John Samwel Malecela
WAKATI Bunge likitaja wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kama vinara wa vurugu zilizosababisha kikao cha
Bunge kuvunjika wiki iliyopita, mkongwe wa siasa nchini, Samuel
Malecela, ameunga mkono msimamo wa wabunge hao na kukiri kwamba walikuwa
na haki ya kupiga kelele.
Malecela ambaye amepata kuwa Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM
taifa, alisema ni uonevu kwa Bunge kutaka kuwachukulia hatua kwa madai
ya kufanya vurugu.
Akitoa maoni yake kuhusiana na mwenendo wa siasa na uendeshaji wa
shughuli za Bunge akiwa nyumbani kwake mjini hapa, Malecela alisema ni
haki ya wapinzani kutoa hoja zao na kupiga kelele bungeni kutokana na
sheria ya kuwapo kwa vyama vingi.
“Wakati wa uanzishwaji wa vyama vingi, nilikuwa katika mchakato huo na
tulijua kuwa hayo ni lazima yawepo, kwa kufanya hivyo inaonesha wazi
kuwa ni wakati wa vyama vingi na ndiyo maana wakati mwingine wanafanya
mambo ambayo yanalenga kuishinikiza serikali kufanya mambo mbalimbali.
“Ikumbukwe kuwa maana ya kuwapo kwa vyama vingi ni tofauti na kuwapo
kwa chama kimoja, kama kingekuwapo chama kimoja ingekuwa sawa na
kuchezea mpira chini ya meza, kutokana na kuwapo kwa wabunge wa vyama
vingi ndiyo maana tunaona hali hiyo inayotafsiriwa kama fujo,” alisema.
Juzi Bunge liliwataja Mbunge John Mnyika (Ubungo), Joshua Nasari
(Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Mbunge wa Viti
Maalumu, Paulina Gekul kwamba ndio vinara wa vurugu bungeni, lakini
likashindwa kuwachukulia hatua.
Siri ya ripoti yafichuka
Wakati Malecela akitoa kauli hiyo, siri ya kile kilichotokea wakati wa kikao cha kamati ya kuchunguza vurugu hizo imefichuka.
Habari kutoka ndani ya Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge,
ambayo kabla ya kuvunjwa ilikuwa inaongozwa na Brigedia Mstaafu, Hassan
Ngwilizi, zilisema kuwa kulikuwa na mvutano mkubwa katika kushughulikia
suala hilo na matokeo yaliyotangazwa bungeni yana utata mkubwa.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa mvutano huo ulitokana na namna
ambavyo kamati hiyo ilivyofanya kazi ya kubaini wabunge waliohusika
kwenye vurugu hizo.
”Kwanza walichukua mikanda iliyorekodiwa na TBC, lakini siku hiyo
ilipiga picha za meza ya Spika tu. Picha za kamera za CCTV, zilionesha
wabunge wakiwasha vipaza sauti, lakini sauti hazisikiki.
“Hansard ilionesha majina ya wabunge hao wa CHADEMA na cha ajabu
hakuna hata mbunge mmoja wa CCM,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kibaya zaidi kamati hiyo haikuwaita wabunge hao kujitetea, lakini
ikaamua kuleta majina yao bungeni na kushindwa kuwachukulia hatua.
Februari 4, mwaka huu, Bunge la Kumi likiwa katika kikao chake cha
tano majira ya jioni palitokea vurugu kubwa ndani ya Bunge, hali
iliyosababisha Naibu Spika, Job Ndugai, kuliahirisha Bunge kwa siku
hiyo, zikiwa ni dakika chache tangu lilipoanza.
Kuahirishwa huko kulitokana na vitendo vya wabunge kupiga kelele
bungeni huku wakipinga kuwa hoja ya Mbunge wa Ubungo John Mnyika
(CHADEMA), ilitaka kuondolewa kwa ubabe.
Wabunge vinara
Miongoni mwa majina ambayo yalitajwa na Ngwilizi kuwa ni ndio vinara
wa vurugu hizo ni wabunge wa CHADEMA, John Mnyika (Ubungo), Joshua
Nasari (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Mbunge wa
Viti Maalumu, Paulina Gekul.
Mnyika: Kamati imebabaisha
Akizungumzia uamuzi wa kamati hiyo, John Mnyika, alisema imetoa
taarifa ya uchunguzi wa upande mmoja bila kuchunguza na kusikiliza
wahusika mbalimbali na kimsingi haijawahoji.
Mnyika alisema kilichofanywa na kamati hiyo ni ubabaishaji, kwa vile
kamati ilipewa hadidu rejea tatu; ya kwanza ikiwa ni chanzo cha vurugu,
lakini yenyewe ikadai ni tafsiri ya muda uliotumiwa na waziri, jambo
ambalo alisema ni uongo.
“ Chanzo ni ubishani kuhusu ukiukwaji wa kanuni uliofanywa na naibu
spika wa kumruhusu waziri kwa kutumia kanuni ya 57, 1, c, kuwasilisha
mabadiliko ya hoja ya kuingiza maneno ya kuondoa hoja ya msingi, uamuzi
ambao ni kinyume cha kanuni ya 57,4 ambayo inakataza kufanya mabadiliko
yanayopingana moja kwa moja na ile ya msingi.
“Na kanuni nyingine ya 58,5 inayosema mwenye mamlaka ya kuondoa hoja
ni mtoa hoja pekee kwa azimio la Bunge. Maana hata mtoa hoja
akishawasilisha hana idhini ya kuondoa bila ridhaa ya Bunge.
Nilipowasilisha hoja asubuhi, hata mimi mwenyewe ningetaka kuondoa
ilibidi niombe idhini ya Bunge. Hiki ndicho kiini kikuu cha ubishani
uliozuka na kimsingi tulitaka kanuni zifuatwe,” alisema Mnyika.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment