Na  Gideon   Mwakanosya, Songea.

Issa Mahyono (38) mkazi wa kijiji  cha Rwinga  wilaya ya Namtumbo  mkoani Ruvuma amefikishwa katika mahakama  ya hakimu  mkazi wa Mkoa wa Ruvuma akikabiliwa na  shitaka la kukutwa na meno 11 ya Tembo yenye uzito wa kilo 46.6 yenye thamani  ya shilingi milioni  38,893,800/=  ambayo ni mali ya serikali  kinyume cha sheria ya Nchi.


Mwendesha mashitaka  ambaye ni mwanasheria wa Serikali  kanda ya Songea Tulibake Juntwa alidai mahakamani hapo mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa  Casmiri Mwarunyungu  kuwa  Mahyono  anashitakiwa  kwa kukutwa na nyara za serikali kinyume na sheria za Nchi.



Alifafanua kuwa  inadaiwa  mnamo  Mei 20 mwaka huu  majira ya saa nne usiku  huko katika kijiji cha matepwende wilaya ya Namtumbo alikamatwa  na Askari Polisi ambao walishirikiani  na kikosi cha kuzuia ujangiri kanda ya kusini akiwa amebeba  meno 11 ya Tembo ambayo yalikuwa yakisafirishwa kwenda  Namtumbo mjini  tayari kwa kutaka kuyauza.



Juntwa alisema kuwa  Mahyono  alikutwa na nyara za serikali  zenye thamani 38,893,800 zilizokuwa na uzito wa kilo 46.6 na kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo huku akijua anavunja sheria.



Mwendesha mashitaka  Juntwa  ameiomba mahakama kuwa isitoe dhamana kwa mshitakiwa  kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba  akiwa nje ya dhamana  anaweza akavuruga  upelelezi.



Kwa upande wake  Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Mwarunyungu alisema kuwa dhamana ni haki ya mshitakiwa  hivyo alibainisha kuwa dhamana yake iko wazi ambayo  alipewa masherti ya dhamana awe na kiasi cha fedha tasilimu shilingi milioni kumi na tano na wadhamini wawili ambao watamdhamini kwa maandishi shilingi milionin kumi na tano kila mmoja.



Hata hivyo mshitakiwa mayono amekana mashitaka yanayomkabili na amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa mashariti aliyopewa ya dhamana  hadi juni  10 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.


MWISHO
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top