Katibu Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
VIONGOZI waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, na Naibu
Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, wameaswa kuacha siasa za
kueneza chuki kwa CHADEMA na Katibu wake, Dk. Willibrod Slaa.
Badala yake wametakiwa kunadi sera na ilani ya uchaguzi ya CCM ili
wananchi wajue serikali ya chama chao inafanya nini katika kutekeleza
kile ilichowaahidi mwaka 2010.
Rai hiyo ilitolewa jana na kada wa CCM mkoani Morogoro, David Mgesi,
katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam.
Mgesi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Morogoro kabla ya
kujiunga CCM mwaka 2005, alisema kuwa anasikitishwa kuona Mwenyekiti
wao, Rais Jakaya Kikwete, akiwafumbia macho Wasira na Nchemba wakati
wakiendelea kukiua chama.
Hata hivyo, Wasira alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alizungumza kwa
kifupi akitaka kujua nani amesema na alipotajiwa alisema, “Hayo ni maoni
yake.”
Wasira alipoulizwa kama ni kweli anatumia mgongo wa CHADEMA
kujitafutia umaarufu wa kupitishwa na CCM kuwania urais 2015 alijibu:
“Kama ungekuwa unaandika kwa Kiingereza ungeweza kusema ni ‘rubbish’,
mimi niko huku jimboni hata sasa nakagua shughuli za maendeleo.”
Kuhusu Nchemba, yeye simu zake zilikuwa hazipatikani muda wote.
Katika madai yake Mgesi alisema, “Kila wanaposimama kuzungumza iwe
jukwaani au kwenye vyombo vya habari propaganda yao ni moja ya kuitukana
CHADEMA na Dk. Slaa kana kwamba CCM haina ajenda wala ilani.”
“Wasira na Nchemba wamekuwa viongozi wa kueneza matusi, chuki kuhusu
CHADEMA wala hawana hoja lakini wameachwa waendelee kukiua chama,”
alisema.
Kada huyo ambaye alitamba kuwa yuko radhi kusulubiwa hata ikiwa ni
kutobolewa macho, alidai kwamba viongozi wengi wa CCM wamekuwa na tabia
ya kutotaka kukosolewa, kama walivyo Wasira na Nchemba ambao
wanaendeleza chuki kwa kila anayewakosoa.
“Waache kumwandamna Dk. Slaa bali CCM itafute mgombea makini
atakayekuwa na vigezo vya kupambanisha naye katika uchaguzi mkuu ujao.”
“Hawa wote wanaojitapa na kupigiwa debe ndani ya CCM ili kugombe
urais, hakuna mwenye sifa za kulinganishwa na Dk. Slaa. Sasa badala ya
sisi kujipanga kwenye chama kumtafuta mtu asiye fisadi, tunajadili
propaganda za uzushi kwa CHADEMA,” alisema.
Mgesi alifafanua kuwa wananchi wa sasa wamebadilika na kwamba hawawezi
kuelezwa uongo kila wakati wakaukubali, hivyo salama ya CCM ni
kuwaeleza imefanya nini badala ya kueneza propaganda za chuki kama
wanavyofanya viongozi wake.
“Hata ukiwatisha wananchi kwa kuwanyofoa kucha, kuwang’oa meno na
kuwatoboa macho wale wanaojitokeza kusema ukweli wa kukosoa bado
haisaidi isipokuwa ni kuukubali ukweli na kujipanga.”
“Mimi kama kada mtiifu wa CCM sijaona mtu wa kumkabili Dk. Slaa kati
ya wale wanaojitokeza kuutamani urais. Chaguzi zetu zimejaa rushwa sasa
unategemea kwa staili hiyo mtu muadilifu kama huyo utampataje?” alihoji
Mgesi.
Kada huyo aliongeza kuwa aliondoka CHADEMA na kujiunga CCM akiwa na
matumaini kuwa Kikwete ni muumini wa sera ya ujamaa, hivyo angeweza
kurejesha misingi ya Azimio la Arusha.
“Matumaini yangu yalikuwa kinyume, wala hakuna tena ujamaa lakini
ninachopigania sasa ni utetezi wa watu hasa wanyonge. Nitaendelea kuwa
ndani ya CCM na anayekataa ukweli huu aje nitamuelimisha,” alitamba.
Kuhusu CCM kushughulikia kero za wananchi, Mgesi alidai viongozi wengi
ni wabinafsi na ndiyo maana wameshindwa kumsaidia Rais Kikwete.
Alitolea mfano mamilioni ya fedha za wananchi zilizopotea katika upatu
wa DECI akidai viongozi wakuu wengi wa serikali walishiriki katika
kuhamasisha biashara hiyo haramu.
“Mathalani mkoani kwangu tawi la DECI lilikuwa katika ofisi za CCM na
aliyelifungua ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Saidi Kalembo, akiwaagiza
watumishi wote wa ofisi yake kuhakikisha wanapanda mbegu.
“Kilosa tawi lilifunguliwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa
Mkullo. Hawa ndiyo viongozi wa serikali na CCM. Nilipohoji ufisadi huu
wakadai kuwa mimi bado nina Uchadema. Hapa tunawezaje kuwakomboa
wanyonge,?” alihoji.
Mgesi aliongeza kuwa hali hiyo iko hivyo hata kwenye ardhi, kwamba
wananchi wa wilaya ya Kilosa wameporwa ardhi yao na viongozi kwa mgongo
wa wafugaji na hivyo kuibua mgogoro mkubwa baina ya jamii za wakulima na
wafugaji.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment