Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema
SIKU 19 zikiwa zimepita baada ya tukio la kutekwa na kuteswa kinyama kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa taarifa ya mwenendo wa uchunguzi linaoufanya kuhusu sakata hilo kama lilivyoahidi awali.

Makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi, kwa nyakati tofauti walipoulizwa na MTANZANIA Jumapili kuhusu mwenendo wa uchunguzi huo unaofanywa na makachero 12, wamekuwa wakipiga danadana kueleza ukweli.

Sambamba na hilo, uchunguzi wa MTANZANIA Jumapili umebaini kuwa uchunguzi wa makachero hao hadi sasa haujawagusa majirani wa Kibanda na hata watu waliomuokota na kumpeleka hospitali akiwa mahututi nao hawajaitwa kuhojiwa na polisi.

Uchunguzi huo wa polisi pia haujawagusa wafanyakazi wenzake wala simu zake za mkononi zinazoaminika kuwa zinaweza kusaidia katika uchunguzi huo, nazo polisi hawajataka kuzikagua.

Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Ahmed Msangi, ambaye ni mmoja wa makachero wanaounda timu ya watu 12 wanaochunguza mkasa wa kutekwa na kuteswa kwa Kibanda, alipotafutwa na gazeti hili jana kupitia simu yake ya kiganjani ili kujua uchunguzi huo ulipofikia, baada ya kupokea simu alianza kufanya vituko.

ACP Msangi baada ya kupokea simu na kujuliana hali na mwandishi kujitambulisha, alipotakiwa kuthibitisha uwepo wake ndani ya timu hiyo na hatua ambazo timu hiyo imefikia katika uchunguzi wake, alianza kuita kwenye simu haloo, halooo, na hata mwandishi alipomwambia kuwa anamsikia ajibu kwa sauti ya taratibu, alizidi kupayuka kwenye simu neno haloo kisha akakata simu.

Alipopigiwa tena na tena, simu yake ilikuwa haipatikani, jambo lilioonyesha kuwa aliizima kabisa.

ACP Msangi ndiye aliyeongoza tume iliyoundwa kuchunguza tukio la kutekwa na kuteswa kinyama kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, ambayo hadi sasa majibu yake hayafahamiki.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta pia Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kupitia simu yake ya kiganjani na alipoulizwa kuhusu mwenendo wa uchunguzi wa sakata hilo, alieleza kuwa hana la kusema, kwa sababu anasubiri majibu ya tume hiyo.

“Tume ikishaundwa huwezi ukatoa taarifa mpaka wao waje na majibu na ndiyo tunasubiri, bado tunategemea baada ya muda muafaka tutatoa taarifa,” alisema Kamanda Kova.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Kamanda Kova alipoulizwa na gazeti hili kuhusu mwenendo wa uchunguzi huo, alisema kuwa suala hilo limekwishapita uwezo wake kwa sababu linashughulikiwa na ngazi ya makao makuu, hivyo wenye uwezo wa kulizungumzia ni maofisa wa makao makuu.

Siku moja baadaye, Kamanda Kova alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa taarifa ya mwenendo wa uchunguzi wa tukio la kutekwa na kuteswa kwa Kibanda ingetolewa na tume wiki iliyopita, jambo ambalo halikufanyika.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, naye ni mmoja wa viongozi waandamizi wa serikali waliokataa kuzungumzia sakata la Kibanda.

Nchimbi alikataa kuzungumzia kutekwa kwa Kibanda Machi 12, baada ya waandishi wa habari kumtaka afanye hivyo katika mkutano aliouitisha kutangaza uamuzi wa serikali kuwafukuza kazi polisi watano kwa kosa la wizi, kwa kile alichodai kuwa suala hilo ni dogo sana linashughulikiwa na Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, naye alipoulizwa sakata hili kupitia simu yake ya kiganjani, yeye alilihamisha kutoka makao makuu na kuelekeza Kanda Maalumu ya kipolisi ya Dar es Salaam kwa kueleza kuwa suala la Kibanda haliko mikononi mwa makao makuu, bali limekabidhiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kulichunguza.

Tangu tukio hilo lilipotokea, Jeshi la Polisi na viongozi waandamizi serikalini wamekuwa wakipiga danadada kuweka wazi ukweli wa waliohusika kumteka na kumjeruhi Kibanda, jambo ambalo limemsababisha kuibuka kwa hisia mchanganyiko kwa jamii kuhusiana na unyama huo.

Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wanaeleza kuwa huenda suala hilo likachukua mwelekeo unaofanana na ule wa tukio la Dk. Ulimboka, ambapo ni takribani miezi tisa sasa hakuna uhalisia wa aliyekamatwa akihusishwa na kutekwa kwake.

Licha ya Dk. Ulimboka kumtaja katika hati ya kiapo, Ofisa wa Ikulu, Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye mhusika mkuu wa kutekwa na kuteswa kwake, hakuna taarifa zinazoonyesha hatua alizochukuliwa Ofisa huyo, tofauti na ambavyo imekuwa ikichukuliwa katika matukio mengine ya kihalifu.

Kumekuwa na maswali mengi kuhusu utendaji kazi wa Jeshi la Polisi na wengi wa waliohojiwa kuhusiana na hilo wamehoji nguvu iliyotumika kuwasaka na kuwatia nguvuni watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Marehemu Liberatus Barlow, ambao walikamatwa siku 12 tu baada ya tukio.

Kamanda Barlow aliuawa Oktoba 13 mwaka jana, saa 8 usiku, kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Minazi Mitatu, huko Kitangiri Mwanza, wakati akimsindikiza Mwalimu Dorothy Moses nyumbani kwake, kutoka katika kikao cha harusi.

Baada ya tukio hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, aliongoza uchunguzi uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa na katika taarifa yake kwa IGP Mwema, alisema makachero walitumia mbinu mbalimbali kwa kuunda kikosi cha nguvu kazi kilichokuwa chini yake kilichojigawa kwenye makundi matatu, moja likiwa la ukamataji, la pili la mahojiano na tatu la intelijensia na makundi yote yalitumia njia za kisayansi, ikiwa ni pamoja na kufuatilia mitandao ya simu.

Tayari watu mbalimbali wamekwishaanza kuonyesha mashaka kuhusu uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Kibanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu ( LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba, alipozungumza na MTANZANIA Jumapili, alisema Jeshi la Polisi lina mambo ambayo halitaki kuyafanyia kazi, hivyo upo umuhimu wa kutafuta nguvu ya ziada ili ukweli uweze kubainika.

Bisimba alisema kuwa kuna masuala ambayo jeshi hilo linakwepa kujihusisha nayo kwa karibu na kutolea mfano tukio la Dk. Ulimboka kutokuwa na taarifa kamili hadi leo.

Makamu wa Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWT) na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Eusebia Munuo, alisema kuwa hiyo ni kazi ya polisi kuchunguza na kutoa taarifa hivyo waachiwe jukumu hilo.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema anashangazwa kuona polisi wakitumika kisiasa katika suala la msingi.

“Mbele ya safari itatugeuka, kwani tunajenga siasa kuwa ni kuteka, kuua watu na hata gazeti lililokuwa likiripoti kwa kina kutekwa kwa Dk. Ulimboka limefungiwa, hivyo ni mchezo wa kuigiza na hali hii ni mbaya kisiasa,” alisema Dk. Lwaitama.
Chanzo: Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top