Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekubali
kusitisha maandamano yake yaliyokuwa yafanyike leo katika majiji manne
ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza, kuwashinikiza Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo
Mulugo kuachia ngazi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),
Said Mwema akiwa pamoja na Kamishina wa Oparesheni (CP) Paul Chagonja,
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova na maofisa
wengine kukutana na viongozi wa CHADEMA chini ya Mwenyekiti, Freeman
Mbowe.
CHADEMA iliwapa viongozi hao wiki mbili tangu Februari 18 mwaka huu,
kuachia ngazi kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya
vinginevyo wangefanya maandamano makubwa leo kuwashinikiza wang’oke.
Hata hivyo, juzi serikali ilitangaza kuyasitisha maandamano hayo
ikidai inatoa nafasi kwa wananchi waweze kumpokea Rais wa China, Xi
Jinping ambaye alianza ziara ya siku mbili nchini, jambo ambalo CHADEMA
walilipinga na kusisitiza kuandamana.
Jana viongozi hao wa polisi na siasa walilazimika kukutana na
kuzungumza kwa kirefu na Mbowe hatimaye kufikia muafaka kwa CHADEMA
kukubali kusogeza maandamano yao hadi hapo baadaye.
Sababu nyingine iliyokataliwa na CHADEMA ni ile ya kwamba Tume ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda inayochunguza kiini cha matokeo mabaya ya
kidato cha nne 2012 inaendelea na kazi yake, wakidai kuwa tume hiyo
haishughulikii suala la Waziri wa Elimu na naibu wake kujiuzulu.
Katika mazungumzo hayo, Mbowe aliongozana na Katibu wa Baraza la
Vijana Taifa (BAVICHA), Deogratius Munishi na Ofisa habari wa chama,
Tumaini Makene ambapo walikubaliana na jeshi hilo kusitisha maandamano
hayo ili kutoa nafasi ya wananchi kushiriki kwa amani na utulivu katika
mapokezi ya Rais wa China.
“Mbowe na IGP Mwema wamekubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya
siku 14 ili kuona utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana
na kushirikiana pasipo migongano kwa pande zote mbili.
Februari 18, mwaka huu, akiwa mjini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Kanda
ya Ziwa Magharibi katika viwanja vya Furahisha, Mbowe alisema Kawambwa
na Mulugo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza
sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika
matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa
ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini
kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na
kuandika.
Katika matokeo hayo, Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla
waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na
asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini
waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820
(asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.
Katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la
pili 6,453, la tatu 15,426, la nne 103,327 na daraja sifuri 240,903.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment