Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
SIKU moja baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kutangaza timu inayoundwa na kundi lake kuwania ukuu wa dola mwaka 2015, maswali yameibuka kuhusu uadilifu wa timu hiyo.

Juzi wakati akizungumza katika kongamano la Mawasiliano katika Nyanja ya Digitali la wanafunzi wa idara ya uhusiano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) jijini Mwanza, Sitta aliitaja timu hiyo inayoundwa na watu wanne kuwa mmoja wao atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Alisema wanaounda timu hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe.

Kutajwa kwa vigogo hao kumeibua maswali toka kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini, ambao wamechambua wasifu wa kila mmoja ikiwa ni pamoja na kupima utendaji na uadilifu wao kama wanafaa kupewa dhamana ya kuongoza nchi.
 
 
Sitta
Sitta ambaye kabla ya kuwa Waziri wa Afrika Mashariki, aliwahi kuwa Spika wa Bunge, baadhi ya wachambuzi wanamuelezea kuwa ni mwanasiasa mlafi wa madaraka, udhaifu ambao ulimsababishia afarakane na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Watu wanaomfahamu Sitta, wanadai kuwa udhaifu wake huo ndio uliomtuma ashiriki siasa chafu ambazo kwa kiasi kikubwa zilisababisha kukiathiri chama.

Sitta kwa kushirikiana na Dk. Mwakyembe, wanadaiwa kushiriki kuiua CCM kutokana na kutajwa kuwa nyuma ya mpango wa kuanzisha chama kingine cha siasa, Chama cha Jamii (CCJ), wakiwa bado CCM.

Inadaiwa kuwa uroho wa madaraka ulimsukuma Sitta kushiriki kuuaminisha umma alikuwa akipambana kuibadili CCM kutoka kwenye makucha ya matajiri na mafisadi wachache, akijipambanua kuwa ni mpambanaji wa ufisadi.

Ni katika msingi huo huo Spika Sitta aliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe kuchunguza uhalali wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ambayo ilimuondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Sitta akishirikiana na baadhi ya wanasiasa akiwemo Dk. Mwakyembe wanashutumiwa kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha ukuaji wa uchumi nchini, kutokana na hatua ya kushinikiza kutonunuliwa mitambo ya Dowans iliyorithi mkataba wa kampuni ya Richmond kwa madai kuwa ni ya kifisadi.

Ni tabia hiyo ya usaliti ya Sitta ndiyo inayoelezwa kuchagiza harakati zilizoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kumuondoa katika wadhifa wa uspika na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake Anne Makinda.

Wanaoamini hivyo, wanarejea taarifa zilizopata kuvuma pasipo yeye mwenyewe kuzitolea maelezo za kusudio lake la kutaka kujiunga na Chadema ili apate madaraka baada ya kufarakana na waliokuwa maswahiba wake wa kisiasa ndani ya CCM.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa baada ya kupima upepo wa kisiasa, Sitta alisitisha uamuzi huo wa kuhamia Chadema kabla chama chake hakijampooza na kumpa uwaziri, baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.

Akiwa Spika, Sitta pia aliwahi kukumbwa na kashfa ya ujenzi wa chini ya kiwango wa ukumbi wa Bunge jipya, bunge hilo lililojengwa kwa mabilioni ya fedha lakini sasa linavuja na ukaguzi umeonyesha kuwa halikujengwa kwa kiwango stahiki na hakuna mitambo ya usalama iliyofungwa ukumbini humo na wakati huo huo kupoteza nyaraka za jengo hilo ya michoro yake.

Ofisi ya Mbunge
Wanaompima Sitta kama anaweza kuongoza nchi, pia wanaliangalia Jimbo lake la Urambo aliloliongoza kwa takribani miaka 35, ambalo hadi leo linadaiwa kuwa liko nyuma kimaendeleo.

Ni kwa muktadha huo, baadhi ya wachambuzi wanahoji kama alishindwa kuliongoza jimbo lenye watu wachache na kulivusha kwenye maendeleo, je ataweza kuongoza nchi yenye watu zaidi ya milioni 40?

Pamoja na hilo pia anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kujenga ofisi ndogo ya Spika, ambayo yeye aliita ya Mbunge jimboni humo.

Ingawa Serikali iliridhia ofisi za wabunge zijengwe kwa kiasi cha fedha kisichozidi Sh milioni 40 kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha, ofisi hiyo ya Sitta jimboni Urambo, ilijengwa kwa Sh Milioni 350.

Wakati huo huo alikuwa akidaiwa kujitibu kwa gharama ya shilingi milioni mbili kwa kununua dawa za mamilioni ya fedha ili kutibu mguu, alizonunua katika moja ya duka la dawa jijini Dar es Salaam.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top