Jaji Joseph Warioba 
Jaji Joseph Warioba
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hali ya mambo yanayoendelea bungeni mjini Dodoma, haoni matumaini ya kupatikana Katiba mpya na hali hiyo imemkatisha tamaa.
 
Wakati Jaji Warioba akikatishwa tamaa na uwezekano wa kupatikana Katiba mpya, Mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini, Prof. Chris Maina, ameeleza kuwa watu wanaotaka kuzuia historia kuandikwa kwa kutumia askari wa kutuliza ghasia, hawatafanikiwa kwani historia itawaumbua.

Jaji Warioba na Prof. Maina, walitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Dk. Sengondo Mvungi, pamoja na hafla ya kutimiza miaka 19 ya kuanzishwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Katika matukio hayo mawili yaliyoendana na uzinduzi wa kitabu cha historia ya maisha ya Dk. Mvungi, Jaji Warioba alisema, tangu mwanzo matumaini yalikuwa ni nchi kupata Katiba mpya kwa maridhiano na kwamba baada ya mchakato huo kutekwa na wanasiasa, matumaini hayo yametoweka.

Alisema, badala yake wanasiasa hao wameacha kuangalia maslahi ya taifa na kutegemea uamuzi wa kura badala ya nafasi ya maridhiano kupewa kipaumbele.

“Sina hakika kama tutapata Katiba mpya, kwani rasimu itakayopendekezwa na Bunge Maalum haitapigiwa kura hadi mwaka 2016, kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema na kuongeza.

Kampeni ya uchaguzi mwakani, Katiba mpya itakuwa ajenda inayoweza kuigawa nchi.

Akizungumzia rasimu iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba, Jaji Warioba alisema limecha maoni yaliyotolewa na wananchi na kuweka yak wake, jambo ambalo ni hatari.

Jaji Warioba, alisema licha ya baadhi ya mambo kuonekana kukubaliwa katika rasimu hiyo, bado yako mengi ya msingi yamewekwa pembeni na kwamba, wabunge waliopitisha uamuzi huo wanapaswa kutoa maelezo ya kutosha kwa wananchi.

Aliyataja baadhi ya mambo ambayo mwelekeo wake ni kukataliwa na wananchi, ni pamoja maadili ya viongozi.

“Katika maadili ya viongozi, wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi, kwa kuwa wanachukizwa na kuporomoka kwa maadili,” alisema.

Kutokana na maoni ya wananchi, Jaji Warioba alisema Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika utangulizi wa rasimu, ambako misingi katika Katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani, lakini kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa nayo ni pamoja na utu, usawa, umoja na mshikamamo.
Aliongeza kuwa, wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye Katiba, ambazo ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa ya Kiswahili.

Hata hivyo, Jaji Warioba alisema ni jambo la kusikitisha Bunge Maalum limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora na kuongeza kuwa, kila mtanzania anapaswa awe na tunu hizo.

Madaraka ya wananchi
Kuhusu madaraka ya wananchi, alisema Katiba inatungwa na wananchi na kwa maoni yao, wanataka wawe na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhiki na uwakilishi wake.
Akilifafanua hilo, alisema ni kweli siyo jambo la kawaida kumwondoa mbunge katikati ya kipindi au kumwekea ukomo, lakini kwa sababu ya rushwa katika uchaguzi, wananchi wanaona ni vema watumie madaraka yao kuwajibisha wabunge wao.

Katika hilo, alisema inawekana kwa kuwa tayari Bunge lina kanuni za kuwajibisha wabunge, vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa, vivyo hivyo wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo.

Mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili
Jaji Warioba, alisema pendekezo la kumwondoa Rais na Mawaziri kutoka kwenye Bunge, limekataliwa kwa sababu kumezoeleka mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi za Jumuiya ya Madola.
“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge, kwani kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji bali madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu, ambaye ni mbunge na hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia na New Zealand.

“Ikumbukwe kwamba, Tanzania ina mfumo wa urais, ambapo Rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu, Amiri Jeshi Mkuu, hivyo Rais na Mawaziri wake kuwa sehemu ya Bunge ni kuchanganya mamlaka, ambapo hali hii ndio inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya Bunge na pia Bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema na kuongeza.
Tumeona wakati mchakato huu wa Katiba jinsi madaraka yanavyoingiliana, ambapo wakati wa kutunga sheria ya mabadiliko ya Katiba, tuliona jinsi Bunge lilivyokuwa linafanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kutunga sheria.

“Lakini baadaye Rais anafanya mazungumzo na watu nje ya Bunge na baadaye Bunge linalazimika kubadili maamuzi ambako hata Bunge Maalum la Katiba limetendewa hivyo… kwa maana hiyo, Bunge halina madaraka kamili na Rais anaweza kuingilia wakati wowote,” alisema.

Alisema, katika Bunge la kawaida mawaziri wanawabana wabunge kupitisha mambo ya Serikali na wabunge mara nyingine wanaingilia kazi za Serikali, kwa mfano Kamati za Bunge kwenda moja kwa moja kwenye taasisi za Serikali kutoa maagizo au maazimio kwenye maeneo ya utendaji.

Hivyo, anachoona dhana ya kutenganisha madaraka ya mhimili ni jambo la msingi sana katika mfumo wa demokrasia na nchi nyingi zimebadili Katiba ili kufanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.

Muundo wa Muungano
Katika suala la Muungano ambalo ndilo limeteka nafasi kubwa ya majadiliano tangu mchakato huo uanze, Warioba alisema pamoja na Tume kuorodhesha kero zaidi ya 40, baada ya uchambuzi wa kina ilionekana kero nyingi ama zimepatiwa ufumbuzi au zinaweza kurekebishwa na tume ilichambua tu zile ambazo zilionekana ni nzito.

Alibainisha kuwa, lalamiko kubwa kwa upande wa Tanzania Bara ni Zanzibar kuvunja Katiba ya Muungano, ambako alihoji kuwa kutokana na yale yaliyopitishwa na Bunge la sasa ni kweli Zanzibar itakubali sheria zinazotungwa na Bunge kutumika nchi nzima bila masharti.

“Swali lingine ni kama kweli Zanzibar imekubali Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu ziwe mamlaka nchi nzima bila masharti, itakubali kuondoa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010 na suala la Bunge kupendekeza kwamba raia awe na haki kupata ardhi. Je Zanzibar wamekubali raia wote wawe na haki hiyo kwa upande wa Zanzibar,” alihoji.

Awasubiri wabunge mitaani
Kuhusu shutuma mbalimbali zilizoelekezwa na wajumbe wa Bunge Maalum kwa wajumbe wa Tume ya iliyokuwa ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema baada ya wajumbe hao kumaliza kuongea katika vipaza sauti vya Bunge, wanapaswa kutambua kuwa wanawasubiri mitaani.

“Wao wanasema Jaji Warioba na wajumbe wenzake ni ‘Shiidaah’ tena wanasema Warioba ni shida kubwa, mimi nawaambia wanakaribia kuacha vipaza sauti vya Bunge waje huku mitaani wawaeleze wananchi yale waliyopitisha na sisi tutabaki katika msimamo wa kutetea maoni ya wananchi, hapo ndipo watakapojua kama walio na shida ni sisi au wao,” alisema.

Maina aonya nguvu za FFU
Kwa upande wake, Prof. Maina, alisema kwa jinsi nchi inavyoshuhudia vioja vya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ndiyo umuhimu wa tume iliyoongozwa na Jaji Warioba unavyoendelea kujidhihirisha.

Alisema, wanaoipinga rasimu ya pili ya Katiba wanaushangaza umma wa Watanzania kwa kueleza kuwa wabunge 75 ni mzigo kwa serikali huku wakishindwa kuainisha wingi wa kuwa na wabunge 360 na gharama zake.

“Leo wanaposema wabunge 75 ni gharama kuliko 360 hauwezi kuwaelewa, wanaposema mawaziri 15 ni gharama zaidi ya 60 pia hatuwaelewi na hawa wanataka kuficha historia na katika hili… wanadiriki kutumia FFU lakini hawajui kuwa historia haifichwi na ina kawaida ya kuumbua na itawaumbua hata wakiwa bado hai,” alisema Profesa Maina.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top