KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga ameingia kwenye kashfa akidaiwa kuamrisha askari wa kikosi hicho mkoani Singida kuliachia gari lililokamatwa usiku likiwa na shehena ya mazao ya misitu juzi.

Kutokana na tukio hilo, askari mwenye namba D.9523 Koplo Azizi wa kituo kidogo cha polisi Ikungi mkoani Singida ameingia matatani baada ya kulikamata gari hilo lenye namba za usajili T 271 BTR na trela namba T 686 BTX lenye urefu wa futi 40.

Mbali na Koplo Azizi, pia kulikuwa na askari wengine wawili waliokuwa chini yake katika ukamataji huo.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa mara baada ya gari hilo kukamatwa, dereva wake alianza kuwatolea lugha za vitisho askari hao na kisha kupiga simu kwa mtu ambaye baadaye aliomba kuongea nao.

Inadaiwa kuwa askari hao walikataa kupokea maagizo ya kwenye simu na kumtaka dereva alipeleke gari hilo kituoni na kufuata taratibu zingine.

“Lile gari lilikuwa linatoka Shinyanga kuelekea Dar es Salaam na wale askari walishangaa utaratibu uliotaka kutumika wa kutekeleza kazi za kipolisi kupitia simu ya mtu waliyemkamata. Utafikiri hakuna mawasiliano rasmi ya Jeshi la Polisi,” kilisema chanzo chetu.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika mvutano wa kutaka gari hilo lifikishwe kituoni, askari hao walipokea amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi (OCD), SSP Majura ya kuwataka waliachie gari hilo, nao wafike kituoni kwa ajili ya kueleza sababu ya kulikamata.

Inaelezwa kuwa amri hiyo ya OCD ni agizo la Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Linus Sinzumwa anayedaiwa kuipokea kutoka kwa Kamanda Mpinga.

“Walipofika kwa OCD ikaamriwa wawekwe ndani na Koplo Azizi alipohoji sababu ya hatua hiyo alitakiwa afike kwa RPC na huko akawekwa ndani katika kituo cha Singida Mjini,” kiliongeza chanzo chetu.
Mtoa taarifa wetu alieleza kuwa baada ya hali hiyo, baadhi ya wananchi walimpigia simu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye alitoa agizo gari hilo likamatwe tena.
Aliongeza kuwa gari hilo lilikamatwa katika eneo la Manyoni na askari wa Maliasili kwa agizo la Nyalandu.

Kauli ya Mpinga
Kamanda Mpinga alipoulizwa kama alitoa amri ya kuachiwa kwa gari lile, alisema kwamba alipokea simu ya dereva kama anavyopokea simu za watu wengine.

Pia alikanusha madai ya kutoa amri ya askari hao kuwekwa ndani na kusema suala hilo aulizwe RPC wa Singida.
Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Sinzumwa alisema hakuna askari polisi aliyelikamata gari hilo bali lilikamatwa na watu wa KDU.

Aidha, aliongeza kuwa taarifa za kushikiliwa kwa askari ni uzushi wa baadhi ya watu wasiotaka mafanikio ya Jeshi la Polisi.
Wakati Sinzumwa akikanusha kumshikilia askari kutokana na tukio hilo, Tanzania Daima lilidokezwa kuwa alishikiliwa katika kituo cha Polisi cha Singida Mjini kwa kesi iliyoripotiwa juzi na kupewa namba 1231/2013.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu kwa simu ili athibitishe kama aliamrisha gari hilo likamatwe hakupokea kujibu hadi pale alipoandikiwa ujumbe mfupi.

“Tafadhali wasiliana na Bw. Mgoo, Afisa Mtendaji wa huduma za misitu, atakuambia, lakini ni kweli gari lilikamatwa Manyoni na bado liko kwa maafisa wa misitu huko,” alijibu Nyalandu kwa ujumbe wa simu.

Afisa mtendaji huyo alipotafutwa kwa simu, alikiri kuwa kuna gari walilikamata na lipo Manyoni. Kwamba maofisa wa misitu walilikamata kwa ajili ya kushughulikia kulipiga faini kwa kusafirisha mazao ya misitu usiku.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top