Jengo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
HATARI! Uwanja wa Ndege wa Mwanza si salama na unaweza kutumiwa na magaidi kama Al-Shabaab kuteka ndege na kuua watu  wakati  wowote, Risasi Jumamosi lina ushahidi mzito.
 
Upelelezi wa kina uliofanywa na gazeti hili bila kujulikana katika operesheni maalum iliyopewa jina la ‘HAKIKISHA NCHI SALAMA’, waandishi wetu waliokuwa jijini Mwanza walifanya jaribio la kutaka kuingiza bastola ndani ya ndege na kugundua ni jambo rahisi kuliko ilivyotarajiwa.

KILICHOGUNDULIWA
Katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa katika viwanja vyote Bongo, Uwanja wa Ndege wa Mwanza ndiyo rahisi kutumiwa na magaidi, hivyo kuna kila sababu ya mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kuchukua hatua ili kunusuru maisha ya abiria na watu wengine.

KAZI YA RISASI JUMAMOSI
Ni kawaida ya gazeti hili kufanya uchunguzi wa aina hii katika viwanja vya ndege na maeneo nyeti ili kuona kama hali ya ulinzi na usalama haiwezi kuruhusu vitendo vya kigaidi kufanyika.Miaka michache iliyopita, waandishi  wetu walifanya jaribio katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar na kufanikiwa kuingia na bastola hadi ndani ya uwanja karibu kabisa na ndege ya rais bila kugundulika pamoja na ukaguzi mkubwa uliofanyika wakati wa kuingia.

Kwa Mwanza, uchunguzi umeonesha kuwa uwanja huo una eneo moja  hatari ambalo mwenye nia ya kuingia na silaha ndani ya ndege anaweza kulitumia. Eneo hilo ni mlango uliopo kwenye jengo linalotazamana na  maegesho ya magari karibu na mlango wa VIP.
Ofisi za Uwanja wa Ndege wa Mwanza
ENEO LILIVYO
Mlango huo  wa kioo upo kwenye jengo jipya la kusubiri abiria kupanda ndege (waiting lounge), umeandikwa ‘EXIT’  ukimaanishani ni wa kutokea wakati wa dharura.

Uchunguzi wa gazeti hili umeonesha jengo hilo halina uzio wala ulinzi hivyo mtu yeyote anaweza kuufikia mlango huo bila kuulizwa na mtu yeyote.

Kibaya zaidi ni kwamba mtu yeyote aliye katika chumba hicho huwa tayari ameshafanyiwa ukaguzi wote na akitoka hapo ni kwenda moja kwa moja kwenye ndege tayari kwa safari.

Al-SHABAAB WANAWEZA KUINGIA NA SILAHA?
Historia inaonesha kuwa uwanja wa Mwanza ndiyo hupendelewa na magaidi kama Al Shabaab au watekaji wengine wa ndege.

Mwaka 1982 ndege aina ya Boeing 737-2R8C ilitekwa na vijana watano wa Kitanzania kutokea katika uwanja huo kwenda Dar lakini wao wakaipeleka jijini Nairobi, Kenya kisha Jeddah, Saudi Arabia na baadaye Athens, Ugiriki na mwishowe London, Uingereza.

Vijana hao walipofika London walitaka kuongea na mwanasiasa marehemu Oscar Nathaniel Kambona baadaye walijisalimisha kwa serikali ya nchi hiyo.

CHA KUJIFUNZA
Hata baada ya tukio hilo, serikali haikujifunza kwa lolote, hasa kuchukua tahadhari. Hilo limethibitika kwa ujenzi wa jengo hilo jipya likiwa na mlango wa kioo unaoelekea  kwenye maegesho ya magari bila uzio wowote.
Taswira ya uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kama magaidi wakitaka kuutumia uwanja huo, mmoja anaweza kukata tiketi za shirika la ndege ambalo hufanya safari zake kati ya Dar na Mwanza kisha kukaguliwa na kuingia hadi kwenye jengo hilo la kusubiria ambayo ndiyo sehemu ya mwisho kabla ya kuingia katika ndege.

Akiwa humo na wakati wa kuingia katika ndege ukifika anaweza kujichelewesha mpaka abiria wengine waende kupanga mstari kwenye mlango wa kuelekea kwenye ndege ambako hufanyika ukaguzi wa tiketi  tu.

Akiwa ameachwa peke yake, mmoja wa magaidi mwenye silaha anaweza kumiminia kioo cha mlango kemikali ambayo itasababisha kioo hicho kupukutika na hivyo kupenyeza bastola au silaha yoyote  na mwenzake kupokea kisha kwenda hadi kwenye ndege bila kukaguliwa kwa vile hakuna sehemu nyingine ya ukaguzi ukitokea kwenye eneo hilo.

KILICHOBAINIKA
Mchoro wa ukurasa wa mbele unaonesha kwa ufasaha ramani ya uwanja  wa Mwanza namna abiria wanavyoingia, kukaguliwa, kukaa mapumziko na baadaye kwenda kupanda ndege. Namba 1 kijani, abiria akiwasili uwanjani hapo.

Namba 2, abiria akipita geti kwa ukaguzi wa awali kisha kuingia ndani ya ofisi ya ukaguzi.

Namba 3 kijani, abiria akifika kwenye eneo rasmi la kukagulia mizigo na vitu vingine vyenye uwezo wa kuhatarisha usalama wa ndege na abiria wake.
Moja ya kikosi cha Al-Shabaab wanaoweza kuzua mashambulizi ya kigaidi.
Namba 4 kijani, abiria akitoka kukaguliwa ili kwenda kujipumzisha kwenye chumba maalum kwa ajili ya kusubiri tangazo la kuingia kwenye ndege tayari kwa safari.Risasi Jumamosi lilibaini kuwa, mlango ulio nje unaoweza kumruhusu gaidi kuingia eneo la abiria wanaosubiri ndege bila kupita kwenye utaratibu wa kukaguliwa. Huu mlango ndiyo tatizo kubwa katika uwanja huo.

ILIPO HATARI YENYEWE
Ukiangalia mchoro ukurasa wa mbele, namba 1 mwekundu ni gaidi akiwasili kwenye uwanja huo kwa ajili ya kufanya uhalifu wowote.
Namba 2 nyekundu, gaidi akifika kwenye mlango huo ambao anaweza kumfikishia salaha mwenzake kwenye chumba maalum cha abiria waliokwisha kaguliwa na kusubiri ndege.

Namba 3 nyekundu, gaidi akiwa amepokea silaha na kuungana na abiria ambao wameshakaguliwa wakisubiri kwenda uwanjani tayari kwa safari.

Namba 4 nyekundu, gaidi akiungana na abiria wengine kwenda uwanjani ambako atakuwa amefanikiwa kuingia kwenye ndege na silaha hiyo.

MFANYAKAZI AZUNGUMZA
Baada ya uchunguzi kukamilika, waandishi wetu waliokuwa safarini kurejea Dar toka Mwanza kikazi walizungumza na mmoja wa wafanyakazi wa ndege kuhusu  mlango huo na kwa mara  ya kwanza alionesha kubaini tatizo hilio na kusema:

“Nitawasiliana na viongozi wa  juu wa uwanja ili hatua za haraka zifanyike kuziba mlango huu kabla haijatokea  hatari.”

Risasi Jumamosi linaendelea na jitihada za kumtafuta Waziri wa Uchukuzi, Harrison George Mwakyembe ili kuzungumzia hali hiyo baada ya kumkosa hewani juzi.
GPL 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top