Samuel Sitta
Na Josephat Isango
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda na
Naibu Spika, Job Ndugai, wanasemekana kutumiwa na maadui wa demokrasia
na mafisadi kummaliza kabisa aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta
na kundi lake.
Habari za kuaminika kutoka vyanzo mbalimbali zimebainisha kuwa kile
kilichotokea bungeni na kusimamiwa kikamilifu na Makinda ulikuwa ni
utekelezaji wa matakwa ya wanasiasa na viongozi kadhaa wenye nguvu za
fedha ambao waliumizwa vibaya na aina ya uongozi na maamuzi ya Sitta
alipokuwa akikalia kiti hicho.
Inadaiwa kwamba mbali na kumkomoa, Makinda pia ameelekezwa kuhakikisha
kuwa Sitta anamalizwa kisiasa, kwa kuwasulubu pia wabunge waliokuwa
wakimuunga mkono, wakiwamo wale wa vyama vya upinzani hususan wa
CHADEMA.
Moja ya chanzo chetu cha habari kimesema kuwa wanasiasa hao wakiwamo
watendaji kadhaa wa serikali, walichukizwa na msimamo wa Sitta, hasa
kusimamia ukweli na haki, na kuonekana kuwapendelea zaidi wabunge wa
upinzani kuliko wale wa CCM.
Katika mkakati huo, iliamriwa kuwa nguvu zote alizotumia Sitta
kuisulubu serikali na wanasiasa walioguswa masilahi yao, zivunjwe,
likiwamo suala la kuunda na kuunganisha kamati ya hesabu za mashirika ya
umma, na ya hesabu za serikali kuwa pamoja, kisha kuhakikisha
inaongozwa na mbunge kutoka chama tawala.
Mbali na mipango hiyo, chanzo chetu kimesema kuwa mabadiliko hayo ya
kamati yamefanywa kutokana na hofu ya kuumbuka kwa serikali kutokana na
matumizi mabaya ya fedha, ikiwa kamati hizo zitaendelea kuwa chini ya
wapinzani.
Katika mpango huo, Naibu Spika Ndugai, amejikuta akilazimika
kukubaliana na maagizo ya mkuu wake wa kazi, licha ya ukweli kwamba
ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa katika Bunge la
Tisa lililoongozwa na Sitta, ikiwa na lengo la kuleta mfumo mzuri wa
utendaji wa Bunge, ikiwa ni pamoja na kurejesha hadhi yake ya
kuiwajibisha serikali.
Ndugai katika kukamilisha azima ya Sitta, alilazimika na kamati yake
iliyoundwa na wabunge wengine, Dk. Harrison Mwakyembe, Nimrod Mkono,
Beatrice Shelukindo, Dk. Willibrod Slaa na Hamadi Rashid Mohamed,
ilifanya ziara katika Bunge la Kenya, Uganda, India, Mauritius na
Zimbabwe.
Kutokana na ziara hizo za mafunzo, Ndugai na kamati yake walipendekeza
kutungwa kwa mambo yatakayolifanya Bunge lisimamie masilahi ya taifa
badala ya vyama, vikao vyake kuoneshwa wazi kwa njia ya runinga ili
wananchi waone na ripoti za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali
zijadiliwe na Bunge pamoja na kuondoa miswada yoyote iliyokuwa inaletwa
kwa dharura bungeni.
Ni kamati ya Ndugai ndiyo ilipendekeza kuwa Kamati ya Mashirika ya
Umma, (POAC), Kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC) ziongozwe na upinzani ili kuongeza uwajibikaji wa
serikali kwa Bunge.
Mbunge mmoja wa CCM ambaye amekuwa bungeni kwa muda mrefu (jina
linahifadhiwa) alikiri kusikitishwa na uamuzi wa Spika Makinda, na
kuonesha hofu ya kuvunjika kwa heshima na hadhi ya Bunge.
“Inasikitisha sana, maana sasa tunaelekea kuvunja hadhi ya Bunge na kulinda uozo wa serikali.
“Katika Bunge la Tisa, Sitta alijitahidi kuwa jasiri, kutopindisha
ukweli ili kuilinda serikali, na alizielewa vizuri kanuni hasa ile ya 8
inayosema: “Hata kama Spika ametoka katika chama fulani anapaswa atende
haki kwa pande zote,” alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema vurugu zilizotokea bungeni zilitokana na maamuzi
mabaya ya kiti cha Spika, kinyume kabisa cha hotuba yake ya kwanza
alipochaguliwa kushika wadhifa huo ya kuliunganisha Bunge kuwa moja.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu, mmoja wa
wajumbe wa iliyokuwa kamati ya Ndugai, Nimrodi Mkono, alisema hawezi
kusema lolote kuhusiana na kuondolewa kwa kamati hizo, ingawa alikiri
kuwa walichokishauri na kukubaliwa na Bunge kilikuwa cha maana na
manufaa kwa taifa.
Kuhusiana na vurugu zilizotokea, Mkono alisema kelele za wapinzani
zilikuwa sahihi hasa baada ya kuona kuwa wanaonewa, kutokana na uchache
wao, hivyo kulazimika kupiga kelele ili hoja zao zisikiwe na Watanzania.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alishangaa kuunganishwa kwa
Kamati ya Mashirika ya Umma pamoja na ile ya Hesabu za Serikali, huku
akihoji kama Spika na wabunge wa CCM wapo tayari kuwa na mwenyekiti wa
Kamati ya Bajeti kutoka upinzani.
Akihojiwa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, kiongozi mmoja
mashuhuri hapa nchini, amelaani aliouita uendeshaji mbovu wa shughuli za
Bunge, na kuongeza kuwa kumetokana na udhaifu wa serikali yenye wabunge
wasiojali masilahi ya taifa.
Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa kauli ya hivi karibuni ya Makinda
wakati akitoa maoni mbele ya wajumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya
Katiba, ya kutaka Spika atoke nje ya chama, ilionesha kuwa huenda hata
yeye analazimika kutekeleza maagizo na maelekezo ya chama na serikali
yake hata kama hayataki.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment