Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo ameleta ujumbe wa salamu za Papa Francis,
ambaye amewataka waumini wake kuukataa ubaguzi wa kidini.
Akizungumza kwenye Ibada ya Matawi iliyofanyika
katika Kanisa Katoliki la St Joseph Visiwani Zanzibar jana, Kardinali
Pengo alisema Papa Francis amehimiza umoja miongoni mwa wafuasi wa dini
zote.
Papa Francis, ambaye ni raia wa Argentina
alichaguliwa kuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, Machi 13, mwaka huu
akichukua nafasi ya Papa Benedict wa 16 aliyestaafu.
Pengo alisema kuwa ujumbe huo unawagusa Watanzania
kwani katika siku za karibuni kumeibuka watu ambao wanadai kuwa
wanapigania imani na kwamba wanafanya hivyo kwa kuua watu wengine
kinyume na mapenzi ya Mungu.
Alisema vitabu vyote vya dini vinaelekeza kuwa
Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake, hivyo kitendo cha mwingine
kumuua mwenzake kwa kisingizio cha kutetea imani ya dini ni kufuru.
“Wakristo hatuwezi kuinua upanga kuua mtu eti kwa
kisingizio kuwa tunatetea Kanisa la Mungu,” alisema Kardinali Pengo,
ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa Papa mpya uliofanyika Vatican
City.
Kumekuwa na matukio ya viongozi wa dini
kushambuliwa katika siku za karibuni hasa Visiwani Zanzibar, akiwamo
Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki ambaye aliuawa.
Katika tukio lingine Katibu wa Mufti wa Zanzibar,
Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindikali wakati Padri Ambros Mkenda pia
wa Kanisa Katoliki alishambuliwa kwa risasi.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alisema
uharibifu wa mazingira umeathiri uoto wa asili na ndiyo maana hivi sasa
Zanzibar visima ambavyo awali vilikuwa vinatoa majisafi ya kunywa, sasa
vinatoa maji yenye chumvi.
Alisema hakuna tena msukumo ambao unayaondoa maji
chumvi katika mfumo, ili wapate majisafi ya kunywa jambo ambalo ni la
hatari na wanajamii wanapaswa kuliangalia kwa mtazamo wa kipekee badala
ya kuwa kama ilivyo sasa.
Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment