Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul 'Diamond'.
STAA wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul
‘Diamond’, Alhamisi iliyopita alijikuta akiutibua msafara wa Rais wa
Zanzibar, Dk. Mohamed Shein kufuatia kuondoka kwenye msiba wakati
ilitangazwa kiongozi huyo ndiye aliyetakiwa kuanza kuondoka.
Ishu hiyo iliyotafsiriwa kama jeuri ya staa huyo ilitokea Mbuzini
Mjini Magharibi, Zanzibar baada ya kumalizika kwa mazishi ya baba wa
Wema Sepetu, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania Urusi, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na Waziri wa Elimu wa zamani katika Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Isaac Abraham Sepetu.
Awali, wakati waombolezaji
wamekaa wakiusubiri mwili wa marehemu ufike, ghafla Diamond aliibuka
akisindikizwa na kundi la wapambe mpaka alipokaa.
Diamond akiwa mstari wa mbele wakati wa mazishi ya Balozi Sepetu.
Diamond alipofika aliwekwa mstari wa mbele ambako walikaa ndugu wa karibu na watoto wote wa marehemu
Mwili ulipowasili, ratiba ya mazishi ikatangazwa na MC ambapo alitaja
utaratibu wa mazishi mpaka watu watakaotakiwa kuweka mashada ya maua
kaburini, akiwemo Rais Shein.
Baada ya mazishi, Mwongoza Shughuli ambaye jina halikujulikana
aliwaomba watu wote wazingatie itifaki ya usalama wa taifa kwamba ni
lazima viongozi wote wa serikali waondoke ndipo waombolezaji wengine
watawanyike.
“Jamani naomba sana itifaki izingatiwe, asiondoke mtu yeyote kabla ya
viongozi wetu wa serikali, akiwemo Rais Shein hawajaondoka,” alisema MC
huyo.
Baada ya MC huyo kutoa mwongozo, watu wote walitulia wakisubiri kiongozi wa kwanza kuondoka ambaye alikuwa ni Rais Shein kama itifaki ilivyotaka.
Lakini kabla Rais Shein hajaanza kusimama, Diamond alinyanyuka na
kuzua kasheshe kwa sababu baadhi ya watu, hasa wa umri wake walianza
kumkimbilia huku wakikanyagana na kusababisha hali ya taharuki.
Baada ya watu kuanza kukimbizana hovyo muongozaji wa msiba huo aliwaomba watulie na kusema kuwa wasiogope ila kuna staa ambaye anapita ndiyo maana watu wamemkimbilia.
“Naomba utulivu huyo ni staa f’lani kapita huko ndiyo maana watu
wanamkimbilia hivyo tulieni kwanza viongozi wetu waondoke,” alisema.
Rais Shein akiweka udongo katika kaburi la Balozi Sepetu.
Baada ya kuona watu wakikimbia hovyo baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa walitaka kumkamata msanii huyo wakisema alisimama kwa makusudi licha ya kusikia tangazo la kiitifaki.
Baadhi ya watu waliohudhuria msiba huo walionekana kushangazwa na kitendo cha Diamond na kusema kuwa ni vyema angesubiri viongozi wote waondoke ndipo na yeye atimke lakini kufanya vile si sahihi.
“Huyu Diamond kwani ana nini? Nakumbuka kwenye msiba wa Kanumba kule
Dar pia aliingia kipindi ambacho ilitangazwa kuna kiongozi anakwenda,
utaratibu ukatibuka, watu wakawa wanamshangilia yeye,” alisema mtu mmoja
aliyetoka Dar kwenda Zanzibar kumzika mzee Sepetu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment