Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe
SERIKALI ya Tanzania, leo inatarajia kutoa tamko juu ya mgogoro wa
mpaka wa Ziwa Nyasa dhidi ya Serikali ya Malawi.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema wamesikitishwa na kauli
ya Serikali ya Malawi, licha ya vikao husika vya kusaka suluhu
vikiendelea.
Alisema tayari Tanzania, inatambua kusudio la Malawi kwenda katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ), kwa lengo la kutaka kumiliki Ziwa Nyasa.
“Kesho (leo) kama Serikali tutatoa tamko letu juu ya mzozo huo, kama mnavyojua mgogoro huu umekuwa ukichukua sura tofauti, lakini mara zote Tanzania tunaamini mazungumzo ya amani ndio suluhisho pekee.
“Naombeni kesho (leo), njooni pale ofisini kwangu tutaeleza hali halisi na mazungumzo yalipofikia,” alisema kwa ufupi.
Mapema wiki hii, Rais wa Malawi, Joyce Banda aliwaambia waandishi wa habari wa nchi hiyo, kuwa anakusudia kuishitaki Tanzania katika Mahakama ya ICJ, kutokana na kudorora kwa mazungumzo.
Pia Rais Banda, alionyesha kukerwa na kamati ya usuluhishi kwa kile alichodai haionyeshi nia na dhamira ya kweli ya kumaliza tatizo hilo.
Hivi karibuni, Waziri Membe akiwa katika mahojiano ya kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na redio Clous FM, alisema Tanzania inaangalia njia zingine za kutafuta suluhu kabla ya kwenda mahakamani.
Alisema pamoja na mazungumzo kuzingatia diplomasia katika mikutano iliyokuwa ikifanyika, Malawi iliendelea na msimamo wao wa kudai wanamiliki eneo lote la Ziwa Nyasa.
Waziri Membe, alisema Tanzania iliendelea kusimamia kauli yake ya kila siku kwamba, inamiliki asilimia 50 ya ziwa hilo jambo ambalo Rais Banda analipinga vikali.
Kutokana na hali hiyo, tayari Malawi imetangaza kujitoa katika mazungumzo ya kidiplomasia.
Pia hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon aliipongeza Tanzania kuwa na msimamo wa kutafuta majawabu ya mzozo wa mpaka wake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.
Mzozo wa Malawi na Tanzania, umekuwa ukichukua sura mpya, huku Rais Banda akionekana wazi kutokuwa tayari kwa suluhu.
Via: Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment