutotaka kuzifanyia kazi
taarifa za matukio mabaya ya kupiga, kuteka na kujeruhi yaliyofanywa na
Green Guard dhidi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA.
Hadi sasa sio IGP Mwema, ama afisa yeyote wa ngazi ya juu wa polisi
aliyetamka waziwazi kuikemea CCM kama wanavyofanya kwa CHADEMA.
CHADEMA kimeripoti katika Jeshi la Polisi, matukio ya kikatili
waliyofanyiwa na vijana hao wa CCM katika mikoa ya Tabora, Dar es
Salaam, Mwanza na Iringa, yakiwemo mauaji ya kada wake wa Arumeru mkoani
Arusha.
Msimamo wa CHADEMA
Kwa upande wake, CHADEMA imezidi kumtaka IGP Mwema kuweka wazi sababu
za msingi zinazomfanya hadi sasa apate kigugumizi na kushindwa kutamka
ikiwa ni halali kwa CCM kumiliki kikosi cha vijana kwa ajili ya ulinzi
wao, lakini iwe nongwa na dhambi kubwa kwa vyama vingine vya siasa.
Taarifa ya CHADEMA kwa vyombo vya habari jana imelishutumu Jeshi la
Polisi kwa kushindwa kuichukulia hatua CCM ambao kwa miaka mingi
imehodhi kikosi hicho cha vijana ambacho wamedai kimehusika na matukio
mengi ya kikatili.
“Jeshi la Polisi wameshindwa kutoa kauli kwa CCM kumiliki kikundi cha
ulinzi, ambacho kimekuwa kikifanya mazoezi ya kijeshi kama kule Igunga,
kikituhumiwa kushambulia, kupiga, kuteka na kutesa wapinzani wa CCM.
“Kwa mfano, wabunge Kiwia (Hainess) na Machemli (Salvatory)
walishambuliwa Kirumba, Peter Msigwa, akashambuliwa Iringa, Mbwana
Masoud akapigwa Igunga, na marehemu Msafiri Mbwambo ambaye waliomuua
walitoroka mbele ya polisi wenye silaha mahakamani,” imesema taarifa ya
CHADEMA.
Aidha, chama hicho kimesema kuwa hadi sasa hakuna ripoti ya kutekwa na
kuteswa kwa Dk. Stephen Ulimboka, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Absalom Kibanda, ukweli wa waliolipua bomu Kanisa Katoliki la Olasiti na
katika mkutano wa CHADEMA, Soweto mjini Arusha.
CHADEMA wamezidi kuongeza kuwa Green Guard wameshutumiwa pia
kuwashambulia waandishi wa habari nchini, na kuwataja waliofikwa na
vipigo hivyo kuwa ni Frederick Katulanda wa Mwananchi, mwaka 2010 katika
uchaguzi mkuu huko Kwimba, Munir Zakaria wa Channel Ten huko Bububu
Zanzibar na Musa Mkama wa Dira katika uchaguzi mdogo wa Igunga.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment