Waokoaji wakiwa hawana cha kufanya baada ya kukosa zana za kuokolea wakati jengo la ghorofa 16 lilipoporomoka |
- Idadi ya waliofariki katika jengo la ghorofa lililoporomoka katika mtaa wa Indira Ghandhi inaripotiwa kufikia 30.
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick (ambaye ameweka kambi katika eneo la maafa tangu yalipotokea Ijumaa,) amesema zoezi la uokoaji wa watu na miili ya marehemu itasitishwa hapo kesho mchana. Tayari Sadick alishatoa agizo la kusimamishwa kwa ujenzi wa jengo la jirani (pia orofa 16, linalomilikiwa na mfanyabiasahra Ali Raza) baada ya kubaini mjenzi ndiye mhandisi aliyehusika kujenga ghorofa lililoporomoka.
- Wapangaji wa maghorofa matatu yaliyopo jirani na eneo lililoporomoka wamehamishwa ili kuzuia maafa zaidi, baada ya ukaguzi wa majengo hayo kubaini kuwemo kwa nyufa.
- Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema bado msaada kutoka kwa wataalamu wa masuala ya uokoaji unahitajika ili kukamilisha shughuli hiyo haraka zaidi.
- Mbunge, James Mbatia amesema kutokana na kuendelea kutokea kwa majanga tofauti nchini, anakusudia kupendekeza katika kikao kijacho cha Bunge, kuundwa kwa kitengo maalumu cha uokoaji kitakachoshughulikia majanga yanayotokea. [wavuti.com inaunga mkono hatua (initiative) hii kwa kuwa iliwahi kuandika na kutamani kuwepo kwa dawati na kitengo maalumu cha kutoa ushauri na nasaha yanapotokea majanga, rejea maandiko hayo Februari 2010 (bofya hapa) na Februari 2013 (bofya hapa)].
- Ndugu wa ndugu wa marehemu wa maafa, wanalalamikia usiri na urasimu mrefu uliopindukia katika kutoa fedha kwa ajili ya kusafirisha miili ya ndugu zao. Fedha hizo zimetolewa na Shirika la Nyumba la Taifa, NHC, baada ya Mhe. Sadick kuwaomba wawasaidie.
- Kufa kufaana? Baadhi ya madereva wa magari yanayosomba vifusi vinavyosombwa kutoka kwenye eno la tukio, wameripotiwa kupeleka kifusi hicho katika sehemu ambazo hawajaelekezwa na kukiuza kwa kati ya Shilingi 20,000/= hadi 30,000/= kwa lori, badala ya kukimwaga Jangwani, ili kurejea haraka kwenye eneo la tukio.
- Watu wanane (8) wanashikiliwa na Serikali/Polisi kwa mahojiano zaidi kuhusu uzembe uliosababisha jengo hilo kuporomoka. Miongoni mwao ni viongozi wa Manispaa ya Ilala --Mhandisi Mkuu, Ogare Salu, Mhandisi wa majengo, Godluck Mbaga na Mkurugenzi Mkuu wa ukaguzi wa majengo, Wilbrodi Muliyabuso-- wengine ni Mhandisi Mshauri ambaye alijisalimisha Polisi pamoja na Diwani wa Kata ya Goba wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka, aliye mmiliki wa kampuni ya ujenzi ya Lucky Construction Limited.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment